SHAIRI: NILIPOKUWA MATEKA


Si wote waliojua,zaidi ya mtekaji,
Mwenyewe sikutambua,nikajisi mjuaji,
Wale walonililia,nikahisi wauaji,
Nilipokuwa mateka,niliwaumiza wengi.



Nilitenda atakavyo,aliyeniteka akili,
Nilipoambiwa sivyo,sikutaka kukubali,
Na nikawajibu ovyo,nikitusi kwa ukali,
Nilipokuwa mateka, niliwaumiza wengi.



Mwanangu na mama yake,walinililia kutwa,
Akakonda bibi yake,hofu ya mwana kuachwa,
Na mawazo yangu kwake,ni kama yalishafutwa,
Nilipokuwa mateka,niliwaumiza wengi.



Marafiki na babangu,waliniona wazimu,
Nilimsahau na Mungu,na sikuhofu kuzimu,
Nikapuuza uchungu,wa mama yangu muhimu,
Nilipokuwa mateka,niliwaumiza wengi.



Mtesi nikamwamini,kila asemalo sawa,
Dada atasema nini,ni'shajiotesha mbawa,
Sijui cha ibadani,na pombe ikawa dawa,
Nilipokuwa mateka,niliwaumiza wengi.



Lile chozi la mamangu,mwanangu na mama yake,
Pia sauti ya Mungu,kupitia watu wake,
Imekuwa tiba kwangu,nipo huru mtu wake,
Nilipokuwa mateka,niliwaumiza wengi.



Nisamehe walimwengu,nisamehewe mbinguni,
Pole na kipenzi changu,unirejeshe moyoni,
Sasa naona uchungu,najua mateka nani,
Nilipokuwa mateka,niliwaumiza wengi.



Mwanangu usinizile,pole kwa yote magumu,
Yasahau yote yale,zikutoke zote sumu,
Yameshapita ya kale,na wala usilaumu,
Nilipokuwa mateka,niliwaumiza wengi.



Mama mkwe nakuomba,yasamehe yalopita,
Usimwambie mjomba,tayari nimeshajuta,
Mbuzi usije muomba,mwenyewe nitamleta,
Tutambike tule na tunywe,tufurahi tusahau.

''Kauli za Makabwela 2017''

Comments

Popular posts from this blog

NOTES ZA USHAIRI

MBINU ZA KUFUNDISHIA

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI