ZANA ZA KUFUNDISHIA
1.
Zana za kufundishia, ni kitu au vitu vyovyote
vinavyojengwa na kutumika katika kuinua kiwango cha elimu. Mwalimu yeyote
anapaswa kujifunza utengenezaji na matumizi ya zana kwani ni nyenzo muhimu sana
katika kazi ya kufundisha na kujifunza. Lengo hasa la kutumia zana katika
kufundisha ni kukuza na kuinua kiwango cha kujifunza cha mwanafunzi. Kikawaida
zana za kufundishia na kujifunzia hupaswa kuwa na sifa kama vile kubebeka,
kuonekana, kuhifadhika, kusadifu mada, iendane na mazingira na iendane na umri wa
wanafunzi. Baadhi ya waandishi wamebainisha aina tano za zana kama vile vitu
halisi, bandia, video na sinema, chati na picha, redio, santuli, tepu rekoda.
Zifuatazo
ni aina kuu tatu za zana za kufundishia
katika ngazi za elimu yaani elimu ya msingi, sekondari, na sekondari ya juu:-
Zana za kuonekana,
hizi ni zana ambazo mwalimu huzitoa katika mazingira halisi ambapo huziandaa
yeye mwenyewe au kuwaagiza wanafunzi waziandae ili kuweza kufanikisha suala
zima la ujifunzaji. Mfano wa zana hizi ni kama vile majani ya miti, mawe, na
nyingine nyingi. Mwalimu huweza kutumia zana kama vile mawe wakati wa
ufundishaji wa hesabu za kujumlisha, kutoa, kuzidisha, na hata kugawanya.
Zana za kusikika,
zana hizi ni zana zinazotoa sauti kama vile redio, kinanda, ngoma. Zana hizi
humsaidia mwalimu katika tathimini ya kujua wanafunzi wenye matatizo ya kusikia
na pia humsaidia mwalimu kufanikisha ufundishaji wake kwa wanafunzi wake hasa
katika mada inayohusiana na usikivu.
Zana za kusikika na kuonekana,
zana hizi ni zana ambazo huweza kutoa sauti na hata kutoa picha. Zana hizi ni
kama vile runinga na tanakilishi. Zana hizi huweza kumsaidia mwalimu katika
ufundishaji wake, ambapo mwalimu huwaongoza wanafunzi kujifunza somo fulani kwa
kutazama picha na kusikiliza sauti itolewayo katika runinga, tanakilishi au
simu. Hivyo zana hizi ni muhimu sana katika suala au mchakato mzima wa
ufundishaji na ujifunzaji kwa sababu haibagui wanafunzi kutokana na hali zao,
mfano wasoona au wasosikia.
Baada
ya kuangalia aina tofauti tofauti za zana, hebu tuangalie faida ya zana za
kufundushia. Zipo faida nyingi za zana za kufundishia lakini hizi hapa chini ni
baadhi tu:-
Hujenga ubunifu,
matumizi ya zana za kufundishia huweza kujenga ubunifu kwa mwanafunzi na pia
hata kwa mwalimu kwani uundaji wa zana huitaji maarifa ya ziada ili
kuikamilisha. Mwanafunzi huweza kuwa mbunifu pindi tu atakapo agizwa na mwalimu
kutengeneza zana, kama vile kufuma kitambaa, kuchora picha na kadharika.
Humjengea mwanafunzi kumbukumbu ya
kudumu, mwanafunzi atakapofundishwa kwa kutumia zana
mbalimbali kama vile tufe kama mfano wa umbo la dunia. Mwanafunzi huweza kuweka
kumbukumbu kwa mda mrefu kwa sababu kujifunza kwa kuona kitu husika humjengea
mwanafunzi uwezo wa kukumbuka tofauti na kujifunza bila kuona kitu husika. Hivyo
utumiaji wa zana katika ujifunzaji ni muhimu sana kwa sababu hufanya somo
kueleweka kwa urahisi.
Hujenga udadisi,
ujifunzaji kwa kutumia zana una faida kwa kuwa hujenga udadisi kwa mwalimu na
mwanafunzi. Hii hutokea pale mwanafunzi anapodadisi kwa undani zaidi namna au
jinsi kitu kilivyoundwa mfano wa zana kama vile redio, runinga na zana zingine.
Hivyo zana zina umuhimu sana katika ujifunzaji na ufundishaji.
Kurahisisha tendo kufundisha na
kujifunza, utumiaji wa zana hurahisisha suala zima la
ujifunzaji na kufundisha. Wanafunzi huelewa zaidi pale wanapoona kitu halisi
hivyo hufanya somo liwe zuri kwa wanafunzi na waweze kulifurahia. Hii humfanya
mwanafunzi aweze kuelewa kwa urahisi zaidi kuliko pale anapojifunza kwa
kufikiri tu pasipo kuona kitu kinachozungumziwa.
Wanafunzi wengi hushiriki,
katika ujifunzaji wa kutumia zana wanafunzi wengi huwepo katika somo kwa
sababu, wanafunzi hupendelea zaidi kujifunza kwa kuona kitu halisia
kinachosemwa na mwalimu wa somo. Mfano wakati wa kufundisha kompyuta, wanafunzi
wengi huudhulia endapo kompyuta itakuepo kama zana ya kufundishia, kwani
wanafunzi wataona kipanya, chombo chenye vibonyezo, kompyuta yenyewe, na kioo
cha kompyuta.
Mwanafunzi hachoki kujifunza,
katika ujifunzaji wa kutumia zana mwanafunzi hachoki kujifunza kwani hushiriki
papo hapo katika suala zima la ujifunzaji. Mwanafunzi hutamani mwalimu aendelee
kufundisha, kwa kuwa vitu vinavyofundisha ni vitu ambavyo mwanfunzi huviona kwa
macho yake mfano kuwaonesha wanafunzi filamu ya riwaya ya mfadhili. Hivyo mwanafunzi hachoki kujifunza.
Kuna
mambo mbalimbali ya kuzingatia wakati wa kuandaa zana za kufundishia, mambo
hayo ni kama vile ukubwa wa zana, idadi ya wanafunzi, maudhui yaendane na zana,
uwezo wa mwalimu katika kuelezea mada.
Kuna
namna tofauti tofauti za kuandaa zana za kufindishia lakini zifuatazo ni baadhi
tu ya namna ya kuandaa zana za kufundishia nazo ni:-
Kuchonga,
hii ni ile namna ya kuandaa zana kwa kutumia miti kama malighafi. Mwalimu
hutumia miti kama malighafi ya kuchongea zana kama vile kinyago, kuchonga rula,
na vifaa vingine vinavyotokana na malighafi miti. Zana za kuchonga hupelekea
mwanafunzi kuwa mdadisi katika kuandaa zana hizo, kwa kuwa hutumia maarifa
mengi katika uandaaji wake.
Kuchora,
namna hii ya kuandaa zana za kufundishia, ni namna inayohusisha matumizi ya
kalamu ya mkaa, rangi za aina mbalimbali, manila, na vifaa vingine. Hapa
mwalimu huweza kuandaa zana kama vile ramani, picha ya baadhi ya wanyama,
alfabeti, namba, maumbo mbalimbali kama vile pembe tatu, mstatili, mraba na
maumbo mengine mengi.
Kufinyanga,
hii ni namna ya uandaaji wa zana kwa kutumia udongo kama malighafi ya
kutengenezea zana za kufundishia. Mwalimu huchanganya udongo na maji ili kuweza
kutengeneza zana kama vile vyungu, sahani, kinyago na kadharika. Mwalimu
anaweza kuwashirikisha wanafunzi katika utengenezaji wa zana hizi ili
kufanikisha somo la stadi za kazi.
Kukusanya,
hii ni namna ya kuandaa zana kwa kutafuta vifaa vya kujifunzia na kifundishia
yaani zana kwa kuzikusanya kutoka katika mazingira halisi. Tendo hili laweza
kutendeka kwa kuwaagiza wanafunzi au mwalimu mwenyewe kuziokota, kununua au
kuchukua kutoka nyumbani kwake. Zana hizo kama machungwa, vijiko, na hata
redio. Zana hizi humsaidia mwalimu katika kufanikisha suala zima la ufundishaji
kwa wanafunzi wake.
Kufaragua,
hii ni namna ya kuandaa zana kwa kutumia vifaa au makunzi yasio halisi na
yanayopatikana katika mazingira husika. Ufaraguzi unaweza kluwa wa namna
mbalimbali kama vile kutumia kitu papo kwa papo kinyume na matumizi yake ya
kawaida, unapotumia kalamu ya mkaa kama kishikizi katika kupiga mstari (hapa
utakua umetumia kalamu ya mkaa kama rula). Au kutumia mpira kama tufe katika
kufundisha kuwa dunia ni duara.
Kufuma,
hii ni namna ya kuandaa zana kwa kutumia nyuzi za rangi mbalimbali kutengeneza
zana kama vile vitambaa, sweta pamoja na zana zingine zinazotokana na malighafi
nyuzi. Mwalimu huweza kuwaagiza wanafunzi walete nyuzi ili kuweza kuziandaa
zana hizo katika mazingira ya shule ili aweze kutambua wanafunzi waliomuelewa
wakati anafundisha darasani. Hii ni nzuri kuliko mwalimu akiwaagiza wanafunzi
wake watengenezee nyumbani.
Kwa
ujumla, katika mchakato wa ufundishaji
na ujifunzaji zana sio lazima vitu au vifaa, kwa sababu kila kitu
kinachoshikika endapo kitakuwa na mchango wowote katika kufanikisha suala zima
la ufundishaji na ujifunzaji kitu hicho kitakua ni zana. Hivyo mwalimu na
wanafunzi pia huweza kuwa zana pindi wawapo darasani kwa ajili ya somo
mahususi.
Fantastic!
ReplyDeleteSomo lipo vizuri
ReplyDeleteNi somo zuri sana tna linaegemea kwenye ufundiahaji wa kiswahili kwa wageni.... Heko
ReplyDeleteAisee nukuuu hizi ziko vizuri sana katika suala la ufundishaji na ujifunzaji kwa mwanafunzi,zitakazo wezesha tendo la urithishaji wa maarifa,ujuzi,stadi,mitazamo,mienendo na mielekeo toka kizazi hadi kizazi.
ReplyDeletebig up sana,