Skip to main content

KISWAHILI FORM 4: UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI

KISWAHILI Form 4 Topic 3

UHAKIKI WA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Dhana ya Uhakiki
Fafanua vipengele vya uhakiki
Uhakiki ni kitendo cha kutathmini, kueleza, kuainisha na kutoa maoni juu ya kazi fulani ya fasihi kwa kuongozwa na kaida maalum. Kwa kiwango cha elimu ya sekondari mhakiki anafanya kazi ya uhakiki ili kuonesha mambo yanayojitokeza kama vile, dhamira, migogoro, ujumbe, falsafa, mtazamo, msimamo n.k
Dhima ya Mhakiki na Nafasi ya Mhakiki
Uhakiki ni kazi ambayo ina mchango mkubwa sana katika kazi za fasihi. Kwa msingi huo uhakiki una dhima zifuatazo:
  • Husaidia wasomaji kuilewa kazi ya fasihi kwa urahisi;Watunzi wa kazi za fasihi hutofautiana katika matumizi ya lugha na taswira, hivyo mhakiki anapofanya kazi ya uhakiki anamsaidia msomaji kuelewa vipengele hivi kwa kuvifafanua kwa lugha rahisi.
  • Husaidia ukuaji wa kazi za fasihi;Mhakiki anapoonesha ubora na udhaifu wa kazi ya mtunzi fulani, watunzi wengine pia watafunguka kifikra na kutunga kazi iliyobora zaidi.
  • Uhakiki hukuza uelewa wa mhakiki; Kwa kuhakiki kazi mbalimbali za fasihi, mhakiki hujiongezea maarifa ya lugha pamoja na mambo yanayotokea katika jamii.
Nafasi ya Mhakiki
Mhahiki ana nafasi kubwa katika kazi za fasihi, Mhakaki ndiye anafafanua kazi ya fasihi ili hadhira iweze kumwelewa vizuri mtunzi wa kazi hiyo. Kwa hiyo hapa mhakiki anasaidia kurahisisha mawasiliano kati ya hadhira na mtunzi.
Vilevile mtunzi huwaonyesha watunzi ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hivyo huwawezesha watunzi kufanya kazi bora zaidi.
Hatua za Kufuata wakati wa Kufanya Uhakiki
Vilevile mtunzi huwaonyesha watunzi ubora na udhaifu wa kazi zao. Kwa kufanya hivyo huwawezesha watunzi kufanya kazi bora zaidi.
Kwanza ni kuisoma kazi ya fasihi; hapa mhakiki anatakiwa kuisoma kazi husika ya fasihi kwa kina na kuielewa vizuri.
Pili ni kuainisha na kuchambua mambo muhimu yanayojitokeza katika kazi hiyo katika vipengele vya fani na maudhui.
Tatu ni kutoa tathimini au kuelezea ubora na udhaifu wa kazi inayohusika.
UHAKIKI WA MASHAIRI
Shairi ni utungo wa kisanaa wenye mpangilio maalum wa lugha ya mkato unaowasilisha mawazo au ujumbe kuhusu mwanadamu au mazingira yake na hufuata utaratibu fulani.
Mashairi yapo ya aina mbili:
  1. Mashairi huru
  2. Mashairi ya arudhi
Mashairi ya arudhi
Haya ni mashairi yanayofuata kanuni za kimapokeo au arudhi za utunzi wa mashairi. Arudhi/kanuni hizi ni pamoja na:
  1. Kugawika kwa shairi katika beti
  2. Beti kuwa na idadi maalum ya mishororo.
  3. Mishororo ya ubeti kugawika katika vipande
  4. Mishororo kuwa na ulinganifu wa mizani
  5. Shairi kuwa na urari wa vina
  6. Shairi kuweza kuimbika / kuwa na mahadhi au mapigo.
  7. Kuwepo kwa kipokeo katika shairi
  8. Kuwa na mtiririko wa mantiki na mawazo au muwala
  9. hairi kuwa na utoshelezo wa beti / kujisimamia kimaana.
Mashairi huru
Pia hujulikana kama mashairi ya kimapinduzi. Haya ni mashairi yasiozingatia lazima ya arudhi na hivyo huwa na muundo huru. Sifa zake kuu huweza kuwa:
  1. Lugha ya muhtasari
  2. Lugha yenye mahadhi
  3. Lugha ya kisanii iliyo na mafumbo na taswira
  4. Mara nyingine hugawika katika beti.
  5. Mishororo kamilifu (inayojitosheleza) na ile isiyo kamilifu (mishata)
Sifa za Mashairi
Mashairi huwa na sifa maalum zinazoyatambulisha kama kazi ya kishairi, yawe ya kimapokeo au kimapinduzi.
Sifa hizi ni kama vile:
  1. Mashairi hutumia lugha ya mkato / muhtasari
  2. Ni sanaa au kazi iliyobuniwa kwa ufundi
  3. Huwa na mpangilio maalum kuanzia mistari hadi beti.
  4. Hutumia lugha teule na msamiati teule uliosheheni tamathali, taswira na jazanda.
  5. Mashairi huwa na sifa ya kuweza kuimbika hivyo shairi ni wimbo na wimbo ni shairi.
Dhima ya mashairi
  1. Kupasha ujumbe kwa hadhira kwa njia ya upole na mvuto
  2. Kuelimisha na kuzindua jamii.
  3. Kuendeleza na kukuza kipawa cha utunzi.
  4. Kuhifadhi msamiati wa lugha ya Kiswahili na Sanaa ya fasihi.
  5. Kuburudisha hadhira na wasomaji.
  6. Kuwasilisha hisia za ndani za mtu na mawazo
Hatua za uhakiki wa mashairi
  1. Soma shairi polepole na kwa makini kupata maana ya jumla.
  2. Soma shairi tena kwa utaratibu ukizingatia maneno na vipande mbalimbali na kuchunguza maana ya kila mojawapo
  3. Pitia maswali yote kwa makini ukitilia maanani aina ya majibu yanayotarajiwa.
  4. Soma shairi tena ukipigia mstari kwa penseli sehemu zinazoelekea kujibu maswali.
  5. Toa majibu kamilifu kulingana na swali kwa lugha ya mtiririko.
Vipengee vya Uchambuzi Wa Mashairi
  1. Anwani/kichwa cha shairi – Huwa ni muhtasari wa shairi katika neno au sentensi moja. Anwani ni kidokezo muhimu cha kinachozungumziwa katika shairi. Anwani huweza kuwa ya moja kwa moja, fumbo, kinaya, kibwagizo au sehemu ya kibwagizo. Ikiwa shairi halina anwani, basi lipewe anwani inayoafikiana na maudhui au dhamira kwasentensi isiyozidi maneno 6.
  2. Maudhui – Haya ni masuala makuu au mambo muhimu yanayohusu mwanadamu au mazingira yake yanayozungumziwa katika shairi. Kwa mfano: malezi, siasa, usalama, unyanyasaji, ufisadi n.k. Maudhui hung’amuliwa kwa wepesi kutokana na kisa kilichomo katika shairi.
  3. Dhamira / shabaha - Ni lengo kuu la mshairi katika kusanifu utungo wake. Dhamira ya mtunzi huwa ni ujumbe kwa kifupi anaoutambua msomaji kutokana na mwelekeo wa usemaji wa mtunzi katika shairi. Mfano: Baada ya kusoma shairi, unaweza kung’amua mtunzi alitaka kusisitiza kauli kuwa uongozi mbaya haufai, misitu ni uhai n.k. Dhamira hutokana na mwelekeo wa mawazo ya mshairi au falsafa yake.
  4. Mbinu na tamathali za lugha - Ni mbinu za uandishi na tamathali za usemi zilizotumiwa na mshairi katika shairi. Mfano:Mazda / ziada / zidi - kurefusha maneno;enda kuwa enenda. Inksari / muhtasari - Ni kufupisha maneno;aliyefika kuwa alofika. Utohozi – Mbinu ya kugeuza msamiati / maneno ya lugha geni ili yaandikike na kutamkika kana kwamba ni ya Kiswahili. Mfano: Time - taimu; One – Wani. Mbinu hii vilevile huitwa ukopaji au uswahilishaji.
Taarifa Muhimu za Mwandishi wa kila Kitabu
Baini taarifa muhimu za mwandishi wa kila kitabu
Mwandishi wa fasihi ni mtu anaeweza kubuni kazi ya fasihi na kuiweka katika maandishi. Unaposoma kazi za fasihi ni lazima ujue taarifa muhimu za mwandishi wa kazi hiyo, ambazo ni jina, kwa sababu kila utakapokua unajibu swali ni lazima utaje jina la mwandishi wa kitabu. Falsafa na utamaduni kujua msimamo wake, na muundo kujua mpangilio wa matukio, mtindo kujua upekee wake na matumizi ya lugha.

Comments

Popular posts from this blog

KISWAHILI FORM 1: FASIHI SIMULIZI

KISWAHILI Form 1 Topic 4 FASIHI SIMULIZI Fasihi simulizi ni moja kati ya tanzu za fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Katika mada hii utajifunza na kisha utaweza kubainisha tanzu na vipera vya fasihi simulizi pamoja na ufafanuzi wake. Na pia utaweza kutofautisha kati ya kipera na kipera au kati ya utanzu na utanzu. Ubainishaji wa Tanzu za Fasihi Simulizi Tanzu za Fasihi Simulizi Bainisha tanzu za fasihi simulizi Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. Tanzu za Fasihi Simulizi ni pamoja na hizi zifuatazo: Masimulizi/hadithi Semi Ushairi Mazungumzo Maigizo Ngomezi Ufafanuzi wa Vipera vya Tanzu za Fasihi Simulizi Vipera vya Hadithi Fafanua vipera vya hadithi SIMULIZI/ HADITHI Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulan...

MBINU ZA KUFUNDISHIA

Mbinu za kufundishia , ni miongozo mbalimbali atumiayo mwalimu wakati wa kufundisha somo aliloliandaa kwa wanafunzi wake. Walimu wanapaswa kuamua kwa kuchagua kwa makini njia na mbinu bora za kufundishia ili wanafunzi wake waweze kujifunza kwa ufanisi. Ziko njia nyingi za kutengeneza mazingira ya mtoto aweze kujifunza na pia ziko mbinu nyingi za kufundishia. Pamoja na wingi huo tunaweza kuzigawa katika makundi makuu mawili kadri ya jinsi zinavyowashirikisha watoto katika tendo la kujifunza, ambazo tunaweza kuziita shirikishi na zisizo shirikishi . Zifuatazo ni baadhi ya mbinu shirikishi na zisizo shirikishi za kufundishia pamoja na faida na hasara zake:- Njia ya majadiliano , njia hii imekuwa ikitumika katika ufundishaji kwa muda mrefu. Katika kujadiliana mwanafunzi mmoja mmoja hupata nafasi ya mawazo aliyonayo kuhusu suala linalojadiliwa na yeye pia huweza kupata mawazo yaw engine. Katika majadiliano mwanafunzi hupata ujuzi mpya nje na ule aliokuwa nao kabla hajashiriki kat...

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI

Ushairi kama moja kati ya tanzu za fasihi inayowasilishwa katika namna zote aidha kwa lugha ya maandishi au kwa lugha ya masimulizi una mchango au nafasi kubwa sana katika kunufaisha au kustawisha maisha ya binadamu kwa kumuelimisha, kumsisimua, kutunza na kuhifadhi amali zake pamoja na kukuza na kuendeleza lugha yake kama moja kati ya vipengere muhimu maishani mwake. Ushairi kama nudhumu katika fasihi simulizi hujumuisha nyimbo, ngonjera, tenzi na mashairi yenyewe. Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au katika kumbo mbalimbli kama asemavyo Mulokozi (1996) kuwa zipo kumbo kuu tatu ambazo ni ushairi wa kijadi au kimapokeo, ushairi wa mlegezo au huru na ushairi wa maigizo. Wanazuoni wafuatao wa mashairi ya kimapokeo wametoa maana za ushairi kama ifuatavyo:- Shaaban Robert (1958:37). “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari…, mawazo, maoni na fikra za ndani zi...