Lugha ni nini?
Lugha ni mfumo maalum wa sauti nasibu zenye maana ambazo hutumiwa miongoni mwa binadamu kwa ajili ya kukidhi malengo ya kimawasiliano miongoni mwa watumiaji husika.
Kutokana na fasili hiyo, kwa muhtasari lugha ni sauti nasibu, lugha ni mfumo maalum, lugha inamhusu binadamu, lugha hutumika kwa ajili ya kuwasiliana. Dhana hizi zitajipambanua zaidi katika sehemu inayofuata(Sifa za Lugha).
Sifa/tabia za Lugha
Lugha ni sauti za binadamu zenye maana
Lugha ni sauti zinazozalishwa na binadamu kwa kutumia ala za sauti kama vile ulimi, midomo ufizi, kaakaa laini, kaakaa gumu, meno, koromeo na viungo vinginevyo; sauti hizi huanzia kama irabu na konsonanti. Sauti hizi ili kuitwa lugha lazima ziwe na maana na kueleweka kwa watumiaji wake. Na hii ndio sifa muhimu kuitofautisha lugha ya binadamu na mawasiliano ya viumbe hai wengine.
Lugha ni sauti nasibu
Tunasema lugha ni nasibu kwa sababu hizi huzuka kwa nadra tu (bila kukusudiwa) na hazina uhusiano wa moja kwa moja na mkile kinachorejelewa. Kwa maana nyingine hakuna makubaliano au mikakati ya pamoja katika kuamua utokeaji wa sauti hizi.
Lugha ni mfumo maalum wa sauti
Hii ni kwa sababu sauti hizi ziitwazo lugha hutokea katika utaratibu maalum unaoanzia kiwango cha chini mpaka kiwango cha juu zaidi. Sauti hizi huanzia katika upekepeke kama irabu au konsonanti, kisha huunda neno, kirai (kikundi cha maneno), kishazi na hatimaye sentensi (tungo). Katika viwango vyote, yaani Kiwango cha Sauti (Fonolojia), Kiwango cha Maumbo (Mofolojia), Kiwango cha Miundo (Sintaksia), Kiwango cha Maana (Semantiki) na Kiwango cha Isimu Amali (Pragmatiki) kunakuwa na kanuni maalum.
i Lugha ni mali ya binadamu
Hakuna kiumbe kingine zaidi ya binadamu kinachotumia lugha. Licha ya kuwa viumbe wengine (ambao si binadamu) hawahusiani na huwasiliana, mawasiliano yao si lugha bali ni ishara, sauti na namna mbalimbali za kuwasiliania lakini hawana lugha. Kwa hivyo lugha ni mali ya kipekee ya binadamu kwa sababu ndiye kiumbe pekee mwenye uwezo wa kuzalisha lugha kwa kuwa ndiye mwenye viungo pekee vyenye uwezo huo.
Lugha hubadilika
Lugha yoyote hupokea au kupitia mabadiliko kutokana na wakati na mazingira. Mabadiliko haya hutokea katika viwango vyote vya lugha kama ifuatavyo:
a. Mabadiliko ya kifonolojia
Haya ni mabadiliko ya kanuni au mfumo wa matamshi katika lugha. Mara nyingi yanatokana na lugha kukopa misamiati ambayo ina sauti zisizopatikana katika lugha inayokopa au mabadiliko mengineyo.
b. Mabadiliko ya kimofolojia
Hay hutokea pale ambapo lugha fulani hubadilika katika utaratibu wake wa kimaumbo hususani katika kanuni za uundaji wa maneno.
c. Mabadiliko ya kileksia na kimaana
Haya ni mabadiliko katika leksimu au maana katika lugha husika, kwa mfano kuongezeka kwa leksimu hutokana na njia au mbinu zote za uundaji wa maneno. Leksimu inapoongezeka na maana huongezeka kwa kuwa huja na dhana (maana) inayowakilishwa.
d. Mabadiliko ya kisintaksia
Haya ni mabadiliko ya kimiundo ambapo lugha hubadilika katika utaratibu tofauti na ule uliokuwepo awali.
Lugha huathiri na kuathiriwa
Lugha yoyote inaweza kuathiri utaratibu wa lugha nyingine, kadhalika lugha hiyo hiyo inaweza kuathiriwa na lugha nyingine katika kiwango, viwangu fulani au viwango vyote vya lugha. Rejea katika sifa ya mabadiliko.
Lugha hupitia mfumo wa kuishi
Lugha hupitia awamu karibu zote za maisha ya viumbe hai kama vile binadamu, wanyama, mimea na vinginevyo. Hatua hizi ni kama ifuatavyo:
a. Lugha huzaliwa
Hii ni punde lugha inapoibuka.
b. Lugha inakuwa
Lugh iikishazaliwa hukua, na kukua kwake ni pale inapojitanua kwa kujiongezea msamiati na (au) matumizi.
c. Lugha ianweza kufa
Kufa kwa lugha ni aple inapokosa watumiaji au kutotumika kwa sababu mbalimbali.
Lugha yoyote ina hadi sawa na nyingine na hujitosheleza
Lugha zote duniani zina hadhi sawa kwa sababu zinajitosheleza kwa sababu hukidhi mahitaji ya wtumiaji wake katika nyanja zote za maisha ikiwemo kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
Lugha hujizalisha
Lugha yoyote hujiongezea msamiati kupitia njia maalum za uundaji wa maneno/msamiati/istilahi ikiwemo Kutohoa au Kukopa, Ufupishaji, Ufananishaji wa umbo au sauti, Urudufishaji, na njia nyinginezo.
Lugha hufungamana na utamaduni wa jamii fulani
Lugha ni sehemu ya utamaduni wa jamii ya watumiaji wake na ni nyenzo ya kuhifadhia na kurithisha utamaduni wote kwa ujumla. Kadhalika, lugha hutumika kuendana na kwa kukidhi shughuli na mambo yote katika maisha ya kila siku.
Dhima za Lugha
Lugha ni chombo cha mawasiliano
Lugha hutumika kupashana habari, kuwasilisha dhana au fikra walizo nazo binadamu, hisia kama vile furaha, huzuni, hasira, maarifa na uhalisia mwingine wa kimaisha kupitia kutoa na kupokea ujumbe.
i Lugha ni kitambulisho
Kupitia lugha tunaweza kumtambua na kumfahamu zaidi mtu au jamii. Utambulisho huo waweza kuwa katika namna mbili kama ifuatavyo:
a. Utambulisho wa mtu binafsi
Kupitia matumizi ya lugha tunaweza kubaini jinsi ya mtu (ni wa kike au ni wa kiume) hata kama hatujamuona ana kwa ana, yaani hata kama tunaona alichokiandika. Kwa mfano wanaume kwa kiasi kikubwa hutumia lugha isiyofasaha ukilinganisha na wanawake, pia wanaume hutumia ubabe katika mazungumzo hasa majadiliano ikiwemo kumkatisha mzungumzaji mwenzake bila kumwacha amalize (yaani hukiuka kwa kiasi kikubwa utaratibu wa kuachiana nafasi katika mazungumzo ukilinganisha na jinsi ya kike). Pia kupitia lugha tunaweza kung’amua falsafa, mtazamo, umri, kiwango cha elimu, hulka na tabia nyinginezo. Kwa mfano mtu mwenye tabia ya unyanyasaji tutambaini katika mazungumzo na kadhalika.
b. Utambulisho wa kikundi cha watu, jamii au taifa
Kupitia lugha tuanweza kufahamu mengi kuhusiana na watu fulani, utaratibu wao, falsafa yao, itikadi yao na kile wanachokiamini. Hivyo, kupitia lugha tunaweza kufahamu kuwa mtu ni mmoja kati ya watu wa itikadi ipi, jamii ipi au taifa gani. Kwa mfano mtu akiongea Kiswahili awapo katika mataifa mengine hubainika moja kwa moja kuwa ni wa Afrika ya Mashariki hususani nchini Tanzania au Kenya. Vile vile tunaweza kufahamu kuwa mtu ni wa dini au dhebu gani, chama gani cha siasa, kabila au taifa gani. Yote ni kwa sababu kundi tunalomuweka linafanana kwa namna fulani ya lugha.
i Lugha ni chombo cha kuunganisha watu
Lugha hupatanisha watu na kuwaweka pamoja mtu na mtu, mtu na watu, watu na watu au jamii na jamii. Kwa mfano kupitia salamu au kauli mbiu ya aina moja watu wanajikia kuwa ni wamoja, wako pamoja na wenye nia sawa ya kimaisha. Rejea nchini Tanzania, lugha ya Kiswahili ndio nyenzo pekee iliyotumika kuwaunganisha watanzania kudai uhuru, pamoja na kuungana kuijenga nchi yao.
i Lugha ni chombo cha kurithishia utamaduni wa jamii
Lugha hutumika kuendeleza na kudumisha mila, desturi, na amali za jamii kutoka kizazi hadi kizazi kupitia misemo na nyenzo nyinginezo zitumiazo lugha. Lugha ndio itunzayo kumbukumbu ya matambiko, miiko pamoja na mila na desturi nyi nginezo.
Lugha ni nyenzo ya kulinda, kuimarisha na kurejesha amani
Lugha ni nyenzo ya kulinda, kuimarisha na kurejesha amani
Lugha hudumisha utulivu, kuheshimiana, kuvumiliana na kuthamiana bila hofu yoyote. Kwa mfano kupitia kampeni za kuimiza kulinda amani kama vile “Tuilinde Amani ya Nchi Yetu”, “Tanzania ni Kisiwa cha Amani” na nyingine kama hizo, kauli mbiu kama hizi hutumika kuimarisha amani katika nchi zetu. Kadhalika, pale inapotokea tishio la kutoweka kwa amani, ni lugha ndiyo inayotumika kurejesha ikiwemo kutumika kupatanisha makundi asimu, na mamlaka ya ulinzi wa amani kutoa matumaini kwa watu wake juu ya kurejea tena kwa amani.
Lugha ni chombo cha kutolea elimu na mafunzo
Binadamu hutumia lugha kupata elimu na kuuelewa ulimwengu ili kuuishi ipasavyo kupitia kufundisha na kujifunza.
Athari ya Matumizi Mabaya ya Lugha
Lugha ikitumika vibaya huwa kinyume na dhima mbalimbali tunazozifahamu na hupelekea yafuatayo (baadhi tu)
i. Lugha ianweka kutumika kukandamiza uhuru wa mtu au taifa
ii. Lugha inaweza kuwatenganisha watu, jumuiya, jamii au taifa (au inaweza kutumiwa kwa lengo hilo).
iii. Lugha inaweza kuwa chanzo cha kuvuruga amani kama chanzo cha migogoro
iv. Lugha inaweza kuleta utabaka na ubinafsi katika jamii
v. Lugha inaweza kukwamisha maendeleo ya jamii (pale inapotumika vibaya)
vi. Lugha inaweza kutumika kunyanyapaa, kudunisha na kuwabagua watu wengine.
BIBLIOGRAFIA
Masebo, J. A. na Nyangwine, N. (2010). Kiswahili: Kidato cha 3&4. Dar es Salaam: Nyambari Nyangwine Publishers.
Matinde, R. S. (2012). Dafina ya Lugha: Isimu na Nadharia, Kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educationa Publishers (T) Limited.
Msokile, M. (1992). Kunga za Fasihi na Lugha. Dar es Salaam: Educational Publishers and Distributors Limited.
Ng’waje M.H.K. (2016). Lulu za Isimu Jamii: Mtazamo wa Kisinkronia, Sekondari na Vyuo. Mwanza: Bagoka Publishing Company Limited.
Nkwera, F.M.V. (1979. Sarufi na Fasihi: Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: Tanzania Publishing House.
Comments
Post a Comment