Tuanze uhakiki huu, kwa kuanza na :
KIPENGELE CHA MAUDHUI
Dhamira
Hili ni wazo kuu au mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika kazi ya fasihi. Na katika diwani hii kuna dhamira kuu na dhamira ndogondogo ambazo zimejitokeza, kwa kuanza tunaanza na;
Dhamira kuu
Dhamira kuu ni wazo kuu linalojitokeza katika kazi za fasihi, na katika diwani hii, wazo kuu ni ukombozi wa jamii, sasa tuanzekuangalia ukombozi huo wa jamii, namna unavyojadiliwa katika diwani hii:
Ukombozi wa jamii
Dhamira kuu inayojitokeza katika diwani hii ni ukombozi wa jamii, mwandishi amejadili ukombozi huo katika Nyanja mbalimbali kama vile ukombozi wa kisiasa, kiuchumi na kiutamduni.
Ukombozi wa kisiasa
Kwa kiasi kikubwa mwandishi amejadili ukombozi wa kisiasa, mwandishi anaona kuwa ili jamii iweze kujikomboa kisiasa, jamii hiyo haina budi kuondokana na matatizo ya kiungozi [uongozi mbaya] uongozi ambao hauwajali wananchi zaidi ya kujali matumbo yao na maisha yao huku wakiwaacha wananchi waliowengi wakiishi maisha ya tabu na dhiki hu kundi hilo la viongozi wachache wakifaidi matunda ya uhuru, kama mwandishi anavyosema katika shairi la " Fungate ya Uhuru" ubeti wa kwanza
anaposema,
"Karamu za fahari, mabembe ya kupepea.
Na majumba mazuri, wamekwisha jijengea.
Watembea kawa magari, hivi zimewazowea." Uk.1
Katika shairi la Viongozi wa Afrika mwandishi pia anasema,
"Viongozo wa Afrika
Wanaotumia mapesa,
Wakaogelea anasa,
Nayo mitindo ya kisiasa,
Wakavamia kwa sesa.." Uk. 21
Vile vile mwandishi anaishauri jamii yake ili iweze kujikomboa kisiasa, jamii hiyo haina budi kufuata itikadi ya ujamaa ambayo mwandishi anaamini kuwa itikadi hii ni tumaini kwa wavuja jasho na wafanyakazi. Rejea shairi la ‘Ujamaa’ ubeti wa pili na tatu [uk. 30]
Mwandishi pia anaitaka jamii yake ili kujikomboa kisiasa, inatakiwa jamii hiyo kuondokana na kupiga viata ukoloni mamboleo, kama tunavyofahamu kuwa ukoloni mamboleo ni ile hali ya nchi kupata uhuru wa bendera lakini kiuchumi, kitamaduni na hata kujiamulia mambo yetu wenyewe kuwategema wakoloni au mataifa ya kimagharibi na Amerika.rejea katika shairi la "Afrika" Uk. 22-23
Masuala mengine ambayo mwandishi anayajadili katika ukombozi huu wa kisiasa ni pamoja na jamii kupinga utawala wa kidikteta unaokandamiza jamii kwa kutawala kimabavu, kama mwandishi anavyosema katika shairi la
"Viongozi wa Afrika"
"Viongozi wa Afrika, wanaotawala kwa mabavu,
Kujifanya ni washupavu,
Wao wachache ni werevu,
Na umma wote ni wapumbavu,
Wanafiki,
Wazandiki."
Katika shairi la "Maendeleo ya Umma" ukurasa wa 2-4 mwandishi anasisitiza hili la kupinga utawala wa kidekteta ili kujikomboa kisiasa anaposema katika ubeti wa nane [8]
Maendeleo ya umma
Watu kuwa na kauli
Katika zao shughuli
Vikaoni kijadili
Na mwisho kuyakubali
Maamuzi ya hali
Udikteta la!
Mwandishi naonesha njia za kuondokana na utawala wa aina hii ni kama vile, jamii kuungana na kupambana na hali hii, jamii kujitoa muhanga, kwa mfano mwandishi anaonesha haya katika shairi la "Unganeni!" anaposema;
Wafanyakazi wa Afrika, tuunganeni,
Na wakulima kadhalika, tushikaneni,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa Mapambano, yalo Marefu,
Ushindi ni wetu.
Pia rejea mashairi ya "Ningekuwa na sauti, Nikizipata Bunduki, Gorila,Afrika,Utawala, Ni vita Si Lelemama, Siku Itafika,Naona n.k" mashairi haya mwandishi anaelezea njia mbalimbali ambazo jamii ya kiafrika inaweza kuzitumia ili kujikomboa kisiasa kwa kuondoka na tawala dhalimu na za kidikteta.
Ukombozi wa Kiuchumi
Hii ni aina nyingine ya ukombozi amabao mwandishi Mohamed Seif Khatibu amelijadili katika diwani hii. Mwandishi anaonesha kuwa jamii ya kiafrika inatakiwa kujikomboa kichumi kwa wafanyakazi na wakulima kuungana kupambana na unyonyaji unaofanywa na mataifa ya Ulaya na Amerika ili kujikomboa kiuchumi, kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Afrika" ukurasa wa 22-23.
Bara la Amerika, Na Ulaya kadhalika,
"Wamestaarabika"
Kunyonya Afrika, Ni kwa mingi miaka,
Nasi tukafukarika.
Vilevile mwandishi anaonesha kuwa ili jamii iweze kojikomboa kiuchumi inatakiwa njia kuu za uzalishaji mali umilikiwe na dola/serikali na si kuwa mikoni mwa watu wachache tu, mwandishi anathibitisha hili katika shairi la "Maendeleo ya Umma" ukurasa wa 2-4 hususani katika ubeti wa tano [5] anaposema;
Maendeleo ya umma
Dola kuthibiti vitu
Vijapo nchini mwetu
Na kuwauzia watu
Toka nguo na sapatu
Pasibakishiwe na kitu
Huo usawa!
Lakini pia mwandishi anaiasa jamii yake kuwa maendeleo ya kiuchumi sit tu kuonekana kwa vitu madukani, kujaa kwa vitu maghalani, wa si vitu kuonekana kwa masoko yetu, bali ili jamii iweze kujikomboa kiuchumi maendeleo hayo ya kiuchumi ni lazima vitu hivyo vimilikiwe na wanyonge ambao ndiyo wengi katika jamii zetu, maisha ya watu wote bila kujali kipato chao, kuwa rahisi, rejea tena shairi la "Maendeleo ya Umma" ukurasa wa 2-
jamii kupinga matabaka amabayo husababisha watu wachache katika nchi za kiafrika kunufaika na rasilimali za nchi huku wakiwaacha wananchi waliowengi kuwa hoi kiuchumi, vilevile mwandishi anaitaka jamii yake kuchukua hatua kupambana na viongozi wezi, wanaondekeza maisha ya anasa na kujilimbikizia mali kuwa ni kikwazo kwa maendeleo ya kiuchumi kwa jamii na nchi husika.
Ukombozi wa Kiutamaduni
Mwandishi pia amejadili suala la ukombozi wa kiutamaduni, mwandishi anaitaka jamii yake kujikomboa kiutamaduni kwa jamii kuwa na utamaduni wa kuheshimiana na kuwa waungwana kama ambavyo utamaduni wa kiafrika unavyotutaka kuishi kwa kuheshimiana na kuwa waungwana kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Maendeleo ya Umma" ubeti wa tisa [9]
Maendeleo ya Umma
Watu kuwa waungwana
Vijakazi na watwana
Nchini kuwa hakuna
Wote kuheshimiana
Wazee hata vijana
Wote ni sawa
Tofauti na sasa katika jamii yetu inayotuzunguka ambapo watu wamekuwa si waungwana, vijana kutokuwa na heshima kwa wazee n.k
Vilevile mwandishi anaitaka jamii yake kujikomboa kiutamaduni kwa kuithamini lugha yake kwa kuwa lugha ni nyenzo muhimu sana katika ukombozi wa kiutamaduni, katika diwani hii mwandishi anaitaka jamii ya kitanzania kuwa na utamaduni wa kuithamini na kuienzi lugha ya kiswahili kwa kuifananisha mgodiau zawadi/tunu isiyokwisha, kama ambavyo anasema katika shairi la "Dafina" ukurasa wa 8-10
Paa, ni kuruka angani, kama ndege na tiara.
Paa, ni mnyama porini,ni mwenye nyingi papara.
Paa,ni kuteka mekoni, moto uwake imara.
Paa, ni toa magambani, samaki atiye sura.
Paa, pia la nyumba, kmakuti au karara.
Dhamira ndogo ndogo
Usaliti
Suala la usaliti pia limepewa nafasi katika riwaya hii, mwandishi amejadili usaliti unaofanywa na viongozi wengi wa kiafrika wanaopewa dhamana za uongozi katika nchi zao. Kwa mfano wakati wa kudai uhuru viongozi waliuaminisha umma kuwa tukijatawala wenyewe kutakuwa na usawa kwa watu wote na maisha yatakuwa mazuri kwa kila mwananchi tofauti na maisha yalivyokuwa katika tawala za kikoloni, lakini mara baada ya kupata uhuru, viongozi hao hao wakausali umma kwa kuanza kujiangalia wao, kijitajirisha wao, kuwakandamiza na kuwanyonya wananchi, kuendekeza maisha ya anasa na starehe huku wananchi walio wengi wakiishi maisha ya tabu na dhiki, Mwandishi anaonesha usaliti katika shairi La "Fungate ya Uhuru" ubeti wa kwanza anaposema,;

Vilevile katika shairi la "Tumesalitiwa!"
mwandishi anaendelea kuzungumzia suala hili la usaliti wa viongozi kwa umma anaposema;
Nikate tama?
Kwani tuendavyo hatufiki.
Vile ipasavyo, hayakamiliki.
Mambo yalivyo, ni unafiki.
Tumesalitiwa!
Lakini pia mwandishi anaonesha namna ambavyo usaliti lilivyokuwa ni tatizo kwa nchi nyingi za kiafrika, kwa mfano mwandishi anaonesha namna ambavyo viongozi wanavyozisaliti nchi zao kwa kuhongwa na mabepari bila kujali uhai wa mataifa yao, mwandishi anaonesha hili katika diwani yake katika shairi la "Viongozi wa Afrika" uk. 21-22 hususani katika ubeti wa 8 anaposema;
Viongozi wa Afrika,
Wanaohongwa na mabepari,
Kwa kuutaka utajiri,
Bila ya kujali hatari,
Nchi zao kuwa fakiri,
Majasusi,
Mafisadi.
Hivyo mwandishi anaitaka jamii yake kupambana na viongozi wasaliti kwa kuchukua hatua mbalimbali kama vile kuwakamata na kuwachukulia hatua kali, kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Nikipata Bunduki" uk. 11-12 hususani ubeti wan ne [4]
"Nikizipata shembea,
Takamata viongozi, wasaliti wa nchini,
Niwachinje kama mbuzi miiko wasoamini…"
Mashairi mengine yanayozungumzia dhamira hii ni pamoja na shairi la "Ni Vita Si Lelemama" uk. 34, "Wingu" uk. 35,
Ukigeukia katika jamii yetu, ni kweli usiopingika, viongozi wasaliti wapo, amabao wameamua kuusaliti umma kwa kuamua kujilimbikizia mali huku wanachi wakiishi maisha ya shida kwa kukosa huduma muhimu kama vile afya, elimu, maji n.k kwa sababu tu viongozi hujijali wao tu na si jamii inayowatawala na wengine kuhongwa na watu matajiri au mataifa mengine ili kuuza rasilimali za mataifa yao bila kujali hatari yoyote ile, huu ni usaliti na jamii inatakiwa kuupinga kwa nguvu zote.
Unafiki
Hii ni hali ya mtu kujifanya rafiki huku ni adui, au kutokuwa mkweli katika maneno yake na vitendo vyake, suala hili la unafiki pia limeshughulisha kalamu ya mwandishi kwa kuonesha namna ambavyo tabia ya unafiki ilivyoshamiri miongoni mwa watu tunaowaamini, kama vile viongozi wa serikali na hata viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini. Kwa mfano mwandishi anaonesha unafiki unaofanywa na viongozi wa serikali kwa kujifanya ni wafuasi wa mfumo na itikadi ya ujamaa huku wakitumia nguvu kubwa kuihubiri majukwaani ili hali matendo yao yakiwa ni ya kibepari, kama vile kujilimbikizia mali n.k. kama mwandishi anavyothibitisha hili katika shairi la "Nikizipata Bunduki" uk. 11-13 anaposema;
Nikipata mikuki,
Lazima ntawachoma, "wajamaa" wa zamani,
Mali nyingi walochuma, kwa hotuba jukwaani,
Ni dhahiri,
Watughuri, mabepari,
Matajiri,
Hubiri haziwalishi!
Vilevile mwandishi ameonesha unafiki unaofanywa na viongozi wetu wa dini, ambao madhabahuni katika makanisa ni misikiti wamekuwa wakihubiri watu kuacha dhambi kama vile wizi n.k. huku wao wakiishi maisha kama wacha Mungu kumbe nyuma ya pazia wamekubuhu kwa wizi tena hata kuwaibia waumini wao. Hili linathibitishwa na mwandishi katika shairi la "Wizi" uk.25 mwandishi anaposema;
Wizi umo;
Kanisani,
Msikitini,
Hekaluni,
Wanyang’anwao ni fukarini.
Vilevile mwandishi anaonesha namna vyombo vya dola kama vile polisi na majeshi mengine ambao jukumu lao kulinda watu na mali zao kinyume chake huwalinda wezi wanaowaibia wananchi, mwandishi anathibitisha hili katika shairi hilo hilo la "Wizi" [uk. 25] ubeti wa tano [5] anaposema;
Walinzi hawapo? La hasha!
polisi hulinda wezi,
majeshi huhalalisha wezi,
na dini zawabariki wezi.
Tukiangalia uhalisia wake haya yanayozungumzwa na mwandishi kwa jamii yetu inayotuzunguka, yana uhalisia kwani yanatokea katika jamii yetu, wapo viongozi wa dini ambao na waumini ambao kwa maneno hujifanya kama watu wema wakati matendo yao ni kinyume. Na hata vyombo hivyo vya dola katika jamii yetu, mchana wanajifanya kama walinzi wetu, usiku hushirikiana na wezi au viongozi wasiowaaminifu kuwaibia wananchi na taifa kwa ujumla, unafiki wa aina hii unatakiwa kupigwa vita.
Unyonyaji
Mwandishi hakuwa nyuma, kujadili suala la unyonyaji katika jamii yake, anaonesha namna ambavyo kundi moja huishi kwa kulinyonya kundi lingine, kwa mfano mwandishi, anaonesha namna ambavyo mataifa ya Ulaya na Amerika yanavyozinyonya rasilimali za nchi zinazoendelea hususani nchi za kiafrika na hivyo kuzifanya nchi hizo kuendelea kuwa masikini ingawa nchi hizo zina rasilimali za kutosha, mwandishi anathibitisha hili anaposema katika shairi la "Afrika" ukurasa wa 22-23.
Bara la Amerika, Na Ulaya kadhalika,
"Wamestaarabika"
Kunyonya Afrika, Ni kwa mingi miaka,
Nasi tukafukarika.
Vilevile mwandishi anaonesha namna ambavyo wakulima wakivuja jasho kwa kutumia nguvu nyingi kulima mazao mbalimbali lakini wanapovuna hayo mazao yao na kuyapeleka sokoni, huko hunyonywa kwa kwa kuuza bei ya chini thamani isiyolingana na nguvu waliyotumia kuzalisha. Hili mwandishi anathibitisha katika shairi la "Naona" uk. 41-42, anaposema;
Naona
Wanakwenda gulioni
Mazao kuyazabuni
Wanapata bei duni
Na kubaki maskini
Unyonge uleule.
Ili kuondokana na unyonyanyi wanaofanyiwa wakulima na wafanyakazi, mwandishi anawataka wafanyakazi na wakulima kote Afrika kuungana kupambana na tabaka linalowanyonya, kama mwandishi anavyosema katika shairi la "Unganeni" uk. 1-2
Wafanyakazi wa Afrika, tuunganeni,
Na wakulima kadhalika, tushikaneni,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa Mapambano, yalo Marefu,
Ushindi ni wetu.
Mashairi mengine yanayozungumzia dhamira hii ya unyonyaji ni pamoja na,
"Utawala" uk. 28-29, "Njama" uk.29,
"Wengine" uk. 24, n.k
Hata tukiigeukia jamii yetu ya leo, bado mataifa ya Ulaya na Amerika yanazinyonya nchi za kiafrika kupitia mgongo wa viongozi wasiowaaminifu, nab ado tabaka la wafanyakazi na wakulima wanaendelea kunyonywa kwa malipo yasiyokidhi mahitaji yao huku wakiwatajirisha watu wachache. Hivyo tunatakiwa kupambana kupinga unyonyaji wa aina yoyote ile kama mwandishi anavyoasa.
Wizi wa mali za umma/ufisadi
Suala la wizi wa mali za umma au ufisadi kama inavyojulikana kwa sasa linajitokeza katika diwani hii, mwandishi anajadili namna ambavyo viongozi mbalimbali wa kiafrika wanavyojitajirisha kwa kuiba rasilimali za taifa na hivyo kuzifanya nchi zetu kuendelea kuwa nyuma kiuchumi, rejea katika shairi la " Fungate " ubeti wa kwanza anaposema,
"Karamu za fahari, mabembe ya kupepea.
Na majumba mazuri, wamekwisha jijengea.
Watembea kwa magari, hivi zimewazowea." Uk.1
Dhamira nyingine zinazojitokeza ni kama vile, kupiga vita rushwa, matabaka, kujitoa muhanga, umojana na mshikamano, ukabila n.k
VIPENGELE VYA FANI
MUUNDO
Katika utanzu wa ushairi, muundo tunaangalia idadi ya mistari katika beti, kama mwandishi katika diwani yake atatumia mistari miwili katika kila ubeti, basi tutasema kuwa mwandishi ametumia muundo wa tathnia, na kama atatumia mistari mitatu kwa kila ubeti, tutaseama kuwa mwandishi ametumia muundo wa tathilitha, na mistari mine ni muundo wa tarbia na mistari mitano na kuendelea utakuwa muundo wa takhmisa.
Kwa upande wake, mwandishi Mohamed Seif Khatibu katika diwani hii, ametumia muundo changamano kwani mashairi tunayoyaona katika diwani hii ametumia miundo zaidi ya mmoja. Kwa mfano kuna mashairi ya muundo wa:
Tathnia [Mistari miwili]
Mfano wa shairi lenye muundo huu ni shairi la "Mjamzito" uk. 7-8
Ubeti 1. Mjamzito, Amelazwa "thieta"
Lazima kupasuliwa.
Ubeti 2. Chake kitoto, tumboni kinatweta,
Hawezi kujifungua.
Ubeti 3. Mwili u moto, tumbo linamkeketa,
Kwa kite anaugua.
Tathilitha [mistari mitatu]
Mfano wa shairi lenye muundo huu ni shairi la "Waja wa Mungu" uk. 27
Ubeti 1 . Dunia, vyakula hawavioni, mafakiri,
Lakini, vyakula kwao pomoni, mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu!
Ubeti 2. Duniani, wanalala majiani, mafakiri,
Lakini, wanalalaghorofani, mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu!
Ubeti 3 . Duniani, nguo mbovu matakoni, mafakiri,
Lakini, nguo tele kabatini, mabepari,
Abadani, hawa si waja wa Mungu!
Mashairi mengine yenye muundo huu ni shairi la "Fungate" [uk, 1], "Nataka
Kusema" [uk. 18], "Nia Yangu Sigeuzi" [uk. 46], "Uwapi Uzuri Wako" [UK.46-47], "Sakubimbi" [uk.44],
"Paka Shume" [uk.45], "Wewe Peke Yako" [uk .45]
Tarbia [mistari minne]
Mfano wa shairi lenye muundo huu ni shairi la "Afrika" uk. 22-23
"Bara la Amerika, Na Ulaya kadhalika,
"Wamestaarabika"
Kunyonya Afrika, Ni kwa mingi miaka,
Nasi tukafukarika."
Mashairi mengine yenye muundo huu ni pamoja na shairi la "Nahodha Mtwesi" [uk.6], "Gorila" [uk.14], "Kunguru" [uk. 26], "Ua Si Ruwaza Njema" [uk.47-48]
Takhmisa/sabilia [Mistari mitano au zaidi]
Shairi lenye muundo huu ni shairi la
"Unganeni" [uk. 1-2]
Wafanyakazi wa Afrika, tuunganeni,
Na wakulima kadhalika, tushikaneni,
Makabwela mnaosumbuka, tukutaneni,
Tujiandae kwa Mapambano, yalo Marefu,
Ushindi ni wetu.
Mashairi mengine yenye muundo huu, ni pamoja na "Dafina" [uk.8],
"Ningekuwa na Sauti" [uk.10-11],
"Utawala" [uk.28-29], "Njama" [uk. 29],
"Ladha ya Maji Katani" [uk. 35-37]
"Mkata" [uk.19], "Joka la Mdimu" [uk. 40] n.k
MTINDO
Mwandishi amatumia mtindo changamano yaani amechanganya mitindo yote ya aina mbili, yaani mtindo wa kimapokeo na mtindo wa kisasa [mambo leo].
Mtindo wa Kimapokeo
Mtindo wa kimapokeo ni mtindo unaofuata na kuzingatia urari wa vina na mizani , kuwa ni idadi ya mistari mine kwa kila ubeti na kuimbika kwa shairi. Mfano wa shairi la kimapokeo ni;
"Kuntu Sauti ya Kiza" [uk. 33
"Nyuki ni mtanashati, umbo na zake tabia,
Yeye yukila wakati, Vichafu kuvikimbia,
Mchana na lailati, Hatui kwa kukosea,
Kuntu Sauti ya Kiza, nyuki hapendi vichafu."
Shairi hilo ni la kimapokeo kwakuwa kila ubeti katika shairi hilo lina mistari mine na kila mstari umeundwa na vipande viwili vya mstari, vilevile shairi hilo lina urari wa vina na mizani kwa kila mstari una silabi kumi na sita [16] na kuna vina vya kati na vina vya mwisho, katika ubeti wa kwanza vina vya kati ni ‘ti’ na vina vya mwisho ni "a"
Mashairi mengine ya kimapokeo ni kama vile, "Mcheza Hawi Kiwete" [uk. 37-38], "Ua Si Ruwaza Njema" [uk. 47-48]
Mtindo wa kisasa
Ni mashairi yasiyofuata urari wa vina na mizani, wala halizingatii idadi ya mistari katika beti na wala si lazima kuimbika. Mfano wa shairi la kisasa ni kama vile, shairi la "Naona" [uk. 41-42]
Naona
Wanakwenda gulioni
Mazao kuyazabuni
Wanapata bei duni
Na kubaki maskini
Unyonge uleule
Ukiliangalia shairi hili utaona kuwa halina urari wa vina na mizani, na mistari yake ni vipande hivyo shairi hilo ni la kisasa kwakuwa halijazingatia kanuni za wanamapokeo. Mashairi mengine ya kisasa ni kama vile,
"Fungate" [uk. 1], "Unganeni" [uk. 1-2],
"Maendeleo ya Umma" [uk. 2-4], " Tumesalitiwa!" [uk. 5], "Haki [uk.5] n.k
MATUMIZI YA LUGHA
Mwandishi ametumia lugha sanifu ya Kiswahili yenye lahaja ya kiunguja iliyojaa lugha ya picha, taswira, misemo mbalimbali na tamathali za semi ni mbinu nyingine za kisanaa.
Lugha ya picha/taswira
Lugha ya picha iliyotumika ni pamoja na kunguru katika shairi la
"Kunguru" [uk. 26-27], tunaposoma shairi hili tunapata picha kuwa, kunguru ni sawa na viongozi ambao tuliwachagua kuondoa matatizo katika jamii kinyume chake wao ndo wakazidi kuleta matatizo badala ya kuyaondoa kama walivyofanya kunguru weusi waliopandikizwa kuondoa uchafu badala yake wao ndo wamekuwa wakileta na kujaza uchafu na kuwa kero kwa jamii, mfano katika shairi hilo mwandishi anasema,
Kunguru walisafilishwa,
Nchini wakahaulishwa,
Na kazi ikatayarishwa,
Ili uchafu kuondoshwa.
Kunguru wakabadilika,
Uchafu wao wakaweka,
Maradhi yakaongezeka,
Ni badala ya kutoweka.
Lugha ya picha au Taswira nyingine iliyotumika ni jina la kitabu lenyewe, "Fungate ya Uhuru" taswira inayojengeka hapa ni kuwa, uhuru ni kama harusi na kama tunavyofahamu katika jamii yetu baada ya shamlashamla za harusi wanaenda fungate kwa mapumziko huku wakiendelea kula na kunywa bila kujali mzigo na uzito wa wale waliofanikisha shrehe yao kwa hali na mali, hivyo mwandishi anawafananisha hao maharusi sawa na viongozi ambao mara baada ya hekaheka za uhuru viongozi mpaka sasa wako katika mapumziko yanayotokana na heka heka za uhuru huo huku wakiendekeza anasa na starehe bila kujali wavuja shajo waliofanikisha uhuru huo. Mwandishi anathibitisha hilo anaposema, katika shairi la " Fungate ya Uhuru" ubeti wa kwanza anaposema,

Taswira nyingine zinazojitokeza katika diwani hii, ni ‘paka shume’ katika shairi la "Paka Shume" [uk.45] ambayo inajenga taswira ya viongozi au watu wadokozi.
Misemo
Misemo inayojitokeza katika diwani hii ni pamoja na:
Paka shume ukurasa wa 45 katika shairi la "Paka Shume" .
Utakiona cha Mtema kuni, Katika shairi la "Nyayo" uk. 31
Umelichimba kaburi, mzima utajizika,
katika shairi la "Sakubimbi" uk. 44
Joka la mdimuni, ukurasa wa 40 katika shairi la "Joka la Mdimuni" uk. 40-41
Patashika na nguo kuchanika Katika shairi la "Joka la Mdimuni" [uk. 40-41]
Vishindo vya kufa na kupona katika shairi la "Kinyang’anyiro" [uk.43-44]
Hatwendi mrama katika shairi la
"Nahodha Mtwesi" uk. 6-7
Ni wachapa kazi, kazi ni kilimo katika shairi la "Naona" uk. 41-42
Matumizi ya tamathali za semi
Tashibiha
Ama havikamatiki ni kama jinga la moto kama katika shairi la "Maendeleo ya Umma" [uk. 2-4]
Nabaki kugunaguna, kama nyani kwenye nyika katika shairi la "Ningekuwa na Sauti" [uk.10-11]
Niwachinje kama mbuzi, miiko wasoamini katika shairi la "Nikizipata Bunduki" [uk. 11-13]
Ulinijia mapema kama ukinda yatima katika shairi la "Si Wewe" [uk. 38-39]
Ni pomoni, mbu ndani, kama ndege za vitani, katika shairi la "Mkata" uk. 19-20
Matopeni, hujazika, mithili nimo karoni,
katika shairi la "Mkata" uk. 19-20
Sitiari
Bao la mkahawani , kila mtu akalia, hapa mwandishi anamfanisha mwanamke malaya sawa na bao la mkahawani/mgahawani ambalo kila mtu hukalia, rejea shairi la "U wapi Uzuri Wako" [uk. 46-47]
Sasa jamvi la wageni, wajapo huwapokea, hapa mwandishi pia humfananisha mwanamke na jamvi/mkeka wa wageni kwa kila mgeni anayetokea yeye lazima atembee nao.
Mgodi wa Kiswahili, ni dafina isokwisha , mwandishi hapa anaifanani lugha ya kiswahili na mgodi wa madini, au kitu chenye thamani kubwa sana. Rejea shairi la "Dafina" [uk. 8-10]
Mashikoni, kibandani, vifaru vya panya ndani, mwandishi anafananisha panya na silaha ya kivita aina ya kifaru katika shairi la "Mkata" uk 19-20
Tashihisi
Na mauti yanamwita , katika shairi la
"Mjamzito" uk. 7
Nyuki ni mtanashati, Umbo na zake tabia , katika shairi la "Kuntu Sauti ya Kiza" uk. 33
Ruya, umenigutusha, ukaniamsha, usingizini, katika shairi la "Ruya" uk. 13-14
Mbinu nyingine zilizotumika ni kama vile;
Takriri
Mbinu hii inajitokeza katika shairi la
"Dafina" uk. 8-9 ambapo tunaona mwanzoni mwa kila mstari katika ubeti kuna maneno yanarudiwa rudiwa. Tazama ubeti ufuatao katika shairi hilo;
"Paa , ni kuruka angani, kama ndege na tiara.
Paa , ni mnyama porini,ni mwenye nyingi papara.
Paa ,ni kuteka mekoni, moto uwake imara.
Paa , ni toa magambani, samaki atiye sura.
Paa , pia la nyumba, kmakuti au karara.
Mgodo wa Kiswahili, ni dafina isokwisha."
Ukiangalia ubeti huo, utagundua kuwa kuwa neno ‘paa’ linajirudia rudia katika kila mstari wa ubeti, na mbinu hii imetuka katika shairi zima, shairi lingine lililotumia mbinu hii ni shairi la "Gorila" uk. 14-16 neno "gorila" linajirudia mstari wa mwanzo na mwisho kwa kila beti. Mashairi mengine ni, "Waja wa Mungu" uk. 27, sentensi,
Abadani, hawa si waja wa Mungu! Inajirudia mwishoni mwa kila beti, rejea pia mashairi ya "Kunguru" uk. 26-27, "Utawala" uk. 28-29, "Wizi" uk. 25, "Maendeleo ya Umma" uk. 2-4 n.k
Lugha ya kejeli/dhihaka
Jina la kitabu "Fungate ya Uhuru" limetumika kidhihaka, mwandishi anawakejeli/dhihaki viongozi ambao wamewasahau wananchi na kujijali wao, kuishi maisha ya anasa na starehe huku wananchi wakitaabika kuwa wako katika fungate. Rejea pia shairi la
"Fungate" uk. 1
Tafsida
Hawezi kujifungua badala ya kutumia neno hawezi kuzaa ambalo ni neno kali sana, katika shairi la "Mjamzito" uk. 7
Jina la shairi "Mjamzito" uk. 7 limetumika kitafsida kaepuka kutumia neno mimba
Vipengele vingine vya maudhui
FALSAFA YA MWANDISHI
Mwandishi Mohamed Seif Khatibu, falsafa yake anaamini katika ujamaa, anaona kuwa itikadi ya ujamaa ndiyo inayofaa kufuatwa na nchi za kiafrika ili kuleta usawa, haki na maendeleo ya watu wake, anaamini kuwa ujamaa unaweza kuondoa unyonyaji, matabaka na mambo yanayofanana na hayo katika jamii.
MTAZAMO
Mwandishi ana mtazamo wa kiyakinifu kwani anaamini kuwa matatizo yanayotokea katika jamii yake yanasababishwa na jamii yake, na mifumo iliyowekwa na watu, matatizo yote aliyoyajadili katika diwani hii mwandishi anaamini yanasababishwa na jamii, na jamii hiyo hiyo ndiyo inayoweza kuyaondoa hayo matatizo.
MSIMAMO
Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi, anaitaka jamii yake ifanye mapinduzi kuondokana na mifumo mibovu na matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii yake kama vile uongozi mbaya, tattizo rushwa, usaliti, matabaka, unyonyaji n.k na kuonesha njia mbalimbali ambazo jamii yake inaweza kuzitumia ili kuondokana na matatizo hayo, miongoni, mwandishi ni mtaka mabadiliko katika jamii.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu Fungate ya Uhuru
linasadifu yale yote yaliyomo katika diwani hii. Jina hili la fungate ya Uhuru limetumika kikejeli, kiuhalisia neno fungate, linamaana ya tafrija, burudani, mapumziko, kula na kunya na kujiliwaza au kujipumbaza baada ya heka heka za harusi na hasa maharusi wawili yaani bwana harusi na bibi harusi, lakini katika diwani hii mwandishi ana maana ya viongozi ambao mara baada ya uhuru ambao uhuru huo watu wengi walijitoa kwa hali na mali, jasho kwa damu kupambana na dhuluma, manyanyaso na ubaguzi uliokuwa unafanywa na wakoloni, viongozi waliopata dhamana ya kutuongoza wamejisahau na kuwaacha wananchi na kuamua kujilimbikizia mali, kuishi maisha ya anasa, kuwanyonya wakulima na wafanyakazi, kukumbati rushwa na ukabila na hivyo kuwa katabaka ka watu wacheche wanaofaidi matunda ya uhuru kama maharusi walio katika fungate.
Hivyo mwandishi katika diwani hii, anazungumzia kwa kiasi kikubwa namna ambavyo viongozi hao, wameusaliti umma na wao kuwa wateule wachache wanaoishi maisha mazuri na ya anasa. Hivyo jina la kitabu kwa kiasi kikubwa linasadifu yale yote yanayozungumzwa katika diwani hii. [Rejea dhamira mbalimbali.
TATHMINI YA MHAKIKI
Kufanikiwa kwa mwandishi
Kwa kiasi kikubwa mwandishi amafaulu katika vipengele vyote vya fani na maudhui, kwa mfano, kimaudhui, amefanikiwa kuonesha matatizo mbalimbali yanaikabili jamii yake na kuipa njia jamii yake namna inavyoweza kuondokana na matatizo hayo. [rejea dhamira mbalimbali]
Kifani amefanikiwa, ametumia muundo changamani jambo ambalo linaweza kumsaidia msomaji wa kazi yake kujifunza namna ya kuandika mashairi yenye miundo tofauti tofauti, pia ametumia mtindo changamani yaani hakufungamana katika mtindo mmoja tu, ametumia mitindo yote, yaani mashairi ya kimapokeo na kisasa ambayo nayo huweza kumfanya msomaji wake, kuweza kujifunza namna ya kuandika na kutunga mashairi kwa mitindo yote hiyo.
Mapungufu
Kma ilivyo kawaida huwa hakuna kazi isiyo na mapungufu, hivyo hivyo katika diwani hii kuna mapungufu mbalimbali yanajitokeza ingawa si kwa kiwango kikubwa sana, kwa mfano, baadhi ya njia ambazo mwandishi anazitoa jamii kuzitumia ili kuondokana na matatizo zinaweza kuhamasisha jamii kujichukulia sheria mikononi wakati vipo vyombo vya kisheria vinavyopaswa kufanya hivyo, mfano rejea shairi la, "Ningekuwa na Sauti" uk. 10-11, na shairi la "Nikipata Bunduki" uk. 11, pia kutumia maneno makali kama vile matakoni badala ya kutumia tafsida makalioni pia ni mapungufu mengine yanayojitokeza katika kazi hii.
Kazi ya kufanya:
Ujumbe gani unajitokeza katika diwani ya Fungate ya Uhuru?

Comments
Post a Comment