AINA ZA USHAIRI (BAHARI)
Bahari; hii ni aina mahususi ya ushairi yenye sifa fulani kiumbo na pengine hata kimaudhui na kimatumizi na zinazoipambanua na aina nyingine ya ushairi.
S.A Kibao (2003) anasema, ushairi wa Kiswahili umegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni: shairi, utenzi na ngonjeara. Anaendelea kusema, aina zote hizi kanuni zake ni za pamoja isipokuwa utenzi ambao una mpangilio wa namna ya pekee.
S. Robert na Amri Abeid (1954) wanasema zipo bahari tatu tu za ushairi nazo ni:wimbo, shairi na utenzi.
A.S. Nabhany na wenzake wameainisha bahari 13 za ushairi na kusema kuwa utungo wowote lazima uingie katika bahari mojawapo. Bahari hizo ni hizi zifuatazo:
1. Ushairi; Ni utenzi wenye mishororo minne na vipande viwili kila msitari. Kila mstari una mizani 16 na kila kipande kina mizani 8. Maudhui yake yanatokana na jambo lolote lile analoliona mtunzi.
2. Wimbo; Ni utungo wenye mishororo mitatu kila ubeti na kila mshororo una vipande viwili. Nyimbo nyingi huongelea mapenzi.
3. Tenzi; Ni utungo wenye vipande vine katika kila ubeti na vina hubadilika kila ubeti isipokuwa kipande cha mwisho. Tenzi nyingi zina mizani nane kila mshororo na nyingine zina mizani 11 na zingine 10.
4. Inkshafi/Duramandhuma; Imepata jina lake kutokana na utenzi wa Aliinkshafi. Tenzi hizi zina maadili ya kidini japokuwa maudhui yake yanaweza kutumika katika maadili ya kidunia. Kila ubeti una mishororo minne na kila mshororo una mizani 11.
5. Ukawafi; Hili ni shairi lenye mishororo mitatu au zaidi katika kila ubeti na vipande vitatu katika kila mshororo. Mizani zinaweza zikatofautiana au zikawa sawa.
6. Wajiwaji/Takhimisa; Una mishororo mitano kila ubeti na mizanai 15 kila mshororo na vipande vitatu katika kila mshororo vina muundo wa mizani 6, 4, 5. Maudhui yake ni ya kidini au kiamisha kwa ujumla, mfano Takhimisa ya Liongo na tenzi ya Inkshafi.
7. Hamziya; lipata jina lake kutokana na kaswida ya Hamziya ambao ni utenzi wa kiarabu. Mishororo ya Hamziya ina vipande 3 vya mizani 5, 4, 6
8. Tiyani-Fatiha; Ni ushairi wa kidini wa kuomba toba, una mishororo 9 kila ubeti ambayo huweza kutofautiana kwa urefu/mizani.
9. Utumbuizo; Haina idadi kamili ya mishororo na mizani, urefu wa mstari au mshororo hutegemea pumzi aliyonayo mwimbaji na lengo lake; mfano ni nyimbo za Liyongo kuna tumbuizo.
10. Wawe; Ni ushairi au wimbo wa kilimo, huimbwa wakati wa kulima au kupanda.
11. Kimai; Inahusu shughuli za majini, ni bahari ya wavuvi na mabaharia. Idadi ya mishororo na vina si lazima.
12. Zivindo; Ni ushairi unaofafanua maana za maneno; na kazi yake ni kujifunza lugha na mkuhifadhi lugha.
Mfano: Kata ni kata ya nyoka
Au kata ya nyweleni
Kata ya tweka, bandikwayo kichwani
13. Sama; Neno ‘sama’ ni mahadhi au sauti, hivyo bahari hii hukusanya washairi wote wenye kufuata mahadhi ya kigeni.
Comments
Post a Comment