SHAIRI: KAMA MNATAKA MALI

Myaka kumi imepita,tangu uache wosia,
Mema mengi tumepata,baba sitokuchukia,
Leo hii nakufwata,najua utasikia,
Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni.


Zama ile tulipata,ila leo ni shughuli,
Leo shamba kulipata,uwe una hela kweli,
Wabunge wanayapata,ama wale wenye mali,
Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni.


Shule niliikamata,lakini kazi sioni,
Hata miti nikikata,mnunuzi yu mashambani,
Faida siji kupata,labda nifike sokoni,
Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni.

Chochote huwezi pata,usipo weka mbolea,
Hiyo mbolea kupata,mazao yanyong'onyea,
Nauongeza ukata,shambani kutegemea,
Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni.

Kaka wamemkamata,eti shamba kavamia,
Japo kwako tulipata,baba ulituachia,
Mweupe amekamata,weusi wawatimua,
Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni.

Kuna habari napata,kaburi kulifukua,
Wapi haki nitapata,niweze kuwazuia,
Nikipinga wakamata,nami ndani kunitia,
Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni.

  NAAMINI UMEKUMBUKA MBALI

Comments

Popular posts from this blog

NOTES ZA USHAIRI

MBINU ZA KUFUNDISHIA

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI