Skip to main content

SHAIRI: MWANANGU NGAO

Mwanangu leta mkeka, utandike upenuni,
Najua unanicheka, kujanika juani,
Sijali naneemeka, na wewe ukae chini,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.


Mwanangu kuna magumu, ya kusemwa na kutendwa,
Nusu tuzilambe sumu, kukufanya ukalindwa,
Tukakubali hukumu, ili usije kupondwa,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Ile aibu ya mwaka, aliyoileta dadako,
Mioyo ikatuwaka, alipoumwa kakako,
Mamako anazeeka, kisa kero za babako,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Shule wafukuzwa ada, madeni huku na kule,
Twachekwa sie wa shida, kufanya mwanetu ule,
Huku na huko ni mada,tunanyoshewa vidole,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Siku nimekengeuka, namnyanyasa mamako,
Mamako hakugeuka, kaficha kulinda jiko,
Na nyumba haikubomoka, akailinda miiko,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Mishale ilituchoma, na miiba kututesa,
Na wala hatukukoma, na hatukomi sasa,
Twasema mwanangu soma, ‘siharakie usasa,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Hatuoneshi makovu, ama kuzinena shida,
Muhimu kwepa maovu, na uishike ibada,
Usijezitaka mbivu, kabla ya kufika muda,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Nilimsumbua mama, nilivyokuwa mtoto,
Nilimwona kasimama, mie damu ya moto,
Na leo inaniuma, sikuwa mwema mtoto,
Mwanangu mzazi ngao, kaficha makovu mengi.

Yauma sikuwa bora, kuigundua huzuni,
Sikuziona busara, nikaziweka kichwani,
Nikaivuna hasara, mama ninamtamani,
Mwanangu mzazi ngao, anayo makovu mengi.

Nakuona wasinzia, na kijua chanichosha,
Sijui yamekwingia, ama ndio nakuchosha,
Wanao ‘tasimulia, na wao utawachosha,
Mama kapika viazi, vipi wawaza mikate?

Comments

Popular posts from this blog

KISWAHILI FORM 1: FASIHI SIMULIZI

KISWAHILI Form 1 Topic 4 FASIHI SIMULIZI Fasihi simulizi ni moja kati ya tanzu za fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Katika mada hii utajifunza na kisha utaweza kubainisha tanzu na vipera vya fasihi simulizi pamoja na ufafanuzi wake. Na pia utaweza kutofautisha kati ya kipera na kipera au kati ya utanzu na utanzu. Ubainishaji wa Tanzu za Fasihi Simulizi Tanzu za Fasihi Simulizi Bainisha tanzu za fasihi simulizi Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. Tanzu za Fasihi Simulizi ni pamoja na hizi zifuatazo: Masimulizi/hadithi Semi Ushairi Mazungumzo Maigizo Ngomezi Ufafanuzi wa Vipera vya Tanzu za Fasihi Simulizi Vipera vya Hadithi Fafanua vipera vya hadithi SIMULIZI/ HADITHI Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulan...

MBINU ZA KUFUNDISHIA

Mbinu za kufundishia , ni miongozo mbalimbali atumiayo mwalimu wakati wa kufundisha somo aliloliandaa kwa wanafunzi wake. Walimu wanapaswa kuamua kwa kuchagua kwa makini njia na mbinu bora za kufundishia ili wanafunzi wake waweze kujifunza kwa ufanisi. Ziko njia nyingi za kutengeneza mazingira ya mtoto aweze kujifunza na pia ziko mbinu nyingi za kufundishia. Pamoja na wingi huo tunaweza kuzigawa katika makundi makuu mawili kadri ya jinsi zinavyowashirikisha watoto katika tendo la kujifunza, ambazo tunaweza kuziita shirikishi na zisizo shirikishi . Zifuatazo ni baadhi ya mbinu shirikishi na zisizo shirikishi za kufundishia pamoja na faida na hasara zake:- Njia ya majadiliano , njia hii imekuwa ikitumika katika ufundishaji kwa muda mrefu. Katika kujadiliana mwanafunzi mmoja mmoja hupata nafasi ya mawazo aliyonayo kuhusu suala linalojadiliwa na yeye pia huweza kupata mawazo yaw engine. Katika majadiliano mwanafunzi hupata ujuzi mpya nje na ule aliokuwa nao kabla hajashiriki kat...

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI

Ushairi kama moja kati ya tanzu za fasihi inayowasilishwa katika namna zote aidha kwa lugha ya maandishi au kwa lugha ya masimulizi una mchango au nafasi kubwa sana katika kunufaisha au kustawisha maisha ya binadamu kwa kumuelimisha, kumsisimua, kutunza na kuhifadhi amali zake pamoja na kukuza na kuendeleza lugha yake kama moja kati ya vipengere muhimu maishani mwake. Ushairi kama nudhumu katika fasihi simulizi hujumuisha nyimbo, ngonjera, tenzi na mashairi yenyewe. Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au katika kumbo mbalimbli kama asemavyo Mulokozi (1996) kuwa zipo kumbo kuu tatu ambazo ni ushairi wa kijadi au kimapokeo, ushairi wa mlegezo au huru na ushairi wa maigizo. Wanazuoni wafuatao wa mashairi ya kimapokeo wametoa maana za ushairi kama ifuatavyo:- Shaaban Robert (1958:37). “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari…, mawazo, maoni na fikra za ndani zi...