Skip to main content

SHAIRI: KWAKO MWANANGU MPENDWA


Naandika kwa furaha,furaha ya kuwa nawe,
Nataka upate raha,usilie juu ya mawe,
Upendo na uwe silaha,pendo lako uligawe,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.



Usiyashike maneno,kukashfu ulimwengu,
Ukaja yaficha meno,kuhofu ya walimwengu,
Ulishike langu neno,siogope ulimwengu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Mama na babako tupo,twakuombea kwa Mungu,
Hata ikiwa hatupo,usiuote uchungu,
Na wema wa Mungu upo,wastahili lako fungu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Brigita na Anita, majina tuu mwanangu,
Vyovyote tungekuita,hata jina la mamangu,
Majina ni ya kupita,hayo ni chaguo langu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Usihofu ufukara,hicho ni kitu kidogo,
Ni akili pia busara,hutochukia mihogo,
Mwanangu kugangamara,si kutwa kupiga zogo,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Usiisake sababu,ya kuukosa ukapa,
Sijui tangu mababu,ufukara upo hapa,
Kujituma ni jawabu,kweli hutotoka kapa,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Pia usijidanganye,utaupata kwa mume,
Ukwasi akunyang'anye,moyo uje ukuume,
Mwanangu kutwa uhanye,matunda uje uchume,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Alice kipenzi changu,wewe ni faraja yangu,
Nimekupa damu yangu,umebeba sura yangu,
Faraja ya mke wangu,twasema asante Mungu,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Utapata marafiki,pia hata maadui,
Pia kuna wanafiki,ambao huwatambui,
Uwe rafiki wa dhiki,upendo haubagui,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Kuna nyakati za dhiki,zisikutoe akili,
Kufuru usidiriki,muhimu kustahimili,
Hiyo mikiki mikiki,isije haribu mwili,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Wana maneno matamu,kutaka kukupoteza,
Wakikidhi zao hamu,ubaki kuomboleza,
Rahisi kuwafahamu,mama atakueleza,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Wengi wanaharibiwa,kila iitwayo leo,
Wengi wanajaribiwa,kwa maneno na vileo,
Akili za kuambiwa,zisije kupa vimeo,
Kwako mwanangu kipenzi,dunia mahali pema.


Mama msikize sana,atakushauri mengi,
Usiwaze kugombana,hekima iwe msingi,
Hakutokuwa na mana,ukimwekea vigingi,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Mungu muweza wa yote,mshukuru muamini,
Simwache siku yoyote,sipaparikie dini,
Siwaze kuwa Dangote,bila Mungu kuamini,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Malezi ni kazi ngumu,ya akili siyo mwili,
Usiongeze ugumu,ukiutumikia mwili,
Ukaja tamani sumu,ukaharibu akili,
Kwako mwanangu kipenzi,dunia mahali pema.


Mheshimu kila mtu,tajiri na hoe hae,
Ila uthamini utu,utu pipa ujae,
Ila usije thubutu,madume yakuhadae,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.


Dunia mahali pema,kila mtu na riziki,
Waza kuyatenda mema,na usiwe mzandiki,
Nikifa ‘talala vyema,Mungu ukimsadiki,
Kwako mwanangu mpenzi,dunia mahali pema.

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI

Ushairi kama moja kati ya tanzu za fasihi inayowasilishwa katika namna zote aidha kwa lugha ya maandishi au kwa lugha ya masimulizi una mchango au nafasi kubwa sana katika kunufaisha au kustawisha maisha ya binadamu kwa kumuelimisha, kumsisimua, kutunza na kuhifadhi amali zake pamoja na kukuza na kuendeleza lugha yake kama moja kati ya vipengere muhimu maishani mwake. Ushairi kama nudhumu katika fasihi simulizi hujumuisha nyimbo, ngonjera, tenzi na mashairi yenyewe. Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au katika kumbo mbalimbli kama asemavyo Mulokozi (1996) kuwa zipo kumbo kuu tatu ambazo ni ushairi wa kijadi au kimapokeo, ushairi wa mlegezo au huru na ushairi wa maigizo. Wanazuoni wafuatao wa mashairi ya kimapokeo wametoa maana za ushairi kama ifuatavyo:- Shaaban Robert (1958:37). “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari…, mawazo, maoni na fikra za ndani zi...

MBINU ZA KUFUNDISHIA

Mbinu za kufundishia , ni miongozo mbalimbali atumiayo mwalimu wakati wa kufundisha somo aliloliandaa kwa wanafunzi wake. Walimu wanapaswa kuamua kwa kuchagua kwa makini njia na mbinu bora za kufundishia ili wanafunzi wake waweze kujifunza kwa ufanisi. Ziko njia nyingi za kutengeneza mazingira ya mtoto aweze kujifunza na pia ziko mbinu nyingi za kufundishia. Pamoja na wingi huo tunaweza kuzigawa katika makundi makuu mawili kadri ya jinsi zinavyowashirikisha watoto katika tendo la kujifunza, ambazo tunaweza kuziita shirikishi na zisizo shirikishi . Zifuatazo ni baadhi ya mbinu shirikishi na zisizo shirikishi za kufundishia pamoja na faida na hasara zake:- Njia ya majadiliano , njia hii imekuwa ikitumika katika ufundishaji kwa muda mrefu. Katika kujadiliana mwanafunzi mmoja mmoja hupata nafasi ya mawazo aliyonayo kuhusu suala linalojadiliwa na yeye pia huweza kupata mawazo yaw engine. Katika majadiliano mwanafunzi hupata ujuzi mpya nje na ule aliokuwa nao kabla hajashiriki kat...

DHANA YA MATUMIZI YA LUGHA, REJESTA, UTATA

Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika. Katika mada hii utajifunza mambo ya msingi ya kuzingatia unapotumia lugha. Utaelewa dhana mbalimbali zinazohusishwa na matumizi ya lugha kama vile rejesta, misimu, utatata katika lugha, lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi. Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika. Dhima ya matumizi ya lugha Dhima kuu ya lugha ni kupashana habari, ujuzi na maarifa mbalimbali. Vilevile lugha husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu. Uhusiano huo unaweza kuwa wa kijamii, kielimu, kibiashara, kihuduma, kisiasa, kiuchumi n.k. Kwa hiyo, kujua jinsi ya kuitumia lugha kama inavyotakiwa, kunasaidia kufikisha vizuri ujumbe unaotakiwa bila kuupotosha. Vilevile kunasaidia kuepuka migongano, hasa ya kijamii kwa kuwa utakuwa umetumia lugha kwa mujibu wa mi...