UCHAMBUZI WA UTENZI WA MWANAKUPONA: MAWAIDHA KATIKA TENDI.
UTANGULIZI.
Katika uchambuzi huu wa UTENZI WA MWANAKUPONA tunatarajia kuangalia vipengele kadhaa vya uchambuzi kama vile historia fupi ya mwandishi, vipengele vya fani na maudhui, na vingine vitakavyojitokeza. Katika uchambuzi huu tutaonesha moja kwa moja nafasi ya mwanamke katika kumtunza mumewe. Hii ni kazi ya uchambuzi kwa hiyo itahusisha vipele mbalimbali vya uchambuzi. Kisha tutaonesha hitimisho na marejeo
HISTORIA FUPI YA MWANDISHI.
Mulokozi (1999) anatueleza kuwa Mwanakupona binti Mshamu Nabhany alizaliwa Pate mwaka 1810. Mwaka 1836 aliolewa na bwana Mohammed Is- Haq bin Mbarak. Lakini inasemekana kuwa alijulikana zaidi kwa jina la Mataka. Mwanakupona aliolewa na Bwanaa Mataka katika ndoa ya wake wengine watatu. Yasemekana kuwa Mataka alikuwa ni mtawala wa Siu na mpinzani mkubwa wa utawala wa waarabu huko Zanzibar. Mwanakupona alipata kuzaa watoto wawili na bwana Mataka ambao ni Mwana Hashimu bint Shee Mataka (1841-1933) na ndiye aliyetungiwa utenzi huu, na Mohammed bin Shee Mataka aliyezaliwa baina ya mwaka 1856 na 1858.
Tunendelea kuelezwa kuwa Shee Mataka alikuwa na watoto wengine watatu kwa wake wengine ambao ni Bakari alieyekufa vitani Pate mwaka 1855, Mohammed (mkubwa) ambaye ndiye aliyerithi utawala wa baba yake mwaka 1855 na kuendeleza upinzani uliokuwa umeanzishwa na baba yake dhidi ya utawala wa waarabu wa Zanzibar. Tunaelezwa kuwa baadaye Sayyid Majid, Sultan wa Unguja alimfanyia hila hadi alifanikiwa kumkamata na kumfungia katika Ngome ya Yesu, Mombasa ambako alifia huko mwaka 1868. Pia yasemekana kuwa baada ya kifo cha Mohammed (mkubwa) Omari alirithi utawala na kuishi hadi miaka ya mwanzo ya karne ya ishirini na alishiriki katika kupinga ukoloni wa Waingereza huko Kenya.
Pia yasemekana kuwa Mohammed (mkubwa) alikuwa mshairi na alitunga tungo za ILELE SIU ILELE na RISALA WA ZINJIBARI ambazo zilihusu mapambano yake na Sultani wa Unguja, na fitina za baadhi ya raia zake wa Siu. Baadaye tunaelezwa kuwa Mwanahashimu aliolewa mara mbili na kufanikiwa kupata watoto wawili ambao waliishi hukohuko Lamu. Alikuwa ni mshairi na alitunga mashairi kadhaa. Baadaye tunaelezwa kuwa kuna maafa yalimkuta bibie Mwanakupona na yaliisibu familia yake na hata aliiamua kuondoka Siu na kuhamia Lamu ambako ndiko alikotungia utenzi wake wa mwaka 1858. Inasemekana kuwa Mwanakupona aliuandika utenzi huu akiwa ni mgonjwa akisumbuliwa na maradhi ya tumbo la uzazi. Alihisi kuwa asingepona, hivyo akaamua kutunga utenzi huu ili uwe ni wosia kwa binti yake ambaye angebaki bila ya uongozi wa mama.
MUHTASARI WA UTENZI.
Kijamiii, Mwanakupona ni utenzi wa kimawaidha uliotungwa na Mwanakupona Binti Msham kwa ajili ya binti yake aliyeitwa Mwanahashimu bint Mataka mwaka 1858. Utenzi huu unaonakena kuwakilisha vyema tungo za utamaduni na maonyo ya wakati huo. Mtunzi aliutunga ili kumlenga binti yake aliyeitwa Mwana Hashimu kwa lengo la kumuonya lakini pia aligusia kwa vijana wengine wa kike wapate kuusoma utenzi huu ili nao wapate maonyo hayo (Ubeti wa 94 na 95). Utenzi huu unaonekana kuibadilisha jamii ya uswahilini baada ya kuona kuwa unafaa hasa kwa malezi ya kijadi hasa kwa watoto wa kike kwa kuwafunda. Yawezekana Jambo hili ndilo linaloufanya utenzi huu uonekane kuwa msaada wa jamii hata leo hii.
Kihistoria, tunaelezwa kuwa huu ni utenzi wa kale uliokuwa unaendana na mazingira ya wakati huo. Mwandishi aliuandika kwa kuilenga jamii ya wakati ule hasa kwa kufuata mila, desturi za jadi za wakati huo kama vile heshima ya ndoa, wanawake kuwekwa utawani, kutoonesha sura zao mbele ya watu, kumtukuza mume kama Mungu wao wa pili. Pia unaonekana kuwa ulikuwa ni utenzi wa kitabaka la utawala.
Kifasihi, UTENZI WA MWANAKUPONA ni utenzi pekee wa kishairi uliotungwa na mwanamke ambao unaonekana kuleta athari kwa waandishi wengine hata kuiga mfano wake wa kutunga tungo za kimawaidha kama vile Said Karama WASIA WA BABA, Shaaban Robert katika utenzi wa HATI NA ADILI, Zainab bint Humud, HOWANI MWANA HOWANI, UTENZI WA ADAMU NA HAWA.
FANI NA MAUDHUI.
FANI.
Senkoro (2011), anaeleza kuwa fani katika fasihi ni ule ufundi wa kisanaa anaotumia msanii katika kazi yake. Mpangilio wa vitushi, (episode) UTENZI WA MWANAKUPONA ni utenzi wenye jumla ya beti 102 ambao unaanza kwa mtunzi kumwita binti yake akaribie akiwa na wino na karatasi ili asikiilize wosia. Anasema kuwa yeye alikuwa ni mgonjwa hivyo hakupata muda wa kumpa wosia binti yake. Anamwambia binti yake kuwa aanze kwa kumtukuza Mungu wake na kumwomba rehema zake. Baada ya hapo anamwambia anataka kumpa hirizi ya kinga yake na kidani cha kujipambia. Halafu anaanza kumpa maonyo aliyokuwa ameyakusudia kama vile kuheshimu mume, kumheshimu mungu, kuwa mwaminifu, kuepuka umbeya, kushika dini na mengineyo. Hayo ni kuanzia ubeti wa (1-25).
Na kuanzia (ubeti. 26-36) mtunzi anaeleza namna mwanamke anavyotakiwa kumfanyia bwana yake. Miongoni mwa mambo hayo ni kutojibizana naye, kumpa kila anachokihitaji, kumuaga vizuri kila anapoondoka, kumpokea vizuri kila anapokuja, kumpapasa na kumpepea usiku, kumkanda mwili, kumsifia kwa watu wengine, kumwandalia chakula, kumnyoa ndevu, na kumpendezesha.
Kuanzia (ubeti 37-56), mtunzi anaonesha namna mwanamke anavyopaswa kuwa yeye binafsi yaani mwanamke aliyeolewa inatakiwa awe msafi kimwili, avae vizuri na kujipamba kila siku, aombe ruhusu kwa mumewe kabla ya kutoka na akitoka asikawie kurudi na anapotembea asijifunue buibui lake na asiongee wala kunena na mtu yeyote njiani na aridhike kila anachopewa na mumewe.
Kuanzia (ubeti. 57-66) mtunzi anamwonya binti yake namna ya kuishi na watu wote kwa ujumla, yaani awe na upendo kwa watu wote bila kuangalia hadhi zao, afanye ushirikiano na wanandugu, marafiki na watu wengine pia awasaidie wanaohitaji msaada. Na atakapofanya hivyo malipo yake yatakuwa ni mbinguni.
Kuanzia (ubeti. 67-102) mtunzi anafanya dua ndefu ya kuwaombea watu wote wakiwemo watoto wake, anajiombea yeye mwenyewe, anawaombea waislamu kwa ujumla, na kisha anamalizia kwa kuwaombea wanawake wote wauosome utenzi huu ili wanufaike nao.
Hivyo tunaona kuwa japokuwa mtunzi amejitahidi kupangilia vitushi lakini inaonesha wazi kuwa amechanganya baadhi ya beti, yaani beti ambazo zilitakiwa ziwepo mwishoni amezipeleka kati ama mwanzoni mwa utenzi, na za mwanzoni kuzipeleka mwishoni ikiwa zingepaswa kuendana na beti fanani ili kukamilisha wazo. Kwa mfano beti za 92 na 93, zilipaswa kuwekwa mwanzoni maana zina mawazo ya mwanzoni kama vile maonyo kwa ujumla, ubeti 22 na 23 zingepaswa kuwekwa kati ya ubeti wa 11na 14 ili kusisitiza suala la dini, na ubeti wa 40 na 42 zingepaswa kuwekwa kati ya ubeti wa 36 na 37 ili kumwonya mtoto wa kike kuwa na tabia nzuri hasa kwa bwana yake kwa kuwa msafi na kufanya kazi.
Matumizi ya lugha, mwandishi huyu hajatumia sana lugha ya picha kama vile sitiari, tashibiha, tashihisi, methali nahau hata vitendawili na taswira japokuwa kwa kiasi fulani anaonekana kutumia lugha ya taswira kama vile hirizi, akionesha kuwa ni kinga ya kujikingia mtu aliyepatwa na matatizo ubeti ( 8-10), kidani,kama lulu au pambo (ubeti. 40) Anasema kuwa;
Na kidani na kifungo
Sitoe katika shingo
Muili siwate mengo
Kwa malashi na dalia
Hapa tunaona kuwa mwandishi ametumia taswira ya kidani inayomaanisha kuwa ni pambo au lulu inayovaliwa shingoni.
Misamiati, aliyoitumia sio migumu sana inaeleweka japokuwa kwa kiasi kikubwa ametumia lahaja ya Kiamu na anaonekana kuimudu vyema lugha yake, lakini kwa mtu asiye mmilisi wa lahaja hiyo anaweza kupata mkanganyiko pindi anapousoma utenzi huu.
Muundo, kwa upande wa muundo mwandishi anaonekana kujitahidi kwa kiasi kikubwa kwani ametumia ushairi wa kufuata urari wa vina na mizani kwa kiasi kikubwa, na kila mshororo unaonekana kuwa na mizani 8.
Motifu, iliyojitokeza katika utenzi huu ni motifu ya msako wa peponi, yaani ile ya kumsaka Mwenyezi Mungu hasa kwa kutenda matendo mema, kutii maagizo yake pamoja na mwanamke kumheshimu mume. Mfano (Ubeti. 26-27) unasema;
26. Siku ufufuliwao
Nadhari ni ya mumeo
Taulizwa atakao
Ndilo takalotendewa
27. Kipenda wende peponi
Utakwenda dalhini
Kinena wende motoni
Huna budi utatiwa
Beti hizi mbili zinatudhihirishia kuwa Mwanakupona aliona kuwa safari ya kufika peponi ni kubwa kwani kinachotakiwa ni kujipanga ili tuweze kuepuka adhabu ya jehanamu. Anamwambia mwanaye kuwa ili kushinda hilo ni vyema kumpenda mumewe na kumtii maana huko mbinguni Mungu atamuuliza kama alimpenda na kumtii huku duniani (Ubeti.28).
Keti naye kwa adabu
Usimtie ghadhabu
Itahidi kunyamaa.
Ushujaa, wahusika wanaoelezwa katika utenzi huu sio mashujaa kama ilivyozoeleka katika tenzi zingine kama vile FUMO LIONGO, SUNDIATA, MAJIMAJI na zinginezo. Huu unaonekana kuwa ni utenzi wa kimawaidha ambao hauonyeshi ushujaa au unguli kwa sababu unatoa mawaidha mengi ya kijadi hasa kwa wanawake pamoja na binti yake. Hivyo tunaweza kusema kuwa utenzi huu haujasadifu ushujaa bali umekuwa na wahusika ambao ni binti yake anayeitwa Mwanahashimu, (ubeti .37), wanawake wengine (ubeti 94), Mungu ambaye anatajwa katika (ubeti. 5, 23, 36,72,73,82, 87 na 88) na mume (ubeti. 42, 47, 48).
Mianzo na miisho ya kifomula, mwandishi ameanza na sala au dua kama kawaida ya tendi za Kiswahili, katika sura ya kwanza (ubeti.4-7) anamwambia mwanaye aketi chini na Mungu wa rehema atasaidia katika kufanikisha jambo hilo. Mfano (ubeti.4) anasema;
Ukisa kutaqarabu
Bismillahi kutubu
Umsalie Habibu
Na sahabaze pamoya.
Pia anamalizia kwa shukrani ya kumshukuru Mungu kwa kumfanikishia shughuli nzima ya utunzi wa kazi yake na kuufanya usomwe na watu wengi ili uje kuwa nyenzo ya maisha yao. Mfano (ubeti.101-102)
101. Mola tutasahilia
Kwa Baraka za Nabia
Na masahaba pamoya
Dini waliotetea
102. Nahimidi kisalia
Kwa Tume wetu nabia
Ali zake na dhuria
Itwenee sote pia.
MAUDHUI.
UTENZI WA MWANAKUPONA unaonekana kujadili masuala ya itikadi ya kijinsia yaani yakukubali na kuheshimu ngazi za mamlaka kama zilivyo bila kuzivunja kwa kuwa ni amri ya Mungu. Hata hivyo mawazo yake yanaonekana kuwa yalitokana na vyanzo kadhaa kama vile, mafundisho ya dini ya kiislamu, yanatokana na mila na desturi za Waarabu zinazofuatwa na wenyeji wa pwani, mtazamo na ozoefu wa tabaka tawala la pwani. Mawazo yote haya yanaunganika na kutupa dhima kadhaa kama zifuatazo.
Dhima za utendi huu
Katika uchambuzi wa kazi yoyote ya kifasihi tunaona kwamba huwa na dhima mbalimbali ambazo huweza kuwa za kijamii, kihistoria na kiutamaduni. Lakini dhima hizo kwa kiasi kikubwa hutegemea muktadha na wakati wa utunzi wake. Kwa mfano utenzi huu ulikuwa na dhima zake nyingi kwa wakati ule lakini kwa sasa hauwezi kuwa na dhima ileile kwa kiwango chote kama ilivyokuwa wakati ule.
Kijamii, inaonyesha kuwa Mwanakupona aliuandika utenzi huu kwa kuzingatia tabaka lake na jamii yake. Kwani alikuwa katika jamii ya tabaka la Kifalme na hivyo dhima zake zilionekana kumsaidia zaidi binti aliyopo katika uwanja huo sio zaidi ya hapo. Kwa mfano alijaribu kuzungumzia masuala yakutojichanganya na watumwa wakati wa kazi (ubeti. 20),kuepuka wajinga wasiojichunga(ubeti.21), kuwa mwaminifu na mpenda haki,(ubeti.14)kujinyenyekeza mbele za wakubwa, (ubeti. 15) kuepuka uropokaji (ubeti.19) kumheshimu Mungu na mtumewe (ubeti .23),kumheshimu mume (ubeti .31),kuheshimu wazazi, kuwa na upendo kwa wote (ubeti61-64),kuwa mtiifu (ubeti.13), kushika dini. Pia baadhi ya dhima hizo zinaonekana kuwa mwongozo kwa watoto wa kike mpaka kwenye jamii ya leo hii, na labda ndio maana tunauona unafaa mpaka sasa. Pamoja na kugusia hayo hakujaribu kuzungumzia maswala ya tabaka la chini kama vile kulima, pamoja na maisha ya tabaka la chini kwa ujumla ila tu, anamwambia mwanaye awasaidie watu wasiojiweza mfano (ubeti.64) Anasema;
Na ayapo muhitaji
Mama kwako simuhuji
Kwa uwezalo mbuji
Agusa kumtendea
Hapa anadhihirisha wazi kabisa kuwa yeye anatoka katika tabaka la juu na kila kitu anacho.
Kihistoria, utenzi huu unatuonesha kuwa ni utenzi wa kale yaani wa miaka ya 1858 ambao ulitungwa na Mwanakupona kwa lengo la kumwonya binti yake na wanawake wengine. Ulikuwa na mashiko zaidi kwa wakati huo na kwa kiasi fulani mpaka sasa unaonekana kushika chati kwani unatoa maonyo na maadili kwa wanawake wa kisasa kama vile kuepuka umbeya, kuacha uvivu (ubeti .37), kuwa na adabu (ubeti.13), kushika dini, upendo kwa wote, wanawake kuwaheshimu waume zao pamoja waume kuwaheshimu wake zao.
Kiutamaduni pia utenzi huu unaoneka kuwa kwa kiasi kikubwa unazungumzia mambo ya kitamaduni hasa utamaduni wa kufuata mila, desturi na jadi za Waswahili, na kwa kiasi kidogo unagusia pia tamaduni za Kiarabu. Kwa upande wa Waafrika kama tunavyojua kuwa wao wana mila na desturi zao za kijadi ambazo hutokea baada ya kijana kuonekana anafikia hatua ya makuzi. Hivyo jamii huchukua jukumu la kuwafunda vijana wa kike na kiume. Kwa mfano hufundwa kuhusu mambo ya ndoa (namna ya kuishi na mume) na maisha kwa ujumla. Hata ndani ya utenzi huu tunaona hayo yakifanywa na mtunzi kwa binti yake, akimwonya juu ya mambo kadhaa ya kiutamaduni kama vile; adabu na heshima, kuepuka umbeya, kuepuka fitina, kuepuka uchoyo (ubeti.64), kuepuka uvivu (ubeti .37), kuwa msafi na kujipamba ili kufurahisha na kumvutia mume ubeti. (40-42), kutomnyima mume chochote anachokitaka (ubeti.29) na kumhudumia kitandani mfano. (ubeti.31) anasema.
Kilala siikukuse
Mwegeme umpapase
Na upepo asikose
Mtu wa kumpepea.
Funzo hili liko katika mila za ndoa kwani utamaduni wa Waswahili husisitiza sana masuala kama hayo hasa kwa kudumisha ndoa kwa kupendana na kutimiziana mahitaji mbalimbali ili kuishi kwa furaha na amani ndani ya nyumba mfano kutabasamu kwa mke kila anapomwona mume wake (ubeti.50).
Pia utamaduni wa Kiarabu ulioguswa ni kama vile; namna ya mwanamke anapovaa na kutoka nje ya nyumba yake inatakiwa aweje, mwandishi anatuonyesha kuwa Waarabu wanatamaduni zao ambazo wanazifuata na kuzitekeleza lakini kwa sasa zinaonekana kabisa kuingia katika utamduni wa waswahili na tunazifuata. Kwa mfano masuala ya kutawishwa kwa mwanamke pamoja na mavazi (ubeti 44-45), pia mwanamke anaambiwa kuwa anapotoka asiangalie wala kuongea na watu njiani, (ubeti .46) anasema
Wala sinene ndiani
Sifunue shiraani
Mato angalia tini
Na uso utie haya.
Tunaona kuwa hizi ni mila za kiarabu ambazo kwa sasa zinaonekana kuleta athari mpaka kwetu mpaka sasa.
Suala la dini, sehemu kubwa ya UTENZI WA MWANAKUPONA unaonekana kujadili zaidi kuhusu maudhui ya kidini na kusisitiza haja ya kuzingatia mafunzo ya dini ya kiislamu. Kama vile, kumtii Mungu na mtume wake (ubeti.23), kupenda na kutenda haki kama dini inavyotaka (ubeti. 12), kumtii mume na kuishi naye kwa upendo kama dini inavyotaka. (Ubeti.26-27), pia utenzi huu unatufundisha kuwa Mungu pekee ndiye anayeweza kutenda chochote unachohitaji na kama ni hivyo basi hatuna budi ya kutanguliza maombezi yetu kwake popote tunapofanya jambo fulani hata baada ya kumaliza shughuli yoyote ni vyema pia kumshukuru. Mfano huu tunauona pia kwa Mwanakupona mwenyewe ambaye alianza kwa dua na kumalizia tena na dua ubeti. (4-7, 66-102).
Falsafa ya mwandishi juu ya utenzi huu inaonekana kuwa mwanamke hawezi kufika mbinguni kama hajamtendea mume wake mambo anayopaswa kufanyiwa katika maisha ya ndoa.
Hivyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa UTENZI WA MWANAKUPONA unaonekana kuwa nguzo ya mafunzo na maonyo kwa wanawake hata wa kizazi cha sasa lakini kwa kuangalia kwa baadhi ya mafunzo ambayo yanaendana na wakati huu maana mafunzo mengi yaliyoelezwa ni ya wakati wa zamani na hayana maana kwa wakati huu. Pia utenzi huu unaonekana kumdidimiza sana mwanamke hata kutopewa uhuru wa kuweza kufanya mambo mengine ya kimaendeleo kwani unamfanya mwanamke muda wote awaze namna ya kumriwaza mume tu.
MAREJEO
Mulokozi, M.M. (1999) Tenzi Tatu za Kale. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili: Dar es Salaam.
Senkoro, F.E.M.K (2011) Fasihi.Dar es salaam. KAUTTU.
Fabulous... Just love this site. Thank you.
ReplyDeleteWoow
ReplyDeleteThanks nimeielewa Sasa
ReplyDeleteNimeelewa Sana Zaid ya sana
ReplyDeleteThis comment has been removed by a blog administrator.
DeleteMchambuzi umejitahidi Sana kuchambua vizuri lakini hujaonesha au hujachambua vizuri gani ya utenzi huu... Naomba urudie kuusoma vizuri...
ReplyDelete