Skip to main content

Dhana ya utafiti.

UTAFITI ni uchunguzi wa asili wenye mpangilio unaofanywa ili kuongeza ujuzi na uelewa kuhusu jambo au tukio lolote liwalo. Aghalabu hutumika katika kuhakiki ukweli wa mambo na desturi.
Vilevile, utafiti hutekelezwa ili kutoa matazamo mpya kuhusu suala linalosibu jamii na kuvumbua vifaa vipya na utaratibu mpya katika kufanyia jambo husika.

Hii ni kwa sababu utafiti kulenga kuboresha maarifa na ujuzi wa binadamu kwa kuibua mitindo mipya ya kuelewa dhana mpya katika jamii. Ukuzaji wa maarifa haya hatimaye hufanikisha uwezo wa kudhibiti na kubashiri hali fulani.
Utafiti mzuri unapofanywa, mara nyingi unatarajiwa pawepo na ulazima wa matokeo yanayokuza maarifa au elimu katika mada inayochunguzwa.
Utafiti mwingine hukusudia kuzaa nadharia ambazo hufaidi chunguzi nyingine za kitaalamu wa matukio fulani yaliyotangulia.
Hivyo kwa maneno mengine, utafiti ni ari iliyorasimishwa na yenye mpango uliokubalika. Ni zoezi la kuchunguza suala lolote kwa lengo fulani maalum (Hurston, 1957).
Gyorgyi (1928), anasema kwamba dhana 'utafiti’ ni faridi inayomwezesha mchunguzi kubaini kile ambacho mtu yeyote mwingine hajafaulu kukiona na kuwazia yale yote ambayo hakuna hayajawahi kufikiriwa. Ahahoji kwamba utafiti ndio msingi wa sayansi yoyote ile.
Utafiti hufanywa ili kutafuta ujuzi au elimu na hufanya  majukumu haya mawili kwa njia ya uwazi na isiyo ya kibinafsi ili kuthibitisha jambo fulani mahsusi.
Ni njia yenye mpango itumikayo kukusanya na kufafanua habari ili kuongeza uelewa wa tukio au matukio yanayochunguzwa kitaaluma. Utafiti wowote ule hulenga kugundua na kurejelea ujuzi na maarifa ya binadamu kuhusu matukio fulani muhimu katika jamii.
Ni njia za kubuni habari au elimu mpya katika nyanja nyinginezo mahsusi ambazo zinahusu jamii na kuiathiri kwa njia moja au nyingine.
Kutafiti aghalabu hutegemezwa kwenye madhumuni ambayo huwa ni kupata majibu kwa maswali mbalimbali kwa kutumia mbinu za kisayansi. Kwa hivyo, kila utafiti huwa na malengo yake ambayo hukusudiwa kuafikiwa kwa kushirikisha mbinu na aina tofauti za utafiti.
Haja ya kutaka kupata maarifa (yenye uhakika) husababisha kuwepo na namna fulani tofauti za utafiti. Mara nyingine utafiti unaweza kufanywa ili kupata ufahamu wa tukio au mtazamo mpya kuhusu tukio fulani.
Aina hii ya utafiti huwa ni utafiti wa kutalii. Utafiti wa kiufafanuzi huazimia kuonyesha kwa usahihi sifa za mtu, kitu, hali au kundi fulani. Kunao utafiti mwingine ambao huongozwa na dhamira ya kuelewa kiasi ambacho jambo fulani hujitokeza.
Utafiti wa kupima haipothesia hufanywa ili kupima uhusiano kati ya mambo mbalimbali katika mazingira husika.Ieleweke kwamba kila mara utafiti wowote unapofanywa, ni muhimu kwa utaratibu mwafaka kuzingatiwa.
Itifaki na utaratibu huu huweza kuonyesha utafiti unahusu nini, sababu za utafiti wenyewe, mahali pa kufanyiwa utafiti, mbinu za kukusanyia data na muda ambao utahitajika katika kukusanya data inayohusiana na mada ya utafiti.
Aidha, ni vyema kubainisha aina ya data itakayokusanywa na pale ambapo data hiyo itapatikana. Utaratibu huu hubainisha aina ya sampuli itakayotumiwa na mtafiti pamoja na jinsi ambavyo data iliyokusanywa itachanganuliwa na namna ya kuwasilisha matokeo ya utafiti.
Hatua hizi zote ni muhimu hasa ikizingatiwa kwamba hulenga kupunguza gharama, upotezaji wakati na kuhakikisha kwamba data sahihi na inayokusudiwa inapatikana hatimaye.
Mbinu ya kimamlaka ilirejelewa sana katika miaka ya awali kama njia ya kimsingi katika kusuluhisha matatizo ya jamii. Wazee walishauriwa kutoa suluhu kwa misingi ya umri, dini au maelezo ya kiukoo. Ingawa mbinu hii inaweza kutumika kwa namna nyingi, inahitaji umakini fulani na namna fulani ya kuthibitisha uhakika wa maelezo husika.
Njia ya kitamaduni ilitumika wakati utafiti fulani ulilenga jamii fulani mahsusi. Kwa mfano, mtafiti wa kianthropolojia na kisaikolojia hujikita katika utamaduni ili kuweza kuvumbua ukwei wa jambo fulani lenye utata.
Kwa kupitia mbinu hii, mambo kuhusu vyakula, mavazi, mazungumzo na imani za kidini yalirejelewa kwa kina ili kueleza mabadiliko mbalimbali yanayoshuhudiwa na jamii.
Mbinu nyingine ilihusu maarifa yanayotokana na ujuzi wa mtu binafsi. Ingawa hivyo, matatizo katika njia hii yalikuwa kwamba iliweza kutupilia mbali maoni, mawazo au fikira ambazo zinaelekea kutofanana au kutopatana na za mtu binafsi, hivyo matokeo yakaegemezwa katika upande mmoja tu.
Mambo muhimu yanapopuuzwa basi ina maana kwamba matokeo ya utafiti huenda yasiwe kamilifu kutokana na kushindwa kuchukua mtazamo kamilifu.
Ingawa wanafalsafa wa zamani waliasisi mbinu za mantiki-mkato (deductive reasoning) na mantiki-dukizi (inductive reasoning) katika utafiti, kadri ya mabadiliko ya vipindi vya wakati, mbinu za kisayansi zimeaminiwa zaidi katika kufanikisha utafiti kwa kuwa zinahimiza matumizi ya nadharia katika kuelezea chimbuko na asili ya kila kinachotafitiwa.
Msingi wa njia hii katika kujumuisha mbinu mbalimbali na kufuata mantiki fulani maalum katika kukusanya, kuchanganua na kuwasilisha data. Hivyo, hutuwezesha kuafikia uamuzi wenye mielekeo bora na mashiko kamili yanayoweza kuthibitishwa.

Comments

Popular posts from this blog

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI

Ushairi kama moja kati ya tanzu za fasihi inayowasilishwa katika namna zote aidha kwa lugha ya maandishi au kwa lugha ya masimulizi una mchango au nafasi kubwa sana katika kunufaisha au kustawisha maisha ya binadamu kwa kumuelimisha, kumsisimua, kutunza na kuhifadhi amali zake pamoja na kukuza na kuendeleza lugha yake kama moja kati ya vipengere muhimu maishani mwake. Ushairi kama nudhumu katika fasihi simulizi hujumuisha nyimbo, ngonjera, tenzi na mashairi yenyewe. Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au katika kumbo mbalimbli kama asemavyo Mulokozi (1996) kuwa zipo kumbo kuu tatu ambazo ni ushairi wa kijadi au kimapokeo, ushairi wa mlegezo au huru na ushairi wa maigizo. Wanazuoni wafuatao wa mashairi ya kimapokeo wametoa maana za ushairi kama ifuatavyo:- Shaaban Robert (1958:37). “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari…, mawazo, maoni na fikra za ndani zi...

MBINU ZA KUFUNDISHIA

Mbinu za kufundishia , ni miongozo mbalimbali atumiayo mwalimu wakati wa kufundisha somo aliloliandaa kwa wanafunzi wake. Walimu wanapaswa kuamua kwa kuchagua kwa makini njia na mbinu bora za kufundishia ili wanafunzi wake waweze kujifunza kwa ufanisi. Ziko njia nyingi za kutengeneza mazingira ya mtoto aweze kujifunza na pia ziko mbinu nyingi za kufundishia. Pamoja na wingi huo tunaweza kuzigawa katika makundi makuu mawili kadri ya jinsi zinavyowashirikisha watoto katika tendo la kujifunza, ambazo tunaweza kuziita shirikishi na zisizo shirikishi . Zifuatazo ni baadhi ya mbinu shirikishi na zisizo shirikishi za kufundishia pamoja na faida na hasara zake:- Njia ya majadiliano , njia hii imekuwa ikitumika katika ufundishaji kwa muda mrefu. Katika kujadiliana mwanafunzi mmoja mmoja hupata nafasi ya mawazo aliyonayo kuhusu suala linalojadiliwa na yeye pia huweza kupata mawazo yaw engine. Katika majadiliano mwanafunzi hupata ujuzi mpya nje na ule aliokuwa nao kabla hajashiriki kat...

DHANA YA MATUMIZI YA LUGHA, REJESTA, UTATA

Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika. Katika mada hii utajifunza mambo ya msingi ya kuzingatia unapotumia lugha. Utaelewa dhana mbalimbali zinazohusishwa na matumizi ya lugha kama vile rejesta, misimu, utatata katika lugha, lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi. Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika. Dhima ya matumizi ya lugha Dhima kuu ya lugha ni kupashana habari, ujuzi na maarifa mbalimbali. Vilevile lugha husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu. Uhusiano huo unaweza kuwa wa kijamii, kielimu, kibiashara, kihuduma, kisiasa, kiuchumi n.k. Kwa hiyo, kujua jinsi ya kuitumia lugha kama inavyotakiwa, kunasaidia kufikisha vizuri ujumbe unaotakiwa bila kuupotosha. Vilevile kunasaidia kuepuka migongano, hasa ya kijamii kwa kuwa utakuwa umetumia lugha kwa mujibu wa mi...