Skip to main content

SHAIRI: NENO LANGU KWAKO



Uchungu wake mzazi,mlenzi ama rafiki,
Moyo unakufa ganzi, ndugu anapofariki,
Imekuwa  wanafunzi, na kuleta taharuki,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Zile ndoto zake mama,ama baba kwa mwanaye,
Jana zimeshasimama,na kuisha hatimaye,
Ni ajali siyo homa, leo hii hawanaye,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Vimezimishwa vipawa,walivyobeba watoto,
Bila ya kugusa dawa,imekuwa kama ndoto,
Ni kama imezinduwa,ShauriTanga na moto,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Walimu waliopotea,na wale waliowapenda,
Dereva katangulia,kaenda na alowapenda,
Shule hakujatulia,myoyo yabaki kudunda,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Pole kwa wanafunzi, mloguswa na hili,
Pole kwa mama wazazi,muweza kustahimili,
Pole pia kwa walezi, leo mwaona miili,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Pole kwa watanzania,nchi imetikisika,
Hili kulishuhudia,myoyo inatetemeka,
Arusha yote walia,wanetu kuwakumbuka,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Naandika kama baba, kaka na mwalimu wenu,
Kwenu darasa la saba,mlofiwa na wenzenu,
Tuwaombee kwa baba,awapokee wenzenu,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Na wale wadogo zao,waliwaacha shuleni,
Pole na ziende kwao, nguvu mtiwe yoyoni,
Msiwaze yale yasiyo, wamekufa ajalini,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Laweza mkuta yeyote, si fukara si tajiri,
Hivyo tuyafute yote, kudhani yasiyojiri,
Na tuwafariji wote, hima bila kusubiri,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Pia niwaase jambo, kwa watumao zao picha,
Hayafai hayo mambo, ni watu siyo mchicha,
Ama tuzishike fimbo, ndipo mtaja zificha,
Neno langu dogo kwao,poleni kwa hili gumu.

Kaditama nasimama,poleni kwa mama zao,
Ninaumia mtima,kuwazia baba zao,
Naingiwa na huruma,juu ya walimu wao,
Mwisho nabaki kusema,wapo naMungu wao.

Comments

Popular posts from this blog

NOTES ZA USHAIRI

USHAIRI     NI    NINI ? Shaaban Robert katika uandishi wa ushairi ameandika Tenzi na mashairi ya kimapokeo. Tenzi : Ni aina ya mashairi ya kimapokeo wenye sifa zifuatazo: Kimaudhui ; Ni utungo wenye maudhui yanayosimulia kwa urefu tukio fulani maalum. Waweza kuwa wasifu wa mtu au jambo la kihistoria. Mfano; S. Robert ameandika utenzi wa vita vya Uhuru, ameeleza kuhusu historia. Pia katika Mapenzi Bora, ameeleza kuhusu sifa za mapenzi bora. Utenzi ni utungo wa pili kati tungo za ushairi zenye beti nyingi. Utungo wa kwanza unaoongoza kuwa na beti nyingi kuliko zote katika ushairi ni Tendi. Lakini hapa tutaangazia tenzi zaidi. Utenzi hauna mizani nyingi aghalabu mizani nane, hauna mshororo bali una nusu mshororo/kipande mstari. Vilevile katika utenzi kipande mstari hakigawiki. Pia katika kipande mshororo kuna vipande vinne kwa kila ubeti. Mistari mitatu ya kwanza huwa na vina vyenye urari na kipande mstari cha mwisho/cha nne huwa...

Mpangilio wa sura katika utafiti

MADHARA YA MATUMIZI YA KARATASI ZA OMR KATIKA KUJIBIA MITIHANI. Na LEONARD RENATUS, 0759392855 Tasinifu hii ni kwa Ajili ya Kukamilisha Masharti ya  kukamilisha  Stashahada ya elimu ya msingi Chuo cha Ualimu Marangu. SURA YA KWAZA UTANGULIZI Utafiti huu umekusudia kuchunguza madhara na changamoto zitokanazo na karatasi za OMR  katika kujibia mitihani inayotolewa na baraza la matihani Tanzania (NECTA) . Katika sura hii utafiti huu utaangalia vipengele vifuatavyo:- Utangulizi. Usuli wa tatizo. Tamko la utafiti. Lengo kuu la utafiti. Malengo mahsusi yautafiti. Umuhimu wa utafiti. Mawanda ya utafiti. Tafsiri za istlahi zilizotumika 1.2    USULI WA TATIZO OMR ni kifupi cha maneno ya Optical Mark Reader ni mashine ambayo inatumika kusahihishia karatasi za wanafunzi waliofanya mitihani. Kwa hapa Tanzania karatasi hizi hutumika katika kujibia mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa darasa la saba . Njia hii ya kusahihishia miti...

MBINU ZA KUFUNDISHIA

Mbinu za kufundishia , ni miongozo mbalimbali atumiayo mwalimu wakati wa kufundisha somo aliloliandaa kwa wanafunzi wake. Walimu wanapaswa kuamua kwa kuchagua kwa makini njia na mbinu bora za kufundishia ili wanafunzi wake waweze kujifunza kwa ufanisi. Ziko njia nyingi za kutengeneza mazingira ya mtoto aweze kujifunza na pia ziko mbinu nyingi za kufundishia. Pamoja na wingi huo tunaweza kuzigawa katika makundi makuu mawili kadri ya jinsi zinavyowashirikisha watoto katika tendo la kujifunza, ambazo tunaweza kuziita shirikishi na zisizo shirikishi . Zifuatazo ni baadhi ya mbinu shirikishi na zisizo shirikishi za kufundishia pamoja na faida na hasara zake:- Njia ya majadiliano , njia hii imekuwa ikitumika katika ufundishaji kwa muda mrefu. Katika kujadiliana mwanafunzi mmoja mmoja hupata nafasi ya mawazo aliyonayo kuhusu suala linalojadiliwa na yeye pia huweza kupata mawazo yaw engine. Katika majadiliano mwanafunzi hupata ujuzi mpya nje na ule aliokuwa nao kabla hajashiriki kat...