SHAIRI: NISEME NINI UJE KWANGU


Kila nikifikiria,ninashindwa kuamua,
Sawa ningevumilia,ila penzi lasumbua,
Kipi sijamwambia,pendo langu kulijua,
Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu.

Neno nimeshachelewa,lanifanya nikose nguvu,
Hasa ninapogunduwa,kisa ni uvumilivu,
Ni kweli hakuelewa,ishara zangu na wivu,
Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu.

Sasa nina taabika,na pendo langu hewani,
Si mchezo nateseka,kasema lirudi ndani,
Nashindwa hata kucheka,sipo tena furahani,
Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu.

Rafiki niseme nini,huyu mtu aje kwangu,
Najua haniamini,atesa fikira zangu,
Mwambie aniamini,mawazo yarudi kwangu.
Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu.

Mwambie napenda Mori,sina utani kwa hili,
Leo mie sina gari,kwenye gari siyo mbali,
Nikikosa nina sori,ya kizungu na kiswahili,
Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu.

Pia mwambie ukweli,wengi wanamtamani,
Hawajui yake hali,wao wapenda kimini,
Tatizo la wake mwili,wakijua hataamini,
Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu.

Wengi nimeshawaona,wakilia kwa uchungu,
Na ngumu sana kupona,wabaki kusema Mungu,
Sipendi kwake kuona,aje kukufuru Mungu,
Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu.

Kaditama ninatua,uufikishe ujumbe,
Mie moyo waugua,sina nguvu hata chembe,
Awai kumgundua,yule wake kama wembe,
Ataumizwa na kulizwa,nipo chaguo lake.

Comments

Popular posts from this blog

NOTES ZA USHAIRI

MBINU ZA KUFUNDISHIA

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI