Skip to main content

DHANA YA THIETA ZA KIJADI

Kwa mujibu wa kamusi ya fasihi istilahi na nadharia (2003) Thieta ni dhana inayotumiwa kurejerea masuala yanayohusisha uandishi na uigizaji wa sanaa za maonyesho. Dhana hii ina upana mkubwa kuliko neno sanaa ingawa mara kwa mara hutumika kama visawe.
Mulokozi (2009) anasema thieta ni maigizo yanayotumia watendaji kuiga tabia na matendo ya watu au viumbe wengine ili kuburudisha na kutoa ujumbe fulani. Ni sanaa inayopatikana katika makabila mengi ya Tanzania.
Udhaifu wa maana(fasiri) hii ni pale inaporejelea thieta kama uigaji wa tabia na matendo ya watu na viumbe, ambapo si kweli kwamba huiga tu matendo ya watu, mfano katika majigambo tunaona mtu anaigiza matendo yake mwenyewe na siyo matendo wala tabia za mtu au viumbe fulani.
Thieta simulizi ni utanzu unaowasilishwa kwa masimulizi ya mdomo sambamba na uigizaji wa matendo (ambayo huweza kuwa ya mtu mwenyewe au mtu mwingine au viumbe vingine) na huifadhiwa kichwani, lakini kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia utanzu huu umepokea mabadiliko na kuanza kuhifadhi katika maandishi, kanda za kurekodia na vinasa sauti. Lakini itaendelea kuwa thieta simulizi katika uwasilishaji wake.
Kuna nadharia mbalimbali zinazoelezea chimbuko la thieta simulizi, kama vile chimbuko la thieta na maigizo ni mungu dhana hii inaugwa mkono na wataalam kama J. Ramadhani, wanaamini kuwa thieta zimetokana na uigizaji wa matendo na shughuli mbalimbali za kidini zilizokuwa zikifanyika katika jamii za Wagiriki na Wayunani (mungu wa Wagiriki aliyeitwa Dioniz). Katika ibada hizo kilikuwepo kitu kilichojulikana kama “Dikrambo” ambapo yaliigizwa matendo ya kimungu.
Udhaifu wa nadharia hii; ni pale wanapoamini thieta simulizi imetokana na uigizaji wa matendo ya mungu wa Kigiriki jambo ambalo si kweli kwani hata jamii za Afrika zilikuwa na ibada mbalimbali za kimiungu.
Nadharia inayodai kuwa thieta simulizi imeibuka kutokana na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi yanayo aminiwa kama chanzo cha thieta simulizi; mfano jando na unyago, michezo ya watoto, ngoma na shughuli zingine za kijamii na kiuchumi.

Si rahisi kutaja na kubainisha vipera vya thieta simulizi kutokana na ukweli kwamba watalamu wenyewe wametofautiana katika kuainisha vipera hivyo. Mulokozi (2009) anaainisha vipera vinne ambavyo ni kama a) Maigizo ya watoto, b) Maigizo ya kidini, c) Maigizo ya kidini na d) Maigizo ya misibani. Mwando na Balisidya (1976) anaainisha vipera vya thieta simulizi kama vile Ngoma, masimulizi ya hadithi, sherehe, majigambo na kusalia miungu (matambiko).
Kutokana na maelezo hayo hapo juu tunaweza kubainisha vipera vya thieta simulizi kama ifuatavyo;
Sherehe kama kipera cha thieta simulizi; kinahusiana na kuingizwa kwa wanajamii kwenye kundi la watu fulani kutoka kundi la watu wa aina nyingine. Mfano kutoka katika kundi la watoto kwenda kundi la watu wazima, kutawazwa uchifu mtu kutoka kwenye kundi la kawaida kuingia kundi la watawala, au mtu kutoka kwenye kundi la askari wa kawaida kuingia kwenye kundi la askari shujaa, au mtu kutoka katika kundi la watu kuingia kwenye kundi la mizimu. Mfano jando na unyago, katika shughuli ya unyago tunaweza kuigawa katika hatua tatu, hatua ya kwanza ni ya kiishara, hatua ya pili ni ya vitendo na hatua ya tatu ni ya kiishara.
Ishara ya hatua ya kwanza inakuwa na utekelezaji wa maandalizi ya kimwili mfano tohara katika kabila la wakurya, hatua ya pili ambayo ni ya vitendo hutumia ngoma katika jamii nyingi za pwani ya Tanzania ambapo mabinti huchezwa ngoma ya kumtoa mwali. Mfano ngoma ya wakaguru inayotumika kumtoa mwali hujulikana kwa jina la “mbete” vilevile hatua ya tatu ni ya kiishara hufanyika baada ya hatua ya pili yaweza kufanyika kwa kumpa au kumvisha mwali nguo mpya, au kumpa jina fulani au kukabidhi kwenye kundi fulani. Mambo yanayotendeka katika sherehe yana dhana ya thieta kwani mambo yote yanayotendeka ni mambo yanayoigizwa kutoka ndani ya jamii.
Masimulizi ya hadithi; hiki kama kipera cha thieta simulizi hujikita katika mchezo fulani unaofanywa na fanani mbele ya hadhira. Mfano hadithi ya sungura na simba fanani atayaweka matendo ya wahusika hawa kisanaa zaidi na kuyaigiza jukwaani (uwanjani) fanani ataambaambaa na kusafiri ili kuweza kukamilisha simulizi na matendo hayo ya wahusika sambamba na kuishirikisha hadhira pale inapohitajika. Mfano katika jamii ya wakaguru fanani anaposimulia hadhira huitikia kwa kusema “Diii” kila baada ya sentensi ya usimulizi. Pia hadhira huweza kushiriki kwa kuimba wimbo. Katika jamii nyingi za kitanzania masimulizi hufanyika katika wakati maalum, jioni baada ya kazi. Dhana ya thieta hujitokeza kwa fanani kuigiza matendo katika  uwasilishaji wake.
Kusalia miungu (matambiko); Mulokozi huita utanzu huu kama maigizo ya kidini, kama utanzu wa thieta simulizi lengo kuu la matambiko kuelekeza matatizo ambayo binadamu ameshindwa kuyatatua kwa nguvu za kawaida. Mfano tatizo la ukame, kuvamiwa na kushambuliwa na magonjwa. Dhana ya thieta katika matambiko inajitokeza pale wahusika wanapoiga matendo yasiyo ya kwao. Mfano katika jamii ya wakaguru linapotokea tatizo la ukame watu huelekea kwa mganga na kuelezwa lazima waende kumuomba mungu wa mvua (kijumba mulungu), watu hulazimika kwenda sehemu maalum na kujenga kijumba cha msonge ndani huwekwa kitanda, kiko na tumbaku. Baada ya hapo huteuliwa watu wawili mwanamke na mwanaume (mwanaume mungu na mwanamke mke wa mungu) ndani ya kijumba hicho hufanya tambiko kisha kutoka kwa wimbo kutoka katika jamii hii ya wakaguru;
Mfano. Mzee: Chigheni ifula (tupe mvua).
             Watani: Mkagone (mlale).
Wanajamii wengine huwapokea na kufuatana nao mpaka kwa mkuu wa ukoo, kabila au nchi. Huko hucheza na kunywa pombe kumfurahisha mungu wao awaletee mvua.
Maigizo ya misibani kama kipera cha thieta simulizi; katika makabila watani na wajukuu wa marehemu hupaswa kufanya maigizo ya matendo ya marehemu. Maigizo haya kama mchezo wa kuigiza husidia kupunguza huzuni za wafiwa na kutoa mafunzo fulani kwa watu waliopo msibani. Mfano katika jamii ya wakurya na waruuli vitukuu (wajukuu wa pili) wa marehemu hupaswa kuigiza katika msiba wa babu au bibi yao.
Ngoma pia kama kipera cha thieta simulizi; ngoma inayogusiwa hapa si ile ya ngoma kama kifaa cha mziki bali hurejelea matendo ya uchezeshaji wa viungo vya mwili na miondoko maalumu. Ngoma huweza kuwa katika sherehe, harusi, jando na unyago. Huchukuliwa kama kipera cha thieta simulizi na huchezwa wakati wowote, ngoma moja huweza kutokea katika harusi na hiyo hiyo ikachezwa katika jando na unyago. Itachezwa kwenye unyago ikiwa na lengo la kuburudisha, kuonya na kukosoa watu. Mfano wa ngoma hizo ni kama mpendoo, mfunyundo (wagogo) na silanga (wapogoro). Ngoma licha ya kuburudisha huwa pia na mafunzo fulani mafano ngoma ya wakaguru “mfunya” huwaasa wasichana kuacha tabia mbaya. Dhana ya thieta hujitokeza pale ambapo kunakuwa na ugizaji wa uchezeshaji wa viungo vya mwili kwa wachezaji na pale watazamaji wanapojiunga kucheza au hutazama ngoma hiyo.
Majigambo pia kama kipera cha thieta simulizi; ni ujigambaji wa watu kuhusu mambo fulani ya kishujaa aliyopata kuyatenda maishani mwake. Majigambo haya husimuliwa katika lugha ya kishairi na masimulizi yake huambatana na vitendo vya mgambaji mwenyewe. Majigambo hupatikana katika jamii nyingi na hutofautiana kati ya jamii moja na nyingine. Majigambo huweza kufanyika katika sherehe mbele ya mtemi, katika ngoma na pombe ili kudumisha hali ya kiushujaa. Mgambaji huwa na dhana mbalimbali za kutendea (miega) na mavazi maalumu. Mfano fanani akiwa anagamba kuhusu vita fulani aliyopigana atafanya uigizaji wa matendo mbalimbali aliyoyatenda huko vitani. Dhana ya thieta simulizi hudhihirika pale mgambaji anapogamba na kuonyesha jinsi alivyomshinda adui.
Tondozi aina ya majigambo ambapo mgambaji hujigamba juu ya matendo mbalimbali yaliyowahi  kutendwa na mtu mwingine katika jamii.
Michezo (maigizo) ya watoto; mchezo huu unakuwa na matendo yanayochezwa na watoto huiga matendo mbalimbali ya kinyumba na kijamii, pia huigiza matendo kama vile kilimo, kufanya biashara n.k. Katika uigizaji huu waigizaji hupeana majukumu kama vile uwepo wa baba na mama, na watoto. Mfano baba na mama.
A. Baba anenda shambani.
B. Mama anapika chakula.
C. Mtoto wa kiume anaenda kuchunga.
D. Mtoto wa kike, anaigiza akifanya kazi kama vile kuosha vyombo na kumsaidia mama kulea mtoto.
Katika mchezo huo hapo juu mchezo huishia kwa wote kukutana kula chakula na kuingia kulala.


Thieta simulizi imepitia vipindi mbalimbali kihistoria kama vile kipindi kabla ya ukoloni, thieta simulizi kipindi cha ukoloni, thieta simulizi kipindi cha baada ya uhuru na thieta kipindi cha utandawazi.
KIPINDI KABLA YA UKOLONI (UJIMA).
Thieta andishi hazikuwepo badala yake zilikuwepo thieta zilizo zengwa au faraguzwa uwanjani mbele ya hadhira katika shughuli maalumu kama vile tambiko, jando na unyago, michezo ya watoto, pia thieta simulizi za kipindi hiki zilikuwa hazina ploti ya kiaristotle.
                                                         Kilele.
                                                             B

                                             
                                          A                                    C
                                 Mwanzo.                          Suluhisho (mshuko).
Katika kielezo hicho hapo juu ndiyo dhana ya ploti ya kiaristotle, ambapo mgogoro unaanzia katika          A unakuwa zaidi mpaka kufika kileleni B na C mgogoro unashuka na kupatiwa suluhisho.
THIETA SIMULIZI KIPINDI CHA UKOLONI.
Wakoloni waliingia bara la Afrika miaka ya (1890–1960). Wakoloni walikusudia kuitawala Afrika kisiasa, kiuchumi na hata kiutamaduni. Kipindi hiki cha ukoloni kimegawanyika katika makundi mawili.
a. Thieta simulizi kipindi cha utawala Wajerumani (1890–1919) walipofika Afrika Wajerumani waliziona tamaduni za Kiafrika zilikuwa za kishenzi hivyo hazikupaswa kutiliwa maanani na kuziendeleza. Thieta simulizi pia ilififia kwa kiasi kikubwa kipindi hiki kutokana na mtazamo wa wazungu kuwa mambo yote waliyoyakuta Afrika yalikuwa ni ya kishenzi.

b. Thieta simulizi kipindi cha Ukoloni wa Mwingereza Tanzania (1919-1960), Mwingereza alitawala sehemu kubwa ya dunia baada ya vita ya kwanza ya Dunia (1914-1918) na Tanganyika ikiwa ni miongoni. Kipindi hiki kilishuhudia mabadiliko makubwa katika thieta simulizi kama vile;
i. Kuibuka kwa thieta za Kizungu; thieta hizi ziliingizwa na utawala wa kikoloni kwa lengo la kuwaburudisha masetla na maofisa wa kizungu na ziliigizwa katika kundi maalumu. Pia zilienda sambamba na ufundishaji wa biblia na imani ya kikristo. Nchini Kenya zilikuwa katika lugha ya kizungu na ziligezwa sana sehemu za Nairobi na Mombasa.
Pia baadhi ya thieta hizo zilianza kufundishwa mashuleni, mfano “shekespeare” na baadhi zilikuwa za kidini. Kipindi hiki pia vilianzishwa vikundi vikundi vya kuigiza thieta za Kizungu, mfano kwa Tanzania vilianzishwa vikundi viwili ambavyo ni Dar es salaam Player (baadaye little theatre) 1947, na Arusha little theatre 1953. Mwaka 1957 baraza la Kiingereza (British council) lilianzisha mashindano ya thieta za Kiingereza nchini Tanzania iliyojulikana kama “school competition”.
ii. Thieta za vichekesho pia zilishamiri sana kipindi hiki; zilianza miaka ya 1920 na zilitungwa papo kwa papo bila kuandikwa kwa lengo la kuwachekesha Waafrika, thieta hizi zililenga kumsuta Mwafrika alionekana mshamba. Mfano mtu kutoka shamba kwenda kuzuzukia mjini.
iii. Kipindi hiki pia kilikuwa na thieta andishi zilizoandikwa kwanza kabla ya kuigizwa jukwaani (uwanjani), 1944-1950 Graham Hyslop Mwingereza aliyekuwa nchini Kenya alianzisha thieta hizi kwa lengo la kuwaburudisha maaskari wake, mfano “Afadhali mchawi” 1957 na “Mgeni karibu” 1957. Baadaye alianza kuzunguka mashuleni na vyuoni nchini Kenya akifundisha muziki na uigizaji. Miongoni mwa wanafunzi wake waliokuja kuibuka hapo baadaye ni Henry Kuria aliyetunga thieta ya “Nakupenda lakini” na Gerishoni Ngugi aliyetunga thieta ya “Nimelogwa nisiwe na mpenzi”.
THIETA SIMULIZI KIPINDI CHA UHURU MIAKA 1960
Baada ya kupata uhuru viongozi wengi wa Afrika walienda mbali zaidi ya uhuru wa kisiasa na kiuchumi wakilenga kurudisha na kuboresha thieta za Afrika zilizofifia kipindi cha Ukoloni, mfano jando na unyago, michezo ya watoto, sherehe na nyingine nyingi.
Thieta za vichekesho ziliendelea kuwepo lakini ziligeuzwa na kuanza kuwasuta Wazungu weusi waliokua wakiringia vyeo na elimu zao na kupuuza tamaduni zao.
Pia kipindi hiki thieta andishi zilizoanzishwa wakati wa ukoloni ziliendelea kuwepo lakini zilibadilishwa na kuanza kuwazungumzia mashujaa wa kiafrika waliopambana na utawala wa kikoloni. Mfano Mkwawa wa wahehe na Kinjekitile Ngwale wa wamatumbi.
THIETA SIMULIZI KIPINDI CHA UTANDAWAZI.
Kipindi hiki kilianza miaka ya 1980 hadi leo. Katika kipindi hiki dunia ilifanywa kuwa kijiji kimoja, mawasiliano yaliboreshwa hivyo watu walingia katika kujifunza starabu mbalimbali za duniani. Matumizi ya sayansi na teknolojia yaliboresha zaidi uhifadhi wa thieta hizo simulizi, hivyo thieta simulizi ilianza kuhifadhiwa katika maandishi, kurekodiwa kwenye kanda za sauti na kuanza kuchezwa kwenye televisheni na redio. Thieta iliboreshwa zaidi na kuanza kurekodiwa kwenye sidii (CD) za kuona VCD na DVD. Kutokana na kuhifadhiwa katika kanda za kuona utanzu thieta au maigizo ulibadilishwa jina na kuitwa FILAMU. Maudhui yake pia ilibadilika na kuanza kuzungumzia maswala ya mapenzi na kutumia majina ya kimagharibi.
Utanzu huu pia ulibadilishwa kutoka kuwa mali ya jamii kama ilivyokuwa awali na kuwa mali ya mtu binafsi, kuigizwa kwa lengo la kupata fedha (kipato) na kutafuta umaarufu. Kipindi hiki utanzu huu ulienda mbali zaidi kwani viliibuka vikundi maalumu kwaajili ya kusambaza kazi hizi. Thieta andishi ya Kiswahili pia ziliendelea kuwepo licha ya maudhui yake kubadilishwa na kuanza kuzungumzia ukatili  wa wanawake na kijinsia, mfano Nguzo Mama ya Muhando, P. na Kwenye Ukingo Wa thim ya Hussein, I.
Ni vigumu kuainisha na kubainisha vipera vya thieta simulizi kutokana na ukweli kwamba wataalam wenyewe wanatofautiana katika aina na idadi, tanzu za fasihi simulizi huingiliana, tanzu za fasihi simulizi hubadilika kulingana na wakati sambamba na kutofautiana kutoka jamii moja na nyingine.



MAREJEO.
Muhando, P. na Balisidya, N. (1976) Fasihi na Sanaa za maonyesho. Dar es Salaam:
                                                         Tanzania Publisher Houser (TPH).
Mulokozi, M.M. (2009) Utangulizi wa Fasihi ya Kiswahili. Dar es Salaam: KAUTTU.
Wamitila, K.W. (2003) Kamusi ya Fasihi Istilahi na Nadharia.Nairobi. Focus Publications Ltd.
Wamitila, K.W. (2010) Kanzi ya fasihi 01: Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi:
                                     Vide-Muwa Publisher Ltd.

Comments

Post a Comment

Popular posts from this blog

NOTES ZA USHAIRI

USHAIRI     NI    NINI ? Shaaban Robert katika uandishi wa ushairi ameandika Tenzi na mashairi ya kimapokeo. Tenzi : Ni aina ya mashairi ya kimapokeo wenye sifa zifuatazo: Kimaudhui ; Ni utungo wenye maudhui yanayosimulia kwa urefu tukio fulani maalum. Waweza kuwa wasifu wa mtu au jambo la kihistoria. Mfano; S. Robert ameandika utenzi wa vita vya Uhuru, ameeleza kuhusu historia. Pia katika Mapenzi Bora, ameeleza kuhusu sifa za mapenzi bora. Utenzi ni utungo wa pili kati tungo za ushairi zenye beti nyingi. Utungo wa kwanza unaoongoza kuwa na beti nyingi kuliko zote katika ushairi ni Tendi. Lakini hapa tutaangazia tenzi zaidi. Utenzi hauna mizani nyingi aghalabu mizani nane, hauna mshororo bali una nusu mshororo/kipande mstari. Vilevile katika utenzi kipande mstari hakigawiki. Pia katika kipande mshororo kuna vipande vinne kwa kila ubeti. Mistari mitatu ya kwanza huwa na vina vyenye urari na kipande mstari cha mwisho/cha nne huwa...

KISWAHILI FORM 1: FASIHI SIMULIZI

KISWAHILI Form 1 Topic 4 FASIHI SIMULIZI Fasihi simulizi ni moja kati ya tanzu za fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Katika mada hii utajifunza na kisha utaweza kubainisha tanzu na vipera vya fasihi simulizi pamoja na ufafanuzi wake. Na pia utaweza kutofautisha kati ya kipera na kipera au kati ya utanzu na utanzu. Ubainishaji wa Tanzu za Fasihi Simulizi Tanzu za Fasihi Simulizi Bainisha tanzu za fasihi simulizi Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. Tanzu za Fasihi Simulizi ni pamoja na hizi zifuatazo: Masimulizi/hadithi Semi Ushairi Mazungumzo Maigizo Ngomezi Ufafanuzi wa Vipera vya Tanzu za Fasihi Simulizi Vipera vya Hadithi Fafanua vipera vya hadithi SIMULIZI/ HADITHI Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulan...

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI

Ushairi kama moja kati ya tanzu za fasihi inayowasilishwa katika namna zote aidha kwa lugha ya maandishi au kwa lugha ya masimulizi una mchango au nafasi kubwa sana katika kunufaisha au kustawisha maisha ya binadamu kwa kumuelimisha, kumsisimua, kutunza na kuhifadhi amali zake pamoja na kukuza na kuendeleza lugha yake kama moja kati ya vipengere muhimu maishani mwake. Ushairi kama nudhumu katika fasihi simulizi hujumuisha nyimbo, ngonjera, tenzi na mashairi yenyewe. Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au katika kumbo mbalimbli kama asemavyo Mulokozi (1996) kuwa zipo kumbo kuu tatu ambazo ni ushairi wa kijadi au kimapokeo, ushairi wa mlegezo au huru na ushairi wa maigizo. Wanazuoni wafuatao wa mashairi ya kimapokeo wametoa maana za ushairi kama ifuatavyo:- Shaaban Robert (1958:37). “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari…, mawazo, maoni na fikra za ndani zi...