Skip to main content

SHAIRI: IWE CHUNGU IWE TAMU

Kwetu ulimi maneno,mengine ni ya ziada,
Siye twatoa misemo,na nyimbo kwenye ibada,
Ladha kwetu siyo somo,ladha kwetu siyo shida,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.


Vya maana twaviona,twanusa na kusikia,
Hizo suti za kushona,na vingi vya kuvutia,
Tulivitamani sana,tumeshindwa kufikia,
Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba.

Iwe biringanya mbichi,ama pilipili manga,
Karoti ama kabichi,ama dagaa mchanga,
Sie milo haichoshi,tunatamani kusonga,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Sie hatuna ratiba,tupatacho tunakula,
Tunachopenda kushiba,hatuchagui vyakula,
Bila soda tunashiba,tunakula kisha sala,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Kwetu hatuna jokofu,hatuchachishi viporo,
'Tabaki na yako hofu,utumbo hauna kasoro,
Kunenepa hatuhofu,leo twala kesho doro,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Si kwamba hatutamani,tamaa twaweka ndani,
Twapiga kazi jamani,siku tuwe na vyetu ndani,
Maisha hatulingani,tajiri na masikini,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Shughuli na matukio,twajua chungu na tamu,
Jaani ndo kimbilio,kama vile si timamu,
Njaa huleta kilio,hatujui neno hamu,
Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba.

Comments

Popular posts from this blog

DHANA YA MATUMIZI YA LUGHA, REJESTA, UTATA

Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika. Katika mada hii utajifunza mambo ya msingi ya kuzingatia unapotumia lugha. Utaelewa dhana mbalimbali zinazohusishwa na matumizi ya lugha kama vile rejesta, misimu, utatata katika lugha, lugha ya mazungumzo na lugha ya maandishi. Matumizi ya lugha ni namna ambavyo wazungumzaji wa lugha hutumia lugha kwa kuzingatia mila, desturi na kaida mbalimbali za jamii inayohusika. Dhima ya matumizi ya lugha Dhima kuu ya lugha ni kupashana habari, ujuzi na maarifa mbalimbali. Vilevile lugha husaidia kujenga uhusiano mwema baina ya watu. Uhusiano huo unaweza kuwa wa kijamii, kielimu, kibiashara, kihuduma, kisiasa, kiuchumi n.k. Kwa hiyo, kujua jinsi ya kuitumia lugha kama inavyotakiwa, kunasaidia kufikisha vizuri ujumbe unaotakiwa bila kuupotosha. Vilevile kunasaidia kuepuka migongano, hasa ya kijamii kwa kuwa utakuwa umetumia lugha kwa mujibu wa mi...

DHANA YA USHAIRI ILIVYOFAFANULIWA NA WATAALAMU MBALIMBALI

Ushairi kama moja kati ya tanzu za fasihi inayowasilishwa katika namna zote aidha kwa lugha ya maandishi au kwa lugha ya masimulizi una mchango au nafasi kubwa sana katika kunufaisha au kustawisha maisha ya binadamu kwa kumuelimisha, kumsisimua, kutunza na kuhifadhi amali zake pamoja na kukuza na kuendeleza lugha yake kama moja kati ya vipengere muhimu maishani mwake. Ushairi kama nudhumu katika fasihi simulizi hujumuisha nyimbo, ngonjera, tenzi na mashairi yenyewe. Ushairi wa Kiswahili waweza kuainishwa katika tanzu au katika kumbo mbalimbli kama asemavyo Mulokozi (1996) kuwa zipo kumbo kuu tatu ambazo ni ushairi wa kijadi au kimapokeo, ushairi wa mlegezo au huru na ushairi wa maigizo. Wanazuoni wafuatao wa mashairi ya kimapokeo wametoa maana za ushairi kama ifuatavyo:- Shaaban Robert (1958:37). “Ushairi ni sanaa inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na tenzi. Zaidi ya kuwa na sanaa ya vina, ushairi una ufasaha wa maneno machache au muhtasari…, mawazo, maoni na fikra za ndani zi...

NOTES ZA USHAIRI

USHAIRI     NI    NINI ? Shaaban Robert katika uandishi wa ushairi ameandika Tenzi na mashairi ya kimapokeo. Tenzi : Ni aina ya mashairi ya kimapokeo wenye sifa zifuatazo: Kimaudhui ; Ni utungo wenye maudhui yanayosimulia kwa urefu tukio fulani maalum. Waweza kuwa wasifu wa mtu au jambo la kihistoria. Mfano; S. Robert ameandika utenzi wa vita vya Uhuru, ameeleza kuhusu historia. Pia katika Mapenzi Bora, ameeleza kuhusu sifa za mapenzi bora. Utenzi ni utungo wa pili kati tungo za ushairi zenye beti nyingi. Utungo wa kwanza unaoongoza kuwa na beti nyingi kuliko zote katika ushairi ni Tendi. Lakini hapa tutaangazia tenzi zaidi. Utenzi hauna mizani nyingi aghalabu mizani nane, hauna mshororo bali una nusu mshororo/kipande mstari. Vilevile katika utenzi kipande mstari hakigawiki. Pia katika kipande mshororo kuna vipande vinne kwa kila ubeti. Mistari mitatu ya kwanza huwa na vina vyenye urari na kipande mstari cha mwisho/cha nne huwa...