Skip to main content

KISWAHILI FORM 1: USIMULIZI

KISWAHILI Form 1 Topic 5

USIMULIZI
Usimulizi ni jumla ya maelezo yanayotolewa na mtu au watu wengi kuhusu tukio fulani. Katika mada hii utajifunza juu ya taratibu za usimulizi wa matukio kupitia njia kuu mbili za masimulizi, yaani kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi. Pia utaweza kujifunza juu ya mbinu mbalimbali za usimulizi.
Njia za Usimulizi wa Hadithi
Elezea njia za usimulizi wa hadithi
Usimulizi hufanyika kwa njia kuu mbili yaani kwa njia ya maandishi na kwa njia ya masimulizi ya mdomo. Kila njia hutegemea namna msimuliaji anavyoweza kuwasiliana na msikilizaji. Ikiwa msimuliaji na msikilizaji hawakukaribiana, njia ambayo itatumika ni ile ya maandishi. Kwa mfano kama utahitaji kumweleza mtu aliyembali kuhusu tukio fulani la kusisimua utalazimika kutumia maandishi, yaani utatumia njia ya kumwandikia barua.
Lakini kama unamsimulia mtu ambaye yupo karibu nawe, utatumia njia ya mazungumzo ya ana kwa ana.

Taratibu za Usimulizi wa Matukio
Fafanua taratibu za usimulizi wa matukio
Usimulizi wa matukio dhamira yake ni kumweleza mtu au watu tukio ambalo wao hawakulishuhudia. Hivyo katika usimulizi msimuliaji hutakiwa kutoa maelezo muhimu ambayo yatawawezesha watu hao kulielewa tukio linalosimuliwa sawasawa na huyo anayeshuhudia.
Mambo muhimu ya kutaja katika usimulizi wa matukio ni pamoja na haya yafuatayo:
  1. Aina ya tukio – msimuliaji atatakiwa kubainisha katika maelezo yake aina ya tukio. Kwa mfano, kama ni harusi, ubatizo, ajali ya barabarani au mkutano.
  2. Mahali pa tukio – ili msimuliaji aweze kuielewa habari inayosimuliwa, ni lazima kumwelewesha ni mahali gani tukio hilo limetokea. Kwa mfano, kama ni mjini inafaa kutaja hata jina la mtaa.
  3. Wakati – katika usimulizi ni muhimu pia kutaja muda ambao tukio limetendeka kama ni asubuhi, mchana au jioni bila kusahau kutaja muda halisi yaani ilikuwa saa ngapi.
  4. Wahusika wa tukio – ni muhimu kutaja tukio limehusisha watu gani, wingi wao, jinsia yao, umri wao n.k.
  5. Chanzo cha tukio – kila tukio lina chanzo chake hivyo ni muhimu kutajwa katika usimulizi.
  6. Athari za tukio – athari za tukio nazo ni sharti zibainishwe. Kama ni ajali, je watu wangapi wameumia; wangapi wamepoteza maisha n.k.
  7. Hatima ya tukio – msimuliaji katika usimulizi wake ni lazima abainishe baada ya tukio kutokea na kushughulikiwa hatima yake ilikuwaje. Kwa mfano, kama tukio ni ajali ya barabarani hatima yake inaweza kuwa majeruhi kupelekwa hospitalini na dereva aliyehusika kukamatwa.
Kwa hiyo misingi hii ya usimulizi hufanya usimulizi wa tukio kuwa na sehemu kuu tatu:
  • Utangulizi – sehemu hii huwa na maelezo tu ya utangulizi ambayo hulenga kuvuta hisia na umakini wa msikilizaji au wasikilizaji. Kwa kawaida utangulizi wa tukio huwa ni maneno machache kiasi yasiyozidi aya moja.
  • Kiini – kiini cha usimulizi huelezea tukio halisi kuanzia chanzo chake, wahusika, muda, mahali na athari za tukio.
  • Mwisho – mwisho wa usimulizi ni matokeo yanayoonyesha matokeo ya mwisho ya tukio linalohusika, wakati mwingine matukio haya yanaweza kuambatana na maelezo ya msimuliaji kuhusu mtazamo au maoni yake binafsi juu ya tukio ambalo amesimulia.
Mbinu za usimulizi
Ili habari inayosimuliwa ipate kueleweka vizuri, sharti msimuliaji ajue mbinu za kusimulia katika hali inayovuta hisia za msikilizaji wake.
Baadhi ya mbinu hizo ni uigizi, utumizi wa lugha fasaha inayozingatia lafudhi sahihi ya Kiswahili.
Kwa upande wa uigizi msimuliaji atatakiwa kuigiza mambo muhimu yanayohusiana na tukio ambalo anasimulia. Nayo ni kama vile milio, sauti na matendo.
Kwa upande wa usimulizi ambao unafanyika kwa njia ya maandishi, sharti usimulizi huo uwe na kichwa cha habari. Kichwa cha habari kinatakiwa kuandikwa kwa maneno yasiyozidi matano, yaliyoandikwa kwa herufi kubwa.
Kwa vile usimulizi wa tukio huwa unahusu tukio lililopita, maelezo yake mengi huwa katika wakati uliopita.

Comments

Popular posts from this blog

KISWAHILI FORM 1: FASIHI SIMULIZI

KISWAHILI Form 1 Topic 4 FASIHI SIMULIZI Fasihi simulizi ni moja kati ya tanzu za fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Katika mada hii utajifunza na kisha utaweza kubainisha tanzu na vipera vya fasihi simulizi pamoja na ufafanuzi wake. Na pia utaweza kutofautisha kati ya kipera na kipera au kati ya utanzu na utanzu. Ubainishaji wa Tanzu za Fasihi Simulizi Tanzu za Fasihi Simulizi Bainisha tanzu za fasihi simulizi Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. Tanzu za Fasihi Simulizi ni pamoja na hizi zifuatazo: Masimulizi/hadithi Semi Ushairi Mazungumzo Maigizo Ngomezi Ufafanuzi wa Vipera vya Tanzu za Fasihi Simulizi Vipera vya Hadithi Fafanua vipera vya hadithi SIMULIZI/ HADITHI Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulan...

MBINU ZA KUFUNDISHIA

Mbinu za kufundishia , ni miongozo mbalimbali atumiayo mwalimu wakati wa kufundisha somo aliloliandaa kwa wanafunzi wake. Walimu wanapaswa kuamua kwa kuchagua kwa makini njia na mbinu bora za kufundishia ili wanafunzi wake waweze kujifunza kwa ufanisi. Ziko njia nyingi za kutengeneza mazingira ya mtoto aweze kujifunza na pia ziko mbinu nyingi za kufundishia. Pamoja na wingi huo tunaweza kuzigawa katika makundi makuu mawili kadri ya jinsi zinavyowashirikisha watoto katika tendo la kujifunza, ambazo tunaweza kuziita shirikishi na zisizo shirikishi . Zifuatazo ni baadhi ya mbinu shirikishi na zisizo shirikishi za kufundishia pamoja na faida na hasara zake:- Njia ya majadiliano , njia hii imekuwa ikitumika katika ufundishaji kwa muda mrefu. Katika kujadiliana mwanafunzi mmoja mmoja hupata nafasi ya mawazo aliyonayo kuhusu suala linalojadiliwa na yeye pia huweza kupata mawazo yaw engine. Katika majadiliano mwanafunzi hupata ujuzi mpya nje na ule aliokuwa nao kabla hajashiriki kat...

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI

Ushairi kama moja kati ya tanzu za fasihi inayowasilishwa katika namna zote aidha kwa lugha ya maandishi au kwa lugha ya masimulizi una mchango au nafasi kubwa sana katika kunufaisha au kustawisha maisha ya binadamu kwa kumuelimisha, kumsisimua, kutunza na kuhifadhi amali zake pamoja na kukuza na kuendeleza lugha yake kama moja kati ya vipengere muhimu maishani mwake. Ushairi kama nudhumu katika fasihi simulizi hujumuisha nyimbo, ngonjera, tenzi na mashairi yenyewe. Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au katika kumbo mbalimbli kama asemavyo Mulokozi (1996) kuwa zipo kumbo kuu tatu ambazo ni ushairi wa kijadi au kimapokeo, ushairi wa mlegezo au huru na ushairi wa maigizo. Wanazuoni wafuatao wa mashairi ya kimapokeo wametoa maana za ushairi kama ifuatavyo:- Shaaban Robert (1958:37). “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari…, mawazo, maoni na fikra za ndani zi...