SHAIRI: WAKATI RAFIKI MWEMA

WAKATI
Huyu ni rafiki mwema,hana unafiki katu,
Wala hahofu kusema,kwa miti hata watu,
Liwe baya liwe jema,kuficha hatothubutu,
Wakati rafiki mwema,hajawahi kuongopa.


Hajawahi kuogopa,ama kuona aibu,
Hohe hae kwa vibopa,wakati kwao jawabu,
Ya ukweli atakupa,hata kwa kukuadhibu,
Wakati rafiki mwema,husema kweli daima.

Husema kweli daima,tena bila kuamuru,
Uwe chali uwe wima,wakumbuka ya Kaburu,
Hasemi ufanye hima,ama jifanye kunguru,
Wakati rafiki mwema,daima namthamini.

Daima namthamini,namfanya mali yangu,
Afanya nijiamini,sihofii mwisho wangu,
Kaskazi na kusini,kwa weusi na wazungu,
Wakati rafiki mwema,haujui unafiki.

Haujui unafiki,aje akulishe sumu,
Anapenda urafiki,hata ukimdhulumu,
Na usipomuafiki,wala hatokulaumu,
Wakati rafiki mwema,atakupa uatakacho.

Atakupa utakacho,wala usimuabudu,
Iwe wazi na kificho,mpole ama bandidu,
Hawezi kupa kisicho,mwema akupe kibudu,
Wakati rafiki mwema,wakati ni kiongozi.

Wakati ni kiongozi,huumbua ufichacho,
Wakati ni kama ngozi,ama mboni ya jicho,
Wakati ni mkombozi,asiyevujisha jasho,
Wakati rafiki mwema,huumbua hufumbua.

Comments

Popular posts from this blog

NOTES ZA USHAIRI

MBINU ZA KUFUNDISHIA

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI