Kamezuka kamsemo,kuhusu hizi siasa,
Naomba nipewe somo,ili nisije kukosa,
Siyo ya sasa michomo,kila siku yanigusa,
Kuwa rangi ya kijani,ushamba na umbulula?
Naomba nipewe somo,ili nisije kukosa,
Siyo ya sasa michomo,kila siku yanigusa,
Kuwa rangi ya kijani,ushamba na umbulula?
Kijiweni wasakamwa,bila ya kupewa hoja,
Na madole utachomwa,uonekane kiroja,
Na mjinga utaonwa,bila hoja hata moja,
Ujanja kuwa antena,kivipi muniambie?
Wewe bado ni mbumbubu,chama gani walipenda,
Siasa siyo kabumbu,kijani dhambi kupenda,
Chafanya kuwa ka mbu,kila siku tunakonda,
Washindwa kunishawishi,matusi yatanivuta?
Utajitwisha uhuni,kwa njia utumiayo,
Nayo lugha ya kampeni,siyo zinivutiayo,
Matusi kutia ndani,hilo hamtii choyo,
Hakuna neno lingine,hadi ukatia tusi?
Wala si sera ya chama,nahisi hawa wahuni,
Hawana kadi ya chama,hawaendi vikaoni,
Watakiharibu chama,kuitwa ni cha wahuni,
Huwezi kumshawishi,bila kumdhalilisha?
Mie napenda siasa,siyo kulibeba jimbo,
Ndugu zangu nawaasa,yaacheni majigambo,
Ntajitenga na siasa,sipoacha haya mambo, KITAKA ASIWE NJANO,MSHAWISHI SI MATUSI.
Comments
Post a Comment