SHAIRI: U WAPI UJITOKEZA

Nakukumbuka kwa jina,kisa mama,alikwita,
Si Jojina Saraphina,Sarah pia aliita,
Mora moja nilikwona,siku kwenu ninapita,
Uwapi ujitokeze,walisema upo Dar.

Nilibadili na njia,kisa kwenu kupapita,
Jina lililipatia,kumbe nawe ulipita,
Wenyeji nawasumbua,hadi mwizi wananita,
U wapi ujitokeze,walisema upo Dar.

Walijua twajuana,hata jina nikakwita,
Sikuwa makini sana,japo moyo ulipwita,
Nilijua ningekwona,nikirudi nakukuta,
U wapi ujitokeze,walisema upo Dar.

Kwa yeyote ajuaye,alipo wangu muhibu,
Aseme alipo yeye,kila swali nitajibu,
Katoka Njombe yeye,mtoto wa baba bubu,
U wapi ujitokeze,walisema upo Dar.

Rangi maji ya kunde,urefu wa wastani,
Nywele lazima upende,kope hadi natamani,
Jino la mbele upande,na kamwanya ka thamani,
U wapi ujitokeze,walisema upo Dar.

Kama umeshaolewa,Sarah sema nitambue,
Nijuwe nimechelewa,ili nisikusumbue,
Mwenzako ni muelewa,sema moyo uamue,
U wapi ujitokeze,walisema upo Dar.
Kama bado njoo kwangu,sina mwingine banati,
Hutoupata uchungu,mwenyewe tapiga goti,
Michepuko nungunungu,hailengwi kwa manati,
U wapi ujitokeze,walisema upo Dar.

Mwisho mama utambue,moyo wangu umependa,
Kwani tangu siku ile,wengine kutwa wadunda,
Na pia nikuambie,wajua kipi wapenda,
U wapi ujitokeze,walisema upo Dar.

Comments

Popular posts from this blog

NOTES ZA USHAIRI

MBINU ZA KUFUNDISHIA

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI