MIE KUWA MWANAMKE
Ni fahari na heshima,shukrani kwa muumba,
Najivunia daima,sitozijali kasumba,
Tangu zama za ujima,mama nguzo ya nyumba,
Mie kuwa mwanamke, ni thawabu kubwa sana.
Timamu hata kilema,ninayo kubwa thamani,
Nilizaliwa na mema,na pendo kubwa moyoni,
Mgonjwa na siha njema,bado ninayo amani,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Nazaliwa kuwa mama,mlezi aliye bora,
Niwe mwana mkulima,tajiri ama fukara,
Daima nitasimama,sitotishwa na bakora,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Zimepita nyingi zama,zenye mila za karaha,
Siwezi waza kuhama,kuitafuta furaha,
Nitatumia hekima,hadi kuipata raha,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Mila ziletazo homa,ni vyema kuzikomesha,
Kama italetwa ngoma,iwe siyo ya kukesha,
Pia nataka kusoma,na wanetu kusomesha,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Sitaki kuwaza nyuma,nyakati zilizoliza,
Tuliponyimwa kusema,kigoli hata ajuza,
Pia tuliachwa nyuma,marufuku kuongoza,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Mwana akiwa na homa,mama wa kwanza kujua,
Akihitaji huduma,mama atamuambia,
Mwanzo na mwisho wa juma,mama amuangalia,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Sasa mama asimama,kuwaongoza wengine,
Pia anafanya hima,awahi kazi nyingine,
Si kusoma si kulima,hafanyi ili mumwone,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Siri ya nyumba ni mama,mle ama mkalale njaa,
Anayo ile huruma,hadi baba ashangaa,
Kiazi atakichoma,mle akigaagaa,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Mama mama mama mama,jina tamu kwa mtoto.
Hata mbu akimwuma,tadhani kachomwa moto,
Dole mwiba ukichoma,utasikia muito,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Maziwa kapewa mama,na uchungu maksudi,
Kapewa nyingi dhima,mama kapewa juhudi,
Kumsifu sitokoma,kumweshimu sina budi,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Nikome hapa kwa leo,kujivuna kuwa mama,
Kwenu mama wa kileo,tunzeni hadhi ya mama,
Mama ninakupa vyeo,najivuna kuwa mama,
Mie kuwa mwanamke,ni thawabu kubwa sana.
Comments
Post a Comment