Skip to main content

KISWAHILI FORM 4: KUTUNGA KAZI ZA FASIHI ANDISHI

KISWAHILI Form 4 Topic 4

KUTUNGA KAZI ZA FASIHI ANDISHI
Mambo ya Kuzingatia katika Utungaji wa Mashairi
Fafanua mambo ya kuzingatia katika utungaji wa mashairi
Utungaji/uandishi wa kubuni ni ule unatokana na hisia ambazo zinamsukuma mtunzi ili atunge kazi yake. Hisia zinaungana na wazo ambapo vitu hivyo vinamsumbua akilini na kumkosesha raha. Mwandishi wa kubuni anataka aliwasilishe wazo lake ili hadhira ifahamu kilichopo moyoni mwake. Mwandishi hukosa usingizi na hivyo hulazimika kuamka na kuandika kile kinachomsukuma akilini mwake.
Uandishi wa kubuni unamtaka mtunzi atumie milango yake ya fahamu kinagaubaga. Kuna milango ya fahamu mitano ambayo ni pamoja na: kuona, kunusa, kusikia, kuhisi, na kuonja.
  • Kuona: je, mhusika unayemfikiria kichwani mwako unamwonaje? Umbo lake ni la kuvutia au kuchusha? Je, macho yake yakoje – je ni ya golori au la? Ni makubwa au madogo? Je, ni mlemavu wa macho?
  • Kunusa: pua zako zinakufanya usikie harufu gani? Je, ni harufu mbaya au nzuri? Je, ni uvundo au marashi? Je, mhusika wako ananuka kikwapa au uturi? Je, ananuka mdomo?
  • Kuhisi: je, unapokaa karibu naye unajihisi nini? Je, unapata mhemko wowote au huhisi chochote? Je, akikupapasa mwilini mwako unajisikia nini? Akikugusa bega unajisikia nini?
  • Kuonja: je, ukiweka kitu hicho mdomoni unaonjaje – ni chungu au tamu? Je, ina pilipili au masala? Je, kuna chumvi au sukari? Je, kitu hicho kina ukakasi au uchachu?
  • Kusikia: je, sauti unayoisikia ikoje? Inamtoa nyoka pangoni? Inakufanya ukose usingizi? Je, ni sauti nzuri au mbaya? Ni nyororo au nzito? Kama ni sauti ya muziki – je, iko chini au juu (kelele)?
Uzoefu wa Mwandishi
Uzoefu ni hali ya kukaa au kujishughulisha na jambo au kitu kwa muda mrefu.
Mwandishi ana uzoefu (uzoevu) wa kukabiliana na maisha kwa kiasi gani? Je, ni matatizo gani ambayo umekutana nayo katika maisha yako? Je, ni mafanikio gani umekutana nayo katika maisha yako? Kwa mfano, katika ajali ya MV Spice (2011) kuna baadhi ya watu waliokolewa na magodoro ya Tanzania? Magodoro haya yana nailoni na je kama yasingekuwa na nailoni? Uzoevu/uzoefu wako ukoje?
Uchunguzi/utafiti
Uchunguzi unapaswa ufanywe na mwandishi ili aweze kuandika jambo au tukio bila kuongopa. Kwa kufanya udanganyifu, mwandishi atapoteza imani yake kwa wasomaji wa kazi zake.
Uchunguzi ili ufahamu au ujue mtu, mnyama, mdudu na kadhalika – anatembeaje, anakulaje, analalaje, anaishije, anachekaje, analiaje, anazaaje, anahusianaje na wenzane na mazingira yake? Haya ni maswali muhimu katika kumwezesha mtunzi kufanya utafiti wa kina ili ajue kitu anachotaka kukiandika akiandikaje na akiwasilishaje ili aweze kuikamata hadhira yake.
Mwandshi baada ya kuzingatia mambo haya sasa anaweza kuanza kutunga kazi yake. Hapa sisi tutajikita zaidi katika utunzi wa mashairi. Kabala hatujaenda katika hatua ya utunzi ni muhimu kujua dhana ya shairi kwa ujumla wake, na baada ya hapo tutakuwa tumekwisha pata maarifa yakutosha juu ya mashairi ambayo yatatuwezesha kutunga mashairi.
Dhana ya shairi
Shairi ni kipande cha maandishi kilichopangwa kwa utaratibu katika mistari. Sauti za silabi hufanana zikiwa kati au mwisho mwa mstari. Maandishi hayo yakisomwa huleta ujumbe na hisia fulani ya kimaisha.
Mpango wa maneno ya shairi, ambao huweza kuimbwa hutoa picha wazi, maana halisi na burudani ya kimuziki. Nyimbo nyingi za makabila zimepangiliwa kishairi ijapokuwa hazikuandikwa
Mashairi yana umbo ambalo huonekana kwa mpangilio wa sauti na idadi ya maneno katika mistari. Umbo hili hutofautisha shairi na tenzi. Kuna mambo kadhaa yanayotakiwa kufahamika kuhusu shairi, nayo ni:
  1. Beti – Kifungu kimoja cha shairi ambacho kina uzani sawa.
  2. Vina – Ni mwisho wa mistari ambayo huwa na silabi zenye sauti ileile mwishoni mwa sentensi.
  3. Mizani – Ni idadi zilizo sawa za silabi katika kila mstari, ubeti hadi ubeti.
  4. Kituo – Huu ni mstari wa mwisho wa ubeti. Kuna vituo vya aina tatu:Kituo cha bahari – ni mstari unaotoka mwanzo hadi mwisho bila kubadilika katika kila ubeti;Kituo cha kimalizio – ni kituo ambacho mstari wa mwisho maneno yake hubadilika ubeti hadi ubeti;Kituo nusu bahari – ni mstari wa mwisho ambao maneno yake nusu hubadilika na nusu hubaki kama ulivyo ubeti hadi ubeti.
Katika mashairi (ya kimapokeo), kila mstari lazima uwe umekamilika na ubeti uwe na maana kamili.
Vipengele vya fani katika mashairi
Vipengele vya fani katika shairi ni pamoja na:
  • Jina / anwani
  • Mandhari
  • Wahusika
  • Muundo –tathnia, tathlitha, tarbia, tathamisa, sabilia n.k
  • Mtindo – pindu, msisitizo, beti kubadilishana vina, kurudiwa kipande kizima cha mstari wa mwisho kikiwa ni chanzo cha ubeti unaofuatia.
Vipengele vya Maudhui kati mashairi
  • Vipengele vya maudhui ni pamoja na: migogoro, ujumbe, falsafa, msimamo, mtazamo, na dhamira za mwandishi.
  • Matumizi ya ushairi ni pamoja na: kuomboleza, kubembeleza, kuliwaza, kufundisha, kuburudisha, kukosoa, na kadharika.
Baada ya hapa sasa unaweza kuanza kutunga shairi lako la kwanza.

Comments

Popular posts from this blog

KISWAHILI FORM 1: FASIHI SIMULIZI

KISWAHILI Form 1 Topic 4 FASIHI SIMULIZI Fasihi simulizi ni moja kati ya tanzu za fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. Katika mada hii utajifunza na kisha utaweza kubainisha tanzu na vipera vya fasihi simulizi pamoja na ufafanuzi wake. Na pia utaweza kutofautisha kati ya kipera na kipera au kati ya utanzu na utanzu. Ubainishaji wa Tanzu za Fasihi Simulizi Tanzu za Fasihi Simulizi Bainisha tanzu za fasihi simulizi Fasihi Simulizi ni kazi ya fasihi inayohifadhiwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo kama vile; hadithi, ngoma na vitendawili. Tanzu za Fasihi Simulizi ni pamoja na hizi zifuatazo: Masimulizi/hadithi Semi Ushairi Mazungumzo Maigizo Ngomezi Ufafanuzi wa Vipera vya Tanzu za Fasihi Simulizi Vipera vya Hadithi Fafanua vipera vya hadithi SIMULIZI/ HADITHI Masimulizi ni fasihi yenye kusimulia habari fulan...

MBINU ZA KUFUNDISHIA

Mbinu za kufundishia , ni miongozo mbalimbali atumiayo mwalimu wakati wa kufundisha somo aliloliandaa kwa wanafunzi wake. Walimu wanapaswa kuamua kwa kuchagua kwa makini njia na mbinu bora za kufundishia ili wanafunzi wake waweze kujifunza kwa ufanisi. Ziko njia nyingi za kutengeneza mazingira ya mtoto aweze kujifunza na pia ziko mbinu nyingi za kufundishia. Pamoja na wingi huo tunaweza kuzigawa katika makundi makuu mawili kadri ya jinsi zinavyowashirikisha watoto katika tendo la kujifunza, ambazo tunaweza kuziita shirikishi na zisizo shirikishi . Zifuatazo ni baadhi ya mbinu shirikishi na zisizo shirikishi za kufundishia pamoja na faida na hasara zake:- Njia ya majadiliano , njia hii imekuwa ikitumika katika ufundishaji kwa muda mrefu. Katika kujadiliana mwanafunzi mmoja mmoja hupata nafasi ya mawazo aliyonayo kuhusu suala linalojadiliwa na yeye pia huweza kupata mawazo yaw engine. Katika majadiliano mwanafunzi hupata ujuzi mpya nje na ule aliokuwa nao kabla hajashiriki kat...

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI

Ushairi kama moja kati ya tanzu za fasihi inayowasilishwa katika namna zote aidha kwa lugha ya maandishi au kwa lugha ya masimulizi una mchango au nafasi kubwa sana katika kunufaisha au kustawisha maisha ya binadamu kwa kumuelimisha, kumsisimua, kutunza na kuhifadhi amali zake pamoja na kukuza na kuendeleza lugha yake kama moja kati ya vipengere muhimu maishani mwake. Ushairi kama nudhumu katika fasihi simulizi hujumuisha nyimbo, ngonjera, tenzi na mashairi yenyewe. Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au katika kumbo mbalimbli kama asemavyo Mulokozi (1996) kuwa zipo kumbo kuu tatu ambazo ni ushairi wa kijadi au kimapokeo, ushairi wa mlegezo au huru na ushairi wa maigizo. Wanazuoni wafuatao wa mashairi ya kimapokeo wametoa maana za ushairi kama ifuatavyo:- Shaaban Robert (1958:37). “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari…, mawazo, maoni na fikra za ndani zi...