3. K.K. Kahigi na M.M. Mulokozi: Malenga wa Bara
SURA YA TATU
Kitangulizi
Majina ya K.K. Kahigi na M.M. Mulokozi si mageni katika uwanja wa iasihi ya Kiswahili. Kati ya kazi zao mbalimbali zilizokwishachapishwa za Mashairi ya Kisasa. (TPH, 1973) Malenga wa Bara (EALB, 1976) na Kunga za Ushairi na Diwani Yetu (TPH. 1982) ndizo ambazo zimewapa nafasi muhimu katika dunia ya ushairi wa Kiswahili. Pamoja na hizo, MuIokozi pia amechapisha tamthilia ya kihistoria inayotumia mawanda ya kiepiki kueleleza maisha ya shujaa Mkwawa,Mukwawa wa Uhehe (EAPH, 1979) naye Kahigi akishirikiana na R.A. Ngemera wamechapisha tamthilia ya Mwanzo wa Tufani (TPH, 1977) yenye kuchambua masuala mabalimbali ya kitabaka katika jamii. Katika kazi zote hizi waandishi hawa wanashughulikia dhamira kadhaa zinazohusu nyanja za utamaduni, saisa na uchumi katika maisha ya Watanzania na Waafrika kwa jumla.
DHAMIRA KUU
Katika diwani yao ya Malenga wa Bara, washairi wamekabili dhamira mbalimbali, hasa za:
1. Maana ya uhuru
2. Dini na kifo, pamoja na maana ya maisha
3. Kumtetea mkulima na mtu mnyonge
4. Matumizi ya nguvu kama njia ya ukombozi wa wanyonge
5. Mjadala kuhusu masuala ya utamaduni
6. Uzalendo na Wasifu
7. Mapenzi
8. Namna tunavyoishi.
Maana ya Uhuru
Mashairi kadhaa yanachunguza maana ya uhuru. Katika shairi la kwanza la "Vuteni Makasia," kwa mfano, washairi wanatumia taswira ya safari kuonyesha kuwa harakati za kutafuta uhuru ni sawa na safari ndefu baharini yenye matatizo mengi (kupigwa risasi, mbundu za adui, vifo, n. k.).
Tunawaona wavuta makasia (wapigania uhuru) wakifurahia ushindi baada ya kunusurika na vishindo vya adui:
10. Wakapiga yowe wakifurahika
"Hakika kweli sasa tumeokoka",
11. Na kila mmoja akafikiria
Vipi mke wake atampokea.
Katika shamrashamra hizi za ushangiliaji, wavuta makasia hawa wanasahau kuwa mwisho wa safari bado. Hii ni tahadhari inayotolewa kuhusu maana ya uhuru; kuwa uhuru si lelemama, ni mapambano ya kuulinda na kuutetea uhuru huo pamoja na kuupalilia. Ushindi tuuonao mwanzoni mwa shairi ni ishara tu ya uhuru wa bendera na wa wimbo wa taifa. Uhuru huu si kamili kama ule wa kiuchumi na kiutamaduni haujapatikana. Kuangamia kwa wavuta makasia mwishoni mwa shairi ni ishara ya kuangamia kwa taifa ambalo baada ya kupata uhuru wa mwanzo lilijisahau likaendelea tu kuusherehekea uhuru huo, bila kuujengea misingi imara ya uchumi, utamaduni na itikadi sahihi.
Shairi la "Kitu cha Kutamani" (uk. 4), pia linaongelea faida za uhuru kwa kutueleza juu ya "uhondo" na "tulizo". Hata hivyo washairi wanasisitiza kuwa mtu apatapo uhuru hana budi kuulinda:
Ni kitu cha kutamani
Cha lazima kwa insani
.....................................
Uhuru ukiupata
Ulinde kwayako mata
Ubeti wa mwisho wa shairi hili nao hali kadhalika unasisitiza jambo hili kwa kueleza kuwa uhuru sio mwisho wa harakati. Hili limekaziwa pia katika shairi la "Uhuru" (uk. 14) ambalo limesisitiza kuwa uhuru si kula makombo hata kama makombo hayo yawe yamenona kiasi gani. Kwa vile shairi hili ni muhimu na fupi tutalidondoa lote:
1. Ni heri kula karanga, na matunda yenye koko,
Na mapumbaya kusaga, yenye wingi wa mnuko,
Kuiiko kuta kumwaga, uhondo mchanganylko,
Na holi uhuru wako, umekwisha kuuaga.
2. Ni heri kutangatanga, kama moshl wa tambiko,
Bila nyumba yo kujenga, bila sikani la kwako,
Kuliko kuwa na uga, na majumba na majiko,
Na hali uhuru wako, umekwisha kuuaga.
3. Ni heri kuyuga yuga, kwa wele na sekeneko
Kuoza kama uyoga, kufunikwa maumboko
Kuliko kuzidi ninga, uzuri wa mwili wako
Na hali uhwu wako, umekwisha kuuaga.
Katika beti hizi tatu washairi wanaeleza juu ya umuhimu wa mtu kujitegemea badala ya kutegemea mikopo na "sadaka" zenye kuhatarisha uhuru wake. Kwa hiyo basi, ni vizuri nchi zijaribu kujitegemea hata kama ni masikini kuliko kuishi maisha ya kuwa na wafadhili wa nje ambao katika kujidai "kusaidia" hapo hapo huwa wanazibana nchi hizo ziuze uhuru wao.
Taswira ya safari imerudiwa katika shairi la "Kwenye Safari Barabarani" (uk. 37) kusisitiza maana ya uhuru ilivyoshikamana na harakati. Hapa kauli ya "Uhuru ni Kazi" inajidhihirisha, na ubeti wa mwisho unauona uhuru kama "gogo zito" ambalo linahitaji tahadhari wakati wa kulisukuma. Umuhimu wa tahadhari hii umejitokeza tena katika shairi la "Mchumba Wangu" (uk. 91). Uhuru hapa ume-fananishwa na mchumba ambaye bila kuchukuliwa kwa uangalifu huweza kumgeuka huyo mwenye mchumba pa kumwangamiza. Beti za 9 na 11 zinaoayesha jambo hili:
9. Hizo pesaze akanza kunihini,
Na kunipokonya zangu kwa uhuni,
Kitwaa kizituma kwao nyumbani,
Sikuweza kuamini!
11. Na nilipotaka kumpa talaka,
Aliita majitu yakanitandika,
Nikapigwa kweli hata nikanyoka,
Sasa siwezi kuwika.
Beti hizi zinaonyesha nguvu za ukoloni mambo-leo, hasa pale ambapo nchi iliyopata uhuru wa bendera imenaswa na mtego wa ulaghai wa mataifa ya kibepari. Kupoteza uwezo wa "kuwika" ni ishara ya kupokonywa uhuru wa kujiamulia mambo. Katika ubeti wa mwisho mshairi anashauriwa kuwa ili kurekebisha yote hayo nguvu hazina budi kutumiwa:
14. Ndipo hasubiri siku ya lipizi,
Nitetane na yeye huyu jambazi,
Nimtie risasi ya kimapinduzi,
Nikomeshe huu wizi.
Suala hili la matumizi ya nguvu na umwagaji damu tutalipa nafasi yake ya pekee kwani limezishughulisha sana kalamu za washairi hawa.
Dini, Kifo na Maana ya Maisha
Washairi hawa hawaamini kuwa dini au hata Mungu ana nafasi yoyote muhimu katika maendeleo ya jamii. Kwa hiyo, mashairi yao yote yanayoongelea dini, kifo na Mungu yanakejeli na kutufanya tukidharau kifo, na tusimtegemee Mungu bali tujitegemee wenyewe katika kuleta maendeleo yetu.
Mashairi ya "Tazama Huyo Kipusa" (uk. 6), "Nikifa" (uk. 7), "Saa ya Mwisho" (uk.10), "Hatima ya Kila Mwali" (uk.22), "Baada ya Matanga" (uk.42), na "Dawa Mbili" (uk.54) ni mifano ya yale yashughulikiayo kifo kwa kuonyesha kuwa kufa ni jambo la kawaida, na kwamba hakuna haja ya kusikitishwa sana nacho.Katika mashairi hayo washairi wameonyesha pia kwamba maisha ni jambo ambalo kama lilivyo na mwanzo, lazima liwe na mwisho pia. Msichana mzuri tumwonae katika "Tazama Huyo Kipusa" na "Hatima ya Kila Mwali" twamona mwishowe akiwa kazeeka na sura yake nzuri ikiwa imechujuka. Taswira hii imetumiwa katika kuonyesha hatima ya maisha ya mwanadamu.
Kwa washairi hawa kifo ni mwisho wa maisha, na hakuna tena maisha ya ahera walajehanamu kwani, kama wasemavyo: "Kumbukizi la mkasa, ni rutuba kuipata."
Washairi hawa wanapopinga udhanifu uliopo katika dini na imani zilizoegemea kwenye nguvu zilizo nje ya uwezo wa mtu na mazingira yake, hapo hapo wanamtahadharisha mtu mnyonge, hasa mkulima, kuwa asiamini kwamba unyonge wake pamoja na shida anazokabiliana nazo hutokana na mambo yaliyoko nje ya uwezo wake. Jambo hili linachangia katika dhamira ya utetezi wa mtu mnyonge, hususan mkulima; dhamira inayofuatia karika mjadala wetu.
Kumtetea Mkulima na Mtu Mnyonge
Mashairi ya "Maombolezo ya Mtu Maskini" (uk.15), "Siku Itafika" (uk.21), "Kauli ya Madhulumu" (uk.33), "Ngonjera" (uk.43), "Vilio vya Dhiki" (uk.53), "Ni Rahisi Kula Kuliko Kulima" (uk.62) "Mwangalie Mkulima" (uk.67), "Kilio Kisikikapo" (uk.69), "Sima na Mayai" (uk.70). "Siku Yetu" (uk.90), "Mimba na Zao Lake Usizaliwe" (uk.94), "Nilipozaliwa" (uk.95), na "Nyimbo za Kijiji" ni baadhi ya mifano ya mashairi yanayojihusisha na dhamira ya kumtetea mkulima na mtu mnyonge. Kwa vile haya ni mengi sana katika diwani hii tutachukua machache kuwa vielelezo.
Shairi la "Maombolezo ya Mtu Maskini" limetumia tamathali nzito nzito kuonyesha undani wa dhiki za masikini. Linaongelea "panya wa uhitaji", "simba wa ubepari", "radi ya maradhi", "mishale ya upofu", "shubiri ya ufakiri", "miiba ya dhuluma" na "funza wa shutuma". Yote haya yamemwandama mtu masikini. Mtu kama huyu, azaliwapo huwa tayari amekwishaanza kufa. Anaona kuwa haishi bali yupo tu "kama kitu tu, kama kijiwe tu, kama kijitu tu." Lakmi hata hivyo washairi hawamkatishi tamaa mtu huyu kwani, kama wasemavyo:
Siku ya wokovu ipo,
Siku ya kukombolewa inakuja!
......................................Mtu atakuwa mtu
......................................
Na mwanadamu atakuwa huru
Siku hiyo itakapofika mtu mnyonge ataacha "kuwapo na kuanza kuishi." Lakini, ili ukombozi huu upatikane, harakati lazima ziwepo kwani siku hiyo ni ya "kitimbanga kuanguka na chamchela kucharuka." Suala hili la mbinu za wokovu wa mtu huyo mnyonge tutalipatia nafasi ya pekee katika mjadala wetu kwani nalo pia limewashughulisha sana Kahigi na Mulokozi.
Katika "Ngonjera", Mulokozi ameshughulikia mgogoro wa maisha ya mtu mnyonge na kuyatolea suluhisho. Misingi ya suluhisho hili ni zao la athari za Azimio la Arusha, ndiyo sababu linaishia na wito wa kurudi kijijini:
KIJANA:
|
Sasa sitasitasila
| |
Nitakwenda kwa haraka, furaha kuitafuta,
| ||
Kisimanimwa baraka, shamba kulikotakata!
|
Ijapokuwa kwa nyakati hizi suluhisho hili la kuwarudisha vijijini watu walioshindwa na maisha mjini ni jawabu linaloonekana kupwaya, katika miaka ya mwisho ya sitini na ya mwanzo ya sabini lilikuwa na misingi kwani nguvu za Azimio la Arusha bado zilikuwa na vuguvugu kubwa, na imani za watu katika vijiji, hasa vijiji vya ujamaa, bado zilikuwa juu sana.
Shairi la "Mwangalie Mkulima" linatoa taswira ya hali duni mno ya mkulima ambaye, twaelezwa, katika jitihada zake za kupasua "udongo na miamba", mwishowe unaambulia kibaba tu. Taswira hii imewekwa sambamba na za watu wengine kama vile "kiongozi na tumbole", "Singh na jiduka lake" oa "mtoto rijale" mwenye benzi ambalo hakulitaabikia. Kwa hiyo upande mmoja wako hao wenye vyao, na upande mwingine yuko mkulima na kuli wenye kutiririsha jasho kuwashibisha hao wa kundi la kwanza. Ubeti wa mwisho wa shairi hili unaungana na mashairi yahusuyo uhuru ambayo tumeyaangalia:
7. Naam watawme wote na kisha,
Tafiti tena ramaniya maisha:
Shangwe za uhuru sasa zimekwisha,
Kilichosalia kejeli komesha!
Kejeli wanayotaja washairi hapa ni kuwa badala ya uhuru kuleta usawa baina ya watu katika jamii, utabaka umeendelea na masikini wamezidi kufukarika wakati matajiri nao wameendelea kutajirika. Jambo hili limesisitizwa pia katika shairi la "Sima na Mayai" ambalo linaonyesha jinsi ambavyo hali ya mkulima mwenye kutoa mchango mkubwa katika elimu ya vijana imebaki kuwa duni wakati ambapo hali za wasomi hao zimebadilika na kuwa nzuri. Maisha ya raha na starehe tuyaonayo katika beti za 1, 3, 5, 7, 9 na 11 yanaashiria ukuta uliopo baina ya waliobahatika kupata elimu ambayo imekuwa daraja la kuwavusha hadi ng'ambo ya pili yenye uhondo wa kiuchumi; na yale ya beti za 2, 4, 6, 8, 10, 12, 13, 14, 15 na 16 ambayo ni ya umasikini hohehahe. Hapa basi, dhamira ya elimu na nafasi yake katika jamii inajidhihirisha: elimu hiyo bado haijawa chombo cha wokovu wa wanyonge.
Beti za 15, 16 na 17 zenye kuonyesha uzee na ubovu wa mwili wa mkulima hapo hapo zinaasa kuwa kuna haja kama si kumlipa mkulima kwa kujitolea kwake muhanga katika kuwaelimisha vijana, walau asiachwe
Kufia kando ya njia
Kama mwanamke mgumba
Kama kokwa lisilo na mbegu
Mkulima anayechangia sana katika kulielimisha taifa ni sawa na "mgomba wenye mkungu bora", mgomba ambao hauna budi kuwekewa mhimili ili ujiegemeze juu yake. Huu ni wito wa kuwalipa wakulima kwa elimu waliyopatia jamii.
Hali duni ya maisha ya mkulima imesawiriwa pia katika "Nyimbo za Kijiji "ambazo zinaonyesha jinsi mvua zilivyochelewa na vile ambavyo "mtama umemalizwa na ndege." Hata hivyo, shairi la "Weka Jembe Mpini" linaleta matumaini mema katikati ya dhiki za mkulima ijapokuwa hatuonyeshwi hasa namna mabadiliko yaonekanayo yanavyopatikana.
Matumizi ya Nguvu kama Njia ya Wokovu wa Wanyonge
Suala la utatuzi wa migogoro inayoshughulikiwa na wasanii katika kazi za fasihi lina nafasi muhimu sana wakati wa kuchambua kazi hizo. Wakati ambapo akina Kahigi na Mulokozi wamejihusisha sana na migogoro ya kijamii, na hata kushauri kuwa baadhi yake huweza kutatuliwa kwa kuthamini na kuendeleza kilimo, washairi hawa wanaelekea kusisitiza kuwa NGUVU na kumwaga damu ni lazima ili kuleta wokovu wa mtu mnyonge. Kwa hiyo basi, tunakutana na mashairi kadhaa yanayosisitiza jambo hili katika Malenga wa Bara. Mathalani, katika shairi la "Siku Itafika" (uk.21), washairi wanatuambia:
4. Siku hiyo itafika, itafika, itafika,
Vilio vitasikika, beberu asononeka,
Damu zitatiririka, dhalimu kuhasirika...
Ili "siku hiyo" ya wokovu wa wanyonge ifike, washairi wanatoa wito katika shairi lao la "Njiaya Damu" (uk.32):
Wito unaita: "Shikeni mikuki
Mapanga na miundu na bunduki
Mwende kwenye kituo cha uhaki"
Kwa hiyo basi, kwa Kahigi na Mulokozi haki itapatikana kwa kupitia mtutu wa bunduki, ndiyo maana wanasisitiza katika shairi hilo hilo:
Ninaona bahari kubwa ya damu
Bali najua kutoka kwenye damu
Patazuka maisha mastakimu
Itashere'ka ya uhuru mizimu.
Mkabala huu wa kuuona umwagaji damu kuwa ndilo jawabu la kuleta haki na usawa baina ya watu unajitokeza katika mashairi ya "Mtokoto" (uk.35), "ViliovyaDhiki" (uk.53), "Inuka" (uk.55), "Siku za Bunduki" (uk.56), "Ni Rahisi Kula Kuliko Kulima" (uk.63), "Fundo Kusukasuka" (uk.65). "Siku Yetu" (uk.91), "Mchumba Wangu" (uk.93), "Nilipozaliwa" (uk.96), "Namna Tunavyoishi" (kurasa za 105 · 108) na "Zama Hizi" (hasa ukurasa wa 115). Mashairi mengine ni "Namna Tunavyoishi" na "Zama Hizi" ambayo tutayachambua kipekee baadaye.
Kwa baadhi kubwa ya wasomaji, inawezekana kuwa ushairi wa umuhimu wa utumiaji nguvu na umwagaji damu katika kuleta wokovu wa wanyonge utaonekana kuwa wa kijaziba mno (amachist); na kubakia kuwa ni umwagaji damu kwa ajili tu ya umwagaji damu. Hata hivyo kuna mistari miwili ya mashairi mawili tofauti ambayo inaonyesha dhahiri kuwa siyo nia ya washairi kuuchukulia umwagaji damu kijuujuu tu. Mstari wa kwanza wa "Nipe Mwongozo" (uk.93) unasema: "Nipe mwongozo haraka, na kikoba cha baruti."
Kwa hiyo siyo suala la baruti na bunduki tu bali lazima harakati hizo ziwe na mwongozo kamili. Jambo hili limerudiwa katika mstari wa mwisho wa shairi la "Maombolezo ya Mtu Maskini" ambamo twaelezwa kuwa siku itakapowadia ya "kitimbanga kuanguka" ili mtu mnyonge aache kuwapo na aanze kuishi, hapo ndipo:
Kila mtu ataishi
Na bunduki begani, jembe mkononi
Na kitabu mfukoni.
Kwa kututolea vitu hivyo vitatu: bunduki, jembe na kitabu, washairi wanadhihirisha kuwa matumizi ya nguvu kama njia ya ukombozi wa mtu mnyonge hayana budi kuambatana na ufanyaji kazi pamoja na kuwa na mwongozo kamili.
Hata hivyo, maswali kadhaa yanazuka kuhusu dhamira hii. Je, matunuzi hayo ni dhidi ya nani hasa katika jamii kama ya Tanzania? Nani watashika hizo bunduki? Chini ya uongozi wa nani? Watazitoa wapi?
Mjadala Kuhusu Masuala ya Utamaduni
Kuanzia miaka ya sitini na tano hadi katikati ya miaka ya sabini kulikuwa na vuguvugu la kiutamaduni katika nchi za Afrika. Hii ilikuwa miaka ya Waafrika kujizatiti na hata kuusisitiza Uafrika wao baada ya mkoloni kuondoka. Mawazo ya kusisitiza Uafrika (Negritude) yalipata msisitizo mpya, na hata kwa upande wa siasa itikadi mbalimbali zilianza kutafutiwa misingi ya Uafrika: kukazuka "usoshalisti wa Kiafrika", "Ujamaa; nakadhalika.
Kwa upande wa masuala ya utamaduni katika Afrika ya Mashariki, mjadala ulioanzishwa na Okot pBitek katika utungo mrefu wa Wimbo waLawino (EAPH, 1975) ulisambaa haraka mno mithili ya moto katika mbuga kavu. Cheche za moto huu za kuutetea utamaduni wa Mwafrika zimejitokeza hapa na pale katika diwani hii ya Malenga wa Bara.
Shairi la "Kwa Shaaban Robert" (uk.5) ambalo ni la kitawasifu, papo hapo linatukuza lugha ya Kiswahili, na lile la "Zuka" (uk. 7) linatoa wito wa kufufua utamaduni wa Mwafrika:
Zuka uwke mzuka,
Utamaduni Afrika!
Yule aliyekuteka
Hatarudi kukuteka!
................................
Zuka, Utathaminika
Zuka, utakumbatika.
Katika kusisitiza umuhimu wa kujirudishia hadhi kwa Mwafrika, washairi wanasisitiza-pia umuhimu wa kuchuja katika ujenzi wa utamaduni mpya:
Chuja, uchuje, mchuja
Utamaduni wa tija
Kumbata ule wa haja
Usikumbate vioja;
Kasumba inayofuja,
Hamna haja kuonja!
Kasumba wanazozipinga washairi hapa ni zile zile anazozikemea Lawino anapomshauri mume wake arudie utamaduni wao badala ya kukumbatia kikasumba tamaduni za nje.
Shairi la "Kitu Nisichokitaka" (uk.10) nalo linawekea mkazo umuhimu wa mtu kuwa na uasili katika utamaduni wake badala ya kuvaa tamaduni za nje zenye kumfanya aooekane kama mwenye nguo iliyojaaviraka. Shairi la "Wimbo Uliosahaulika" (uk.87) haU kadhalika linasuta kuabudu mambo ya nje: kuanzia "mitishamba ya kigeni inayoukwajua mwili wangu" - hapa ikamaanisha madawa ya kigeni kama vile Ambi wanayotumia baadhi ya Waafrika ili kujaribu kuiondoa "aibu" ya weusi wa ngozi zao na kuwafanya wawe weupe kama Wazungu - pamoja na "utumwa (wa) talasimu za kigeni shingoni.../na mizimu nisiyoijua...," mambo ambayo yanaashiria dini na imani ngeni zinazomfanya Mwafrika awe mtumwa wa mawazo nchini mwake. Beti za 4, 5, 6 na 7 za shairi hili zinatoa uamuzi wa hatua za kuchukuliwa katika kurudia utamaduni wa Mwafrika na kutupilia mbali kujidharau.
Japokuwa dhamira kuu katika shairi la "Mlima wa Kimombo" (uk.97) ni ile ihusuyo aina ya elimu itolewayo katika jamii, washairi pia wameihusisha dhamira hiyo na masuala ya utamaduni, kwani katika elimu hii kuna kuvaa "pekosi kike, Nywele za wafu, Kucha za damu." Haya ndiyo yale yale anayoyapiga vita Lawino dhidi ya akina "Klementina'' wa Afrika.
Kwa jumla tunaweza kusema kuwa mashairi yote ambayo yamejishughulisha na masuala ya utamaduni katika diwani hii, hapohapo yameungana na yale yaelezayo maana ya uhuru kwani sehemu mojawapo muhimu ya uhuru wa mtu inahusu kuthamini na kuuamini utamaduni wake.
Uzalendo na Wasifu
Uzalendo ni mapenzi ya mtu kwa nchi yake; ni kipimo cha yale mapenzi aliyo nayo mtu kwa wanajamii wenzake. Kwa maana hiyo ya harakaharaka basi, itadhihirika wazi kuwa "uzalendo" wauonyeshao Kahigi na Mulokozi katika diwani yaMalenga wa Bara umepevuka zaidi ya ule wa Mashairi ya Kisasa uliokuwa wa kuisifu tu nchi katika ukubwa wake: mapenzi yasiyo na welekeo wowote (angalia kwa mfano mashairi ya "Nitaisifu Tanzania" na "Nakuahidi Tanzania")
Mashairi ya "Kwa Shaaban Robert" (uk.5) "Sudi ya Tanzania" (uk.36), "Nchi Yangu Utadiriki" (uk.80) na "Kiswahili" (uk.84), ni ya wasifu na kizalendo, na hapohapo yanamtetea mtu mnyonge. Haya yanaungana na yale ya kumtetea mkulima na masikini, na kudhihirisha kwamba dhana ya uzalendo ni suala la kitabaka. Mtu hawezi kuipenda nchi tu katika ukubwa wake bila kuelekeza hisia zake za mapenzi kwa tabaka fulani katika nchi hiyo. Kwa mfano, katika shairi la "Nchi Yangu Utadiriki", zaidi ya kuonyesha mapenzi yao kwa Tanzania, hapohapo washairi wanasisitiza kuhusu mapinduzi yatakayowainua makabwela baada ya kuzinduka na kutambua uhalisi wa utabaka wa jamii katika ubeti wa mwisho:
Tanzania utadiriki
Kwa taayo ya mapinduzi,
.......................................Watazinduka makabwela,
Watainuka makabwela,
Zitakatweni silisila!
Uzalendo wa akina Kahigi na Mulokozi, basi, si ule wa kuipenda nchi kwa ajili ya kuipenda tu, bali umeelekezwa kwa tabaka la wanyonge kama vile makabwela.
Mapenzi
Robo nzima ya kitabu cha Mashairi ya Kisasa ni ya mashairi ya mapenzi baina ya wavulana na wasichana; mapenzi ya "sili silali". Ijapokuwa hapa na pale ile hali ya "sili silali" inaibuka katika Malenga wa Bara, washairi wamepunguza sana idadi ya mashairi ya mapenzi ya namna hiyo. Wakati ambapo mashairi ya "Barua Kwa..." (uk.39), "Wimbo Kabla ya Kulala" (uk.79), na "Mapenzi" ni ya kuonyesha tu hisia za mtu kwa mpenzi wake, yale ya "Sifa Zako Nitataja" (uk.24) na "Asali ya Nyuki" (uk.83) japokuwa ni ya mapenzi pia, yanatoa ujumbe wenye kupevuka zaidi ya ule wa "sili silali". Kwa mfano katika "Sifa Zako Nitataja", baada ya sifa mzo mzo ambazo zimetolewa kuhusu mpenzi mwenye umbo na sura nzuri sana, tunajulishwa kuwa jina la mpenzi huyo ni Kapesa. Jina hili linatupa maana nyingine ya shairi hili ambayo inaungana na ile ya dhamira ya fedha inavyoabudiwa katika jamii.
Namna Tunavyoishi
Yako mashairi mawili katika Malenga wa Bara ambayo ni muhimu sana kwani yanatoa taswira ya maisha yalivyo katika jamii yetu nyakati hizi. Hayo ni "Namna Tunavyoishi" (uk. 105) na "Zama Hizi" (uk. 113). Kwa vile haya yana umuhimu wake, uchambuzi tutakaofanya wa mashairi haya, hasa wa lile la "Namna Tunavyoishi", utafuata ubeti hadi ubeti; au walau utazingatia mafungu ya beti zenye kushirikiana.
Beti mbili za kwanza za shairi la "Namna Tunavyoishi" zinauliza maana ya uhuru na pia maana ya maisha hasa pale ambapo "uhuru" na maisha hayo yamezungukwa na taabu, vilio, afya mbaya, na watu ambao hawaishi bali wanadumu tu. Taswira hii ya dhiki imesisitizwa katika beti za tatu na nne ambazo zinaeleza jinsi maradhi mbalimbali yalivyoenea katika jamii. Beti za tano hadi kumi na moja zinaonyesha kuwa badala ya kukaa na kulalamikia dhiki, watu wanyonge hawana budi kuharakatika. Washairi wanaziona harakati hizi kuwa sawa na safari juu ya barabara iliyo na kokoto. Wanasema:
Na katika kupigana, hutokea tukakonda
Ya kokoto kalisana, barabara ina nunda
Lakini wanasisitiza kuwa kwa vile umma wa watu hauwezi kukaa tu na kuvumilia dhiki ziletwazo na "zimwi na vifutu" (viongozi wapotofu), basi nguvu lazima itumiwe ili kuleta mabadiliko yanayotakiwa, kwani, kama wasemavyo wenyewe:
Maisha ni harakati, mazingira kuyadhidi
Hajaya kunyonya titi, la uhai kufaidi
Na mtu kila wakati, budi awekejuhudi
Lau kwenye harakati, atashindwa na hashindi.
Katika kuyaangalia maisha ya leo, washairi wameonyesha uzuri na ubaya wa maisha hayo; lakini wamesisitiza ile dhamira ambayo imewashughulisha sana katika ushairi wao: kwamba uhuru si sherehe zisizo na mwisho. Maisha ya leo hayajatufikisha mahali pa kusherehekea:
Haujajiri wakati, wa mtu kushereheka
Akalinyonya na titi, kwa raha kufaidika
Kilasiku harakati, zinazidi kucharuka
Kinyume na E. Kezilahabi katika diwani yake ya Kichomi (Heinemann, 1974) ambamo mashairi yake mengi yanakatisha tamaa, Kahigi na Mulokozi katika Malenga wa Bara, na hasa katika shairi hili la "Namna Tunavyoishi", wamesisitiza kuwa ushindi wa watu wanyonge hauna budi kupatikana kwani lazima "kule mbele kupateka."
Kwa Kahigi na Mulokozi, dunia ya leo imezungukwa na uovu na uozo mwingi sana ambao lazima upigwe vita japokuwa baadhi ya mafundisho ya dini hudai kuwa mabaya yote yatalipizwa siku ya kiyama. Wanasema:
Japo Dini zimezuwa, etimoto utazima
Bali sisi tunajuwa, kuwa hakuna kiyama
Mwanga wa moto muruwa, hakuna wa kuuzima.
Kwa washairi hawa, zama zetu bado si za uhuru kamili, ndiyo maana shairi linamalizia na wito wa kusimama imara kuuwania uhuru ili kuangamiza dhiki na kuleta "ngoma mpya ya dunia."
Maudhui ya shairi la "Zama Hizi" yanalandana sana na ya shairi la "Namna Tunavyoishi". Shairi linasisitiza kuwa dhiki zimekithiri, magonjwa yamesambaa, na uhuru si uhuru kamwe: hata ule "uhuru" uliopatikana mwanzo umetekwa nyara huku wale walioshiriki katika kuupigania wanaendelea na maisha duni:
Sasa asaliya Uhuru yaliwa na kiboko wa inda,
Na mashujaa wajana walamba midomo mikavu
Kote kuna vilio vya nyasi na miti inayoungua
Dhamire Nyinginezo
Katika kuchambua dhamira mbalimbali zinazojitokeza katika Malenga wa Bara tumeorodhesha mashairi kadhaa kwa kila dhamira. Mashairi hayo yanawakilisha tu orodha ndefu zaidi, na ni juu ya msomaji kuyaangalia yale ambayo hayajaorodheshwa na kujaribu kuyachambua na kuyaainisha.
Hata hivyo, hapa tutaangalia baadhi ya mashairi mengineyo ambayo kidhamira yanajitegemea.
Shairi la "Jua la Dhahabu" (uk.18) linaongelea Azimio la Arusha na jinsi ambavyo, sawa na jua,
Miali yake imepenya
Anga la nchi yangu
Na kukifukuw kiw
Kiza kinachoongelewa hapa ni ubepari na unyonyaji ambao ulipigwa vita na Azimio la Arusha. Jua hili linatakiwa liwake ili liwamulikie wanyongc vidato vya kupandia kuelekea kwenye neema na maendeleo yatakayowasha tabasamu katika mioyo yao. Nguvu hizi za Azimio zimeelezwa pia katika shairi la "Ngoma ya Radi" (uk.110) ambalo Umeonyesha jinsi ngoma hiyo ilivyowazindua wanyonge.
Kati ya mashairi yote ya diwani hii, shairi ambalo linaonekana limekosa welekeo, halina kichwa wala miguu, ni lile la "Vita" (uk.l9) lenye beti zote ishirini na mbili zikishangilia vita ambavyo hatuelezwi ni vya nani, bali kupewa tu vidokezo vinavyopwaya katika ubeti wa pili na wa tatu vyenye kugusia kuwa vita hivi ni vya watu ambao,
Bezo wamepita
Kwonyesha wataka, kuwasio duni
Kwonyesha hakika, kuwa si manyani
Vidokezo hivi havitoshi kutueleza kwa hakika kama vita hivi ni vya kumpigania nani hasa.
Shairi la "Buyu la Kaya Limevunjika" (uk.29) ni la maombolezo na kilio cha watoto kwa kutokwa na mama yao. "Buyu la kaya" ni ishara ya shibe na uhai, kwani aghalabu buyu hutunzia maziwa ambayo hupendwa sana na watoto. Lakini pia katika shairi hili nafasi, na hata dhana ya mama katika familia imeelezwa. Twaelezwa kuwa wakati mama alipokuwa hai nyumba ilikuwa inang'ara na kunukia. Ila:
Sasa uchafu umetanda, mnuko umechacha
Na haipo furaha,
Shairi hili basi, linaonyesha kuwa nyumba bila mama si nyumba: ni mahame ambamo hamna uhai, furaha wala raha.
Shairi la "Soga" (uk. 85) - shairi ambalo linatumia sana ucheshi katika kuyatoa maudhui yake - linaasa kuwa kila hali na kila kitu kina pande kuu mbili, na kusisitiza dhamira ya nguvu za pesa katika jamii. Washairi wanasema:
Na dunia ni mfuko na nchi zote ni masoko!
Fedha ndiyo bwana, fedha ndiyo Mungu
Anayekanusha hamjui Mungu!
Washairi wameamua kumalizia diwani yao kwa shairi lenye kuleta matumaini kwa wanyonge. Shairi la "Siku Imefika" (uk.120) linaeleza jinsi ukoloni wa Mreno ulivyoangushwa, na jinsi kaburu anavyopapatika kutokana na harakati za ukombozi. Ni shairi la nderemo, chereko-chereko na la kuleta matumaini mema kwa wote wanaonyonywa, wanaonyanyaswa na kuonewa.
MATUMIZI YA BAADHI YA VIPENGELE VYA FANI
Katika kuzichambua dhamira mbalimbali za Malenga wa Bara, kila mara tumekuwa tukigusia pia masuala ya fani. Kwa mfano, katika kuiangalia dhamira ya "Maana ya Uhuru" tulitaja jinsi taswira ya safari ilivyotumika kueleza dhana ya uhuru. Mashairi ya "Vuteni Makasia", "Kwenye Safari Barabarani", "Msafiri Mpya" (uk.40), na "Kauli ya Mzee" (uk. 22) yametumia pia kipengele cha fani cha taswira ya safari kutolea maudhui yake yahusuyo harakati za ukombozi za kujitafutia uhuru kamili. Vipengele vingine vikuu vya fani walivyotumia Kahigi na Mulokozi katika diwani yao ni:
1. Tamathali za semi
2. Misemo, methali na nahau
3. ishara ya ngoma
4. Taswira za usambamba
5. Majigambo
6. Mtindo wa tambo
7. Mtindowavinanamizani.
Tamathali za Semi
Tamathali za semi zimetumiwa katika mashairi mengi humu kutajirisha maudhui, na pia kuleta picha kamili ya lile wanaloiieleza washairi.
Mathalani, katika sbairi la "Vuteni Makasia" tunaelezwa hivi kuhusu mwendo wa mashua:
9. Mashua ikenda ikichachamaa
Uso wa bahari ikiuchubua
Hii ni tashihisi, kwani, kama tujuavyo bahari haina uso uwezao kuchubuliwa, bali uso huu ni wa kuwazika tu.
Shairi la "Maombolezo ya Mtu Masikini" limejazana tamathaii zenye kuonyesha undani wa dhiki za mtu masikini kama vile "panya wa uhitaji", "simba wa ubeberu", "matiti ya uwingu wenye ubahili". Yote haya yamesaidia kueleza vizuri zaidi dhiki hizo kuliko vile ambavyo ingekuwa kama washairi wangetumia maneno kama vile "ubeberu mbaya", "maradhi mengi", na kadhalika, ambayo ni ya kawaida mno.
Katika shairi la "Sima na Mayai" mzazi anamuasa kijana wake kwa njia ya tamadhali asemapo:
16. Usiniache kufw kando ya njia
Kama mwanamke mgumba
Usiniache ning'oke kamo muyombo
Usio na mzizi wa hati
Tamathali ya tashbiha imetumika - hapa kusisitiza umuhimu wa wasomi kuwahudumia wale wahowasomesha. "Mwanamke mgumba." "kokwa lisilo na mbegu" na "muyombo usio na mzizi wa kati" ni ishara za viumbe wasio au visivyo na uwezo wa kuendeleza uhai duniani. Mzazi anayelalamika katika shairi hili wakati huohuo anamdai kijana wake kuwa yeye si nigumba, si kokwa lisilo na mbegu wala si muyombo usio na mzizi wa kati kwani tayari ameshadhihirisha uwezo wake wa kuendeleza maisha kwa kumzaa kijana huyo msomi. Uwezo huo pia tunaweza kuuchukulia kiishara kuwa ni kule kujitolea kwa mzazi au jamii kuwasomesha vijana.
Mfano mwingine wa matumizi ya tamathali umo katika shairi la "Kwa Shaaban Robert" ambako twaelezwa kuwa maandishi yake ya kudumu yanakata "kama panga.''
Ni dhahiri kuwa iko mifano mingi mingine ya tamathalt za semi katika diwani hii ambayo wasomaji huweza kuitafiti na kuigundua wenyewe.
Misemo, Methali na Nahau
Mashairi kadhaa katika diwani hii yametumia misemo, methali na nahau si kama njia ya kupamba tu bali pia katika kutajirisha yale yanayoongelewa.
Mathalani, katika shairi la "Saa ya Mwisho, (uk. 10) msemo wa "Nguvu huvunjwa na pesa" umetumiwa kuonyesha nguvu za pesa katika jamii.
Shairi la "Mlima wa Kimombo" nalo limetumia methali kadhaa kuwa njia ya jadi ya kupinga kukumbatia utamaduni wa kigeni bila kuchuja. Misemo na methali kama "Mtoto mwenye njaa haonyeshwi titi," "Muwinda ndege huzunguka apajue mahali mtama ulipomalizwa na ndege," "Utokapo nje huwa kware," "Uzuri wa tunda la mtwetwe ndani limeoza," "Anayekohoa na kutema huwa anapunguza ugonjwa," "Mto unaotiririka haurudi nyuma," na kadbalika; ni raifano mizuri ya pamna misemo na methali vinavyotumiwa kuyajenga maudhui. Kwa mfano, katika methali ya "Mto unaotiririka haurudi nyuma" kuna fundisho la kutokukata tamaa katika harakati za kujikomboa; fundisho ambalo ndani yake pia lipo tumaini la ushindi.
Ishara ya Ngoma
Katika baadhi kubwa ya jamii za Afrika, ngoma hutumika kwa wito au kwa ajili ya vifijo na hoihoi za ushangiliaji.
Katika Malenga wa Bara, ngoma imetumika kwa makusudi hayo hayo. Katika shairi la "Kwenye Safari Barabarani", kwa mfano, washairi wanasema:
10. Najinsi tuendeavyo lengo lile,
Ndivyo jinsi ngoma zetu lelelele,
Ziongezavyo mipwito ya kelele
Kelele zizochangamana rajua.
Mipwito hii ya ngoma ni ishara ya ushindi ambao hauna budi kupatikana katika vita vya ukombozi wa watu wanyonge.
Shairi la "Sherehe" (uk.49) pia limetaja ngoma katika beti zake nyingi likieleza jinsi "ngoma mafungu mafungu" zitakavyochezwa katika sherehe hii (ambayo hata hivyo, hatuoni msingi wake). Ni sherehe, vicheko, vifijo na ushangiliaji wa jambo ambalo washairi hawatuonyeshi kinagaubaga kuwa ni jambo gani.
Mstari wa mwisho kabisa wa shairi la "Namna Tunavyoishi", unasema: "Kwa sababu haisiti, ngoma mpya ya dunia." Hii "ngoma mpya ya dunia," sawa na ile tuikutayo katika shairi la "Ngoma ya Radi", ni tangazo la maisha mapya; ni mbiu ya mgambo kuhusu maisha ya usawa, haki na upendo baina ya watu watakapojikomboa.
Taswira za Usambamba au Ulinganishi
Taswira ziitwazo za usambamba au za ulinganishi ni zile ambazo hutupa nyuso mbili za jambo katika kujenga maudhui fulani. Kwa mfano, katika riwaya ya Kasri ya Mwinyi Fuad, (TPH, 1974) taswira ya usambamba mapatikana katika maelezo ya rana na anasa za masikani ya mamwinyi yalinganishwapo na maelezo ya umaskim na unyonge wa masikani ya watu wa hali za chini kama vile nyumbani kwa Mzee Sharwani.
Kwa upande wa ushairi pia, taswira za usambamba zimetumiwa na washairi tofauti. Tutatoa mifano nuwili ya mashairi yaliyotumia taswira za namna hii katika Matenga wa Bara. Mashairi hayo ni ya "Sima na Mayai" na "Habari Mpya."
Katika shairi la "Sima na Mayai," maelezo ya maisha ya mkulima masikini (beti za 2, 4, 6, 8, 10, 12, 13, 14, 15, 16, 17) yameelezwa, sambamba na yale ya msomi mwenye nafasi nzuri kiuchumi (beti za 1, 3, 5, 7, 9 na 11). Usambamba huu unatusaidia katika kulinganisha maisha ya watu wa aina hizo mbili.
Kutokana na taswira hizi za mlinganisho sisi wasomaji tunaiona sima ya mtama upande nunoja, na upande wa pili tunaliona rundo la mayai si kwa maana ya moja kwa moja ya vyakula hivyo, bali kwa dhana iletwayo na mlinganishao wa taswira hizi mbili. Katika mlinganisho huu tunapata ufafanuzi wa ndani zaidi unaohusu masuala ya elimu, siasa, uchumi, utaroaduni na utabaka wa jamii.
Taswira za usambamba na za mlinganisho zinajitokeza pia katika shairi la "Habari Mpya". Humu tunalinganisha maneno ya Kasisi na ya "kijana mmoja pandikizi", na hatimaye Kasisi anapofariki, tunaupata ujumbe uliokusudiwa.
Majigambo
Matumizi ya majigambo si jambo geni katika ushairi wa Kiswahili. Tangu zamani yamekuwa yakitumika sana, hasa katika mashairi ya malumbano ambamo washairi walijitapa na kuringia ushairi wao kwa nia ya kuwadunisha washairi wengine walio "adui" zao katika mijadala mbalimbali.
Katika Malenga wa Bara mbinu hii ya majigambo haikutumiwa sana, na pale ilipotumiwa imeongeza nguvu za shairi linalohusika. Katika shairi la "Kauli ya Ununa" (uk.89) kwa mfano, washairi wameonyesha nguvu za kauli ya umma kwa majigambo yaliyojengwa ndani ya tamathali ya sitiari. Umma umeitwa "Nyundo" ambayo ina:
ulimi: ncha yenye kingo
Hukatisha nyemi, hubomoa nyongo
Ni mkoma wami ningiapo zogo.
Huu ni umma ulioshikamana kwa umoja kukataa ulwana.
Majigambo yamerudiwa katika shairi la "Soga" (uk.85) ambamo kwa njiaya ucheshi washairi wanapinga "Unyama" (bila hasa kutueleza ni unyama gani wanaouongelea) kwa kusema:
13. Jina langu Nyundo unanijua,
Kila nikidunda ninapasua...14. Bali fuadini sitaki unyama!
Mtindo wa Tambo
Mtindo wa tambo hutumia mafumbo katika utoaji wa maudhui ya shairi. Tambo huwa sawa na kitendawili ambacho msomaji anatakiwa akifumbue. Katika malumbano washairi wengi walitumia mashairi ya tambu kuwafumbia washairi wenzao ili wakune vichwa kwanza kabla ya kuvumbua yale yaliyokusudiwa na waliyoaandika. Tumeona jinsi shairi ia "Vuteni Makasia" lilivyo tambo ambalo ndani yake mmejificha maana ya uhuru.
Shairi la "Usemi wa Nyoka" nalo ni la tambo. Limetumia ucheshi kwa kumtumia nyoka ambaye baada ya kujigamba mbele ya kadamnasi inambidi atoroke harakaharaka ili kujihami na ghadhabu za tembo. Katika fumbo hili liko fundisho kuwa kujitapa si tabia njema.
Shairi la "Asali na Nyuki" (uk. 83) nalo pia ni mfano mzuri wa aina ya tambo; na katika fumbo hili msomaji anaweza kutoa maana mbalimbali. Malhalani, asali huweza kuwa uhuru, mapenzi au jambo lolote lile analolitamani mtu hadi anajitolea kwa hali na mali ili alipate.
Mtindo wa Vina na Mizani
Katika diwani ya Malenga wa Bara, washairi hawakufungwa na mtindo wa aina moja wa ushairi. Humu imo mitindo mbalimbali, tangu ile ya kimapokeo yenye mpangilio mahsusi wa vina, mizani, na beti, hadi ile ya kisasa ambayo huamuliwa na kuainishwa na kile kiongelewacho. Kwa vile mtindo wa kimapokeo umezoeleka kwa baadhi kubwa ya wasomaji, hatutaushughulikia humu. Zaidi tutaangalia ile mitindo ambayo huenda ni migeni kwa wasomaji wengine japokuwa watakapoichunguza kwa undani wanaweza kuigundua hata katika nyimbo na ushairi wa makabila yao.
Katika shairi ia "Zuka" (uk. 7), washairi wameanza na ubeti ufuatao kanuni za kimapokeo kwa kutupa mistari yenye nuzani minane minane ambayo huishia na kina cha "ka". Ubeti wa pili wa shairi hili ni mchanganyiko wa mitindo ambamo ndani yake kina cha "ma" kimctawala. Wamefanya makusudi kabisa katika ukurasa uliotangulia kuandika katika mtindo wa mjazo uonekanao wa kinathari. Mtindo huu umetumiwa kwa sababu kubwa mbili: Kwanza, kuonyesha mabadiliko va msimuliaji kuwa sasa ni sauti ya watu na si ya msimuliaji wa nafsi ya kwanza; na pili, kuonyesha kuwa dhana ya mistari katika beti za shairi ni matokeo ya uandishi na kamwe isije kuchukulika kuwa kigezo cha sheria na kanuni za ushairi wa Kiswahili.
Baada ya hapo, washairi wamebadili tena mtindo na kutupa ubeti wenye kanuni sawa na ule wa kwanza. Kanuni hizi ni za mizani minane minane na kina cha "ja" kwani maneno ya ubeti huu yanatolewa na sauti nyingine. Hata katika ubeti unaofuatia yanatokea mabadiliko ya mtindo kwa sahabu hizo hizo. Hapa kuna kina cha "ji" ambacho kinatokea ndani kwa ndani badala ya kuwekwa katika sehemu mahsusi tu. ''Ubeti" wa mwisho, mfupi kuliko zote, ni wa hitimisho ambalo linabeba uzito wa aina yake:
Watu wanasikia,
Tangazo la zinduko jipya,
Mimi nimeshasiksa.
Ni wazi kuwa "tangazo hili" linaonyesha uzalendo uliopevuka zaidi ya ule wa kuipenda tu nchi tuukutao katika diwani ya kwanza ya washairi hawa ya Mashairi ya Kisasa.
Kuhusu vina, wakati mwingine washairi hawa wameviweka vina mwanzoni mwa baadhi ya mistari. Kwa mfano, katika shairi la "Jua la Dhahabu" ubeti wa tatu neno "Waka" limeleta vina na mapigo ya aina yake katika mianzo ya mistari kadhaa.
Washairi wanatumia sana mtindo wa marudiorudio ya maneno ili kusisitiza jambo, na wakati huohuo kuleta mapigo ya aina fulani. Kwa mfano katika mashairi ya "Siku Itafika" na "Siku Imefika" meneno ya vichwa hivyo yamerudiwarudiwa sana kusisitiza kwanza tumaini jema la wanyonge, na pili cherekochereko za ushindi. Vivyohivyo katika shairi la "Vilio vya Dhiki" jina la shairi limerudiwarudiwa kuonyesha wingi wa vilio hivyohivyo vinavyodai haki.
Katika shairi la "Sima na Mayai", japokuwa kuna kumdiwarudiwa kwa maneno "nikumbuke" na "kumbuka" ili kuwasisitizia vijana wasomi juu ya umuhimu wa kuikumbuka na kuitumikia jamii iliyowasomesha, mtindo hasa uliotumika ni ule wa ushairi huria wenye kulandana na msimuliaji (narrator) ambaye ni mkulima mzee na masikini.
Hii ni mifano tu ya baadhi ya mitindo waliyoitumia washairi hawa. Ni dhahiri kuwa iko mitindo mingi sana humu. Kwa mfano, japokuwa katika shairi la "Mlima wa Kimombo" mtindo wa vina na mizani wa kimapokeo unatumika, washairi wamechanganya pia mitindo mingine kufuatana na mambo tofautitofauti wanayoyashughulikia.
Mara nyingi wasimuliaji katika mashairi haya ni wa nafsi ya kwanza, "mimi", nafsi ambayo inafaulu kutufanya tuyaamini zaidi yale yasemwayo kuwa yanatokana na uzoefu wa kuyaishi maisha wayaelezayo.
Labda kwa kumalizia tungetahadharisha tu kuwa Kahigi na Mulikozi hawana vita wala uadui na ushain wa kimapokeo. Kwa hakika tukichunguza sana zaidi ya nusu ya mashairi yao katika Malenga wa Bara ni ya kimapokeo yenye kuzirigatia masuala ya vina na mizani. Jambo hili ameshindwa kuliona Jumanne Mayoka ambaye upinzani wake katika kitabu chake cha Mgogoro wa Ushairi na Diwani ya Mayoka (TPH, 1986) unaonyesha dhahiri kuwa hajakisoma kitabu chaMalenga wa Bara. Tena wakati mwingine katika kujaribu kuzingatia mno vipengele hivi vya vina na mizani baadhi ya mashairi ya Kahigi na Mulokozi yamekuwa na udhaifu. Kwa mfano katika shairi la "Kwa Shaaban Robert" ili kuleta mlingano wa kina cha "ni" kwenye beti za 3, 8, na 9, washairi wametumia maneno "uliyoyaandikeni", "uliyotu-achieni" na "tunakuoneni", ambayo husemwa kwa watu wengi na si kwa mtu mmoja kama walivyofanya hapa.
Udhaifu mwingine ni ule wa kawaida wa ngonjera za Mnyampala ambamo mhusika mmoja hubadilika ghafla katika msimamo wake. Katika "Ngonjera" (uk.43-49), ni vigumu kuamini mabadiliko ya mawazo ya Kijana anayeamka ghafla na kuwa mwanamapinduzi wakati ambapo muda mfupi sana uliopita alikuwa mbumbumbu hasa.
Hata hivyo, ni dhahiri kwamba Kahigi na Mulokozi wamefaulu katika kushughulikia masuala mbalimbali ya kijamii-ya siasa, utamaduni na uchumi - katika mashairi yao kwa kutumia ufundi wao wa t'ani katika kuyatolea maudhui yaMalenga wo Bara.
Maswali
1. "Kahigi na Mulokozi wamefaulu kushughulikia masuala mbalimbali ya kijamii na pia katika ufundl wao wa kisanii kwenye Malenga wa Bara "Jadili.
2. "Kahigi na Mulokozi wanashauri katika baadhi kubwa ya mashairi yao kwamba watu washike marungu, mapanga, bunduki na risasi wauane bila sababu za kuridhisha." Jadili hoja hii na uthibitishe kwa mifano dhahiri.
3. Je, mawazo ya Kahigi na Mulokozi kuhusu Mungu, dini na maana ya maisha ni yapi katika Malenga wa Bara?Unayaonaje mawazo hayo?
4. Chagua dhamira mbili kati ya zifuatazo na ujadili zilivyojitokeza katika diwani ya Malenga wa Bara:
(a) Maanayauhuru
(b) Kumtetea mkulima
(c) Uzalendo
(d) Mapenzi.
5. Jadili kufaulu au kutokufaulu kwa fani ya mashairi ya Malenga wa Bara katika kuyashughulikia maudhui.
6. Chagua vipengele vitatu vya fani ya ushairi kati ya vifuatavyo na ujadili vilivyotumika katika Malenga wa Bara:
(a) Majigambo
(b) Misemo, methali na nahau
(c) Taswira ya safari
(d) Ishara
(e) Tamathali za semi.
Comments
Post a Comment