Skip to main content

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI

Ushairi kama moja kati ya tanzu za fasihi inayowasilishwa katika namna zote aidha kwa lugha ya maandishi au kwa lugha ya masimulizi una mchango au nafasi kubwa sana katika kunufaisha au kustawisha maisha ya binadamu kwa kumuelimisha, kumsisimua, kutunza na kuhifadhi amali zake pamoja na kukuza na kuendeleza lugha yake kama moja kati ya vipengere muhimu maishani mwake.
Ushairi kama nudhumu katika fasihi simulizi hujumuisha nyimbo, ngonjera, tenzi na mashairi yenyewe. Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au katika kumbo mbalimbli kama asemavyo Mulokozi (1996) kuwa zipo kumbo kuu tatu ambazo ni ushairi wa kijadi au kimapokeo, ushairi wa mlegezo au huru na ushairi wa maigizo.
Wanazuoni wafuatao wa mashairi ya kimapokeo wametoa maana za ushairi kama ifuatavyo:-
Shaaban Robert (1958:37).
“Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari…, mawazo, maoni na fikra za ndani zinazoelezwa kwa muhtasari wa ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu”.
Mathias Mnyampala (1965:Dibaji)
“ushairi ni msingi wa maneno ya hekima tangu kale, ndicho kitu kilicho bora sana katika maongozi ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa vina na mizani maalumu kwa shairi”.
Amri Abedi (1954:1).
“Ushairi au utenzi ni wimbo, hivyo kama shairi haliimbiki, halina maana”.
Mbali na maana hizo za ushairi kwa mujibu wa wanamapokeo, zifuatazo ni maana za ushairi kwa mujibu wa wanamlegezo:-
Kezilahabi katika mbonde, J.M (1976:123).
Ushairi ni tukio, hali au wazo ambalo limeoneshwa kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno fasaha yenye mizani kwa kifupi ili kuonesha ukweli fulani wa maisha.
Topani (1974:X).
“Anasema, shairi ni utungo unaoeleza hisia za undani za binadamu kwa mpangilio fulani wa maneno”.
Mlokozi na Kahigi (1982:25).
Wao wanatafsiri ushairi kuwa ni sanaa ilyopambanuliwa kwa mpangilio maalumu wa maneno fasaha na yenye muwala, kwa lugha ya mkato, picha, sitiari au ishara, katika usemi, maandishi au mahadhi ya wimbo, ili kuleta wazo au mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisia fulani kuhusu maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.
Kwa ujumla na kwa kawaida fasiri ya ushairi ilyozoeleka bila kujali ni wa kimapokeo au mlegezo, ni ile isemayo kuwa ushairi ni sanaa inayotumia lugha teule na mpangilio fulani wa maneno ili kuweza kufikisha ujumbe lengwa kwa jamii. Ushairi ni tofauti na nathari kwani hauelezi tu bali huonesha hisi, wazo, hali kitu au tukio fulani kwa kuathiri hisia zetu. Na kuhusu kuwepo kwa makundi ya wanamapokeo na wanamlegezo au wanamapinduzi ni kutokana na imani zao kuhusu ushairi. Wanamapokeo ni wale washairi wa jadi wanaoshikilia kuwa ili utungo fulani uweze kuwa shairi ni lazima utungo huo ufuate sheria na kanuni fulani kama vile ulali wa vina na mizani, idadi, idadi maalumu ya mishororo katika beti ambazo huitwa arudhi, na wanamlegezo/wanamapinduzi/wanausasa ni wale  wanao  amini  kuwa ili utungo Fulani uweze kuingia katika kundi la mashairi si lazima uzingatie arudhi.Kundi  hili  husisitiza  kuwa la muhimu  katika  utungo  nsiyo sheria  bali ni ujumbe au maudhui/malengo  kwa  hadhira yake.
Kutokana  na  mitazamo  inayotumiwa  na  wanamapokeo  na  wanausasa   katika  kutafsiri ushairi, inaonesha  kuwa  tafsiri  zao  zinalingana  katika  namna/vipengele vifuatavyo;
Ushairi  ni  wimbo. Wataalamu  wa  pande  zote  mbili wanaamini  kuwa  kitu kinachoitwa ushairi ni sharti  kiwe  katika  mahadhi ya wimbo ,yaani kiweze kuimbika. Mfano, Mwanamapokeo  Amri
Abeid(1954:1) anasema ushairi ni wimbo, hivyo  basi  shairi  kama haliimbiki halina maana.Wakati mwana mapinduzi  Mulokozi  nae  anasema lazima shairi liwe na mahadhi  ya wimbo(liimbike)
Ushairi ni sanaa; Wanamapokeo na wanamapinduzi katika kueleza maana ya ushairi wanaamini kuwa ushairi ni kazi ya sanaa. Hii inamaana kwamba kuna ufundi maalumu unaotumika kusuka/kutunga mashairi. Hii  inaweza  kuthibitishwa na mwanamapokeo  Shaaban  Robert  na  mwanamlegezo  Mlokozi na Kaligi  ambao  wote  wanaelezea  ushairi  kuwa  ni  sanaa.
Ushairi  unailenga na kuibua  hisia  za  jamii.Wanazuoni wa pande zote mbili wa kimapokeo na wa kisasa wanaamini  kuwa ushairi  ni lazima ulenge na kuibua hisia za jamii.Kwa mfano wanamapokeo Mathuis Mnyampala  (1965)  na  Shaban Robeert (1958) pia wanamapinduzi na Kahigi(1982) pamoja na Topan (1974) wote wanasisitiza  kuwa ushairi ni lazima uilenge jamii kwa kuibua hisia za jamii hiyo husika.
Ushairi  hutumia lugha (maneno) ambayo ni fasaha.Jambo hili katika ushahiri linatiliwa mkazo na wanazuon i wa makundi  yote .Mfano wale wa kimapokeo na hata wa kisasa.Wataalamu waoweza kuthibitishia hili ni mwanamapinduzi  Kazilahabi ambaye anasema ushahiri huwa na uzuri wa maneno fasaha  na mwanautamaduni  Shaban  Robert  asemaye kuwa ushairi huwa na ufasaha wa maneno.
Pamoja  na ulinganifu huo unaojitokeza  baina ya wataalamu wa mashairi ya kimapokeo  na wale wa mashairi ya  kimlegezo  katika  kutoa  maana  ya  ushairi, bado kuna migongano kadha wa kadha ya kimtazamo  inayo  wafanya  wahitilafiane. Tofauti  zao ni  pamoja  na  hizi zifuatazo;
Urari  wa  vina  na  mizani (arudhia). Wanamashairi  karibuni  wote wa kimapokeo  wanasisitiza  kuwa  utungo  ili uitwe  shairi  lazima taratibu maalumu za utunzi  kama  anavyoeleza  mathius  Mnyampala  (1965) ufanano(urari ) wa  vina na mizani. Lakini wana  ushairi  wa kimapinduzi wote hawaoni  umuhimu  wa  jambo  hilo, wao wanaona utungo  uwao wowote ule unaweza kuwa shairi  ilimradi ufikishe ujumbe kwa jamii. Kwa wanamapinduzi kuhusu  urari wa vina na mizani ni kazi ya ziada isiyo ya lazima katika mashairi.
Idadi ya mistari, wana ushairi wa kimapokeo wanasisitiza kuwa katika usahairi  lazima kuwa na idadi maalumu ya mishororo katika kila ubeti  na ni shariti iadadi hiyo ifanane kwa beti zote lakini wataalamu wa mashairi ya kisasa wao wanaona shairi hata ukiwa na idadi ya mistari inayotofautiana katika beti zote ni sawa tu, cha kuzingatia ni maudhui yaliyomo na sio fani.

Ni maneno ya hekima tangu kale, kama asemavyo  mwanamapokeo Mathias Mnyapala (1965:Dibaji) lakini mashairi ya kimlegezo ni mpya yameibuka baada ya mashairi ya kimapokeo. Kwa wanamashairi wa kisasa wanaamini kuwa umri sio kigezo cha kufafanulia mashairi na huweza  kutumia lugha  yeyote aipendayo mtunzi
Matumizi  ya lugha, mashairi kwa mujibu wa wanamapokeo  lazima yatumie lugha ya mkato na mnato  lakini wanamapinduzi wanaona hicho si kigezo cha msingi  katika utoajiwa maana ya ushairi ,mshairi atumie lugha kadri awezavyo yeye. Mfano Mathias Mnyapala na Shabani Robert (Wanamapokeo) wanasisitiza matumizi ya lugha ya mnato na mkato lakini wanamapinduzihawaongelei suala hili katika kutoa maana ya mashairi au ushairi.
Pamoja na ufanano au ulinganifu na utofauti unaojitokeza baina ya wanzuoni wa kisasa na wale wa kimapokeokatika kueleza  au kutoa maana ya mashairi pia ni vyema kuwa ushairi uzingatie mambo yafuatayo;
Ni vyema ushairi ubadilike kutokana na wakati na mazingira, mashairi lazima yapambanue matukio halisi yanayotokea katika jamii husika na  katika wakati huo. Mfano, katika kipindi cha mafuriko basi  washairi watunge mashairi yanohusu mafuriko kwa ajili ya jamii hiyo iliyokumbwa na janga hilo, jamii nyingine itakayokubwa na janga la njaa basi ushairi wao uwe ni wa kuhusu suala hilo  katika kipindi hicho.
Aidha pamoja na kuwepo kwa watu wenye vipawa vya ushairi kwa kuzaliwa navyo, haina budi pia kutumia wataalamu waliosomea maishairi katika kutoa fasili za ushairi na kutengeneza diwani za mashairi  badala ya kuwa kila mtu anazungumza anachofikiri yeye kuhusu ushairi na mashairi
Kwa ujumla mashairi yoyote yale, yawe ya kimapokeo au ya kisasa ni mashairi tu ili mradi jamii inufaike kutokana na mashairi hayo kwa kusisimka, kuelimika, kutunziwa amali zake na kukuziwa na kuendelezewa lugha yake.


                                                               
                                                                 MAREJEO.
Abeid, A. (1954). Sheria za kutunga Mashairi na Diwani ya AMR. EALB, Nairobi.
Mulokozi,M.M. na Kahigi.K.K(1982). Kutunga za Ushairi na Diwani Yetu. TPH, Dar es salaam.
Robert,S.(1958). Hotuba juu ya Ushairi. JeASC 28/1:37-42.
Mnyampala, M. (1965). Diwani ya Mnyamlepa, EALB, Nairobi.
Topan F (1974). “Dibaji” katika Kezilahabi ukurasa:x.
Kezilahabi, E. (1976). Ushairi wa mapokeo na wa wakati ujao. Katika Mbonde J.P. 121-137

Comments

  1. Ushairi ni utungo wa kimasikizi unaotumia lugha ya mjazo ipi kufikisha ujumbe kwa jamii.

    ReplyDelete
  2. Ushairi, Ni sanaa ya lugha ya mkato yenye ubunifu unaoelezea jambo kwa kuvutia hisia

    ReplyDelete
  3. Ushairi ni tungo inayo zingatia urari wa vina na mizani ...nalengo lake kufikisha ujumbe kwa hadhira kusudiwa

    ReplyDelete
  4. Kazi nzuri sana nimesoma nimeelewa vizuri

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

NOTES ZA USHAIRI

USHAIRI     NI    NINI ? Shaaban Robert katika uandishi wa ushairi ameandika Tenzi na mashairi ya kimapokeo. Tenzi : Ni aina ya mashairi ya kimapokeo wenye sifa zifuatazo: Kimaudhui ; Ni utungo wenye maudhui yanayosimulia kwa urefu tukio fulani maalum. Waweza kuwa wasifu wa mtu au jambo la kihistoria. Mfano; S. Robert ameandika utenzi wa vita vya Uhuru, ameeleza kuhusu historia. Pia katika Mapenzi Bora, ameeleza kuhusu sifa za mapenzi bora. Utenzi ni utungo wa pili kati tungo za ushairi zenye beti nyingi. Utungo wa kwanza unaoongoza kuwa na beti nyingi kuliko zote katika ushairi ni Tendi. Lakini hapa tutaangazia tenzi zaidi. Utenzi hauna mizani nyingi aghalabu mizani nane, hauna mshororo bali una nusu mshororo/kipande mstari. Vilevile katika utenzi kipande mstari hakigawiki. Pia katika kipande mshororo kuna vipande vinne kwa kila ubeti. Mistari mitatu ya kwanza huwa na vina vyenye urari na kipande mstari cha mwisho/cha nne huwa...

KISWAHILI FORM 1: FASIHI SIMULIZI

KISWAHILI Form 1 Topic 4 FASIHI SIMULIZI Fasihi simulizi ni moja kati ya tanzu za fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Katika mada hii utajifunza na kisha utaweza kubainisha tanzu na vipera vya fasihi simulizi pamoja na ufafanuzi wake. Na pia utaweza kutofautisha kati ya kipera na kipera au kati ya utanzu na utanzu. Ubainishaji wa Tanzu za Fasihi Simulizi Tanzu za Fasihi Simulizi Bainisha tanzu za fasihi simulizi Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. Tanzu za Fasihi Simulizi ni pamoja na hizi zifuatazo: Masimulizi/hadithi Semi Ushairi Mazungumzo Maigizo Ngomezi Ufafanuzi wa Vipera vya Tanzu za Fasihi Simulizi Vipera vya Hadithi Fafanua vipera vya hadithi SIMULIZI/ HADITHI Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulan...