Skip to main content

Posts

SHAIRI: SIKU HII MWAKA JANA

Haikuwa ijumaa,japo tarehe ni kumi, Sikuwa nimezubaa,kama nazuru Mikumi, Ilikuwa ni furaha,amani tele moyoni, Siku hii mwaka jana,ilikuwa safi sana. Mapema nawasha simu,ninapokea salamu, Natafakari salamu,naganda kama sanamu, Wa ukweli na muhimu,kanitumia salamu, Siku hii mwaka jana,ilikuwa siku safi. Tabibu wa moyo wangu, wengi mnamfahamu, Natamani awe kwangu,ngoja ashike elimu, Namweka moyoni mwangu,nafasi hii adimu, Siku hii mwaka jana, ilikuwa siku bora. Alimpigia mama,mama alozaa chema, Nitampenda daima,hata leo ninasema, Mama aloleta chema,ni’pe nini huyu mama, Siku hii mwaka jana ,ilikuwa siku njema. Yupo wapi huyu wangu,simuni hapatikani, Nimepata na machungu,mwenzangu haonekani, Mpenzi urudi kwangu,nifurahi duniani, Leo ya mwaka jana,tofauti kubwa sana.

SHAIRI: WAKATI RAFIKI MWEMA

WAKATI Huyu ni rafiki mwema,hana unafiki katu, Wala hahofu kusema,kwa miti hata watu, Liwe baya liwe jema,kuficha hatothubutu, Wakati rafiki mwema,hajawahi kuongopa. Hajawahi kuogopa,ama kuona aibu, Hohe hae kwa vibopa,wakati kwao jawabu, Ya ukweli atakupa,hata kwa kukuadhibu, Wakati rafiki mwema,husema kweli daima. Husema kweli daima,tena bila kuamuru, Uwe chali uwe wima,wakumbuka ya Kaburu, Hasemi ufanye hima,ama jifanye kunguru, Wakati rafiki mwema,daima namthamini. Daima namthamini,namfanya mali yangu, Afanya nijiamini,sihofii mwisho wangu, Kaskazi na kusini,kwa weusi na wazungu, Wakati rafiki mwema,haujui unafiki. Haujui unafiki,aje akulishe sumu, Anapenda urafiki,hata ukimdhulumu, Na usipomuafiki,wala hatokulaumu, Wakati rafiki mwema,atakupa uatakacho. Atakupa utakacho,wala usimuabudu, Iwe wazi na kificho,mpole ama bandidu, Hawezi kupa kisicho,mwema akupe kibudu, Wakati rafiki mwema,wakati ni kiongozi. Wakati ni ...

SHAIRI: MAMA YANGU VUMILIA

MAMA YANGU VUMILIA Nilijua simulizi,haziwezi kutokea, Wakuota hao wezi,leo ninashuhudia, Kuvumilia siwezi,mama namsaidia, Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi. Baba alipofariki,najaribu kukumbuka, Hakupigwa na mkuki,mafua yalimshika, Namengine sikumbuki,najua wayakumbuka, Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi. Maneno waliongea,kuwa wewe wahusika, Kila mara nasikia,eti mali wazitaka, Ila ninavyokujua,mamangu hukuhusika, Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi. Shangazi kakuvamia,wale ng'ombe eti wake, Shemejio nasikia,eti wewe wake mke, Leo umetimuliwa,nyumba baba sio yake, Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi. Leo eti tumepanga ,ziko wapi zile hati, Wanakutishia panga,eti mali huzipati, Wifi zako wanachonga,eti upige magoti, Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi. Mie darasa la tano,mama naona wateswa, Siji kwenye mikutano,juzi nilikoswa koswa, Wanitishia sindano,nile vilivyotokoswa, Mama yangu vumilia,mola yupo hakutupi. MOLA AWAPIGANIA,MSICHOKE KUMWABIA

SHAIRI: IWE CHUNGU IWE TAMU

Kwetu ulimi maneno,mengine ni ya ziada, Siye twatoa misemo,na nyimbo kwenye ibada, Ladha kwetu siyo somo,ladha kwetu siyo shida, Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba. Vya maana twaviona,twanusa na kusikia, Hizo suti za kushona,na vingi vya kuvutia, Tulivitamani sana,tumeshindwa kufikia, Iwe chungu iwe tamu, cha msingi ni kushiba. Iwe biringanya mbichi,ama pilipili manga, Karoti ama kabichi,ama dagaa mchanga, Sie milo haichoshi,tunatamani kusonga, Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba. Sie hatuna ratiba,tupatacho tunakula, Tunachopenda kushiba,hatuchagui vyakula, Bila soda tunashiba,tunakula kisha sala, Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba. Kwetu hatuna jokofu,hatuchachishi viporo, 'Tabaki na yako hofu,utumbo hauna kasoro, Kunenepa hatuhofu,leo twala kesho doro, Iwe chungu iwe tamu,cha msingi ni kushiba. Si kwamba hatutamani,tamaa twaweka ndani, Twapiga kazi jamani,siku tuwe na vyetu ndani, Maisha hatulingani,...

SHAIRI: KAMA MNATAKA MALI

Myaka kumi imepita,tangu uache wosia, Mema mengi tumepata,baba sitokuchukia, Leo hii nakufwata,najua utasikia, Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni. Zama ile tulipata,ila leo ni shughuli, Leo shamba kulipata,uwe una hela kweli, Wabunge wanayapata,ama wale wenye mali, Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni. Shule niliikamata,lakini kazi sioni, Hata miti nikikata,mnunuzi yu mashambani, Faida siji kupata,labda nifike sokoni, Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni. Chochote huwezi pata,usipo weka mbolea, Hiyo mbolea kupata,mazao yanyong'onyea, Nauongeza ukata,shambani kutegemea, Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni. Kaka wamemkamata,eti shamba kavamia, Japo kwako tulipata,baba ulituachia, Mweupe amekamata,weusi wawatimua, Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni. Kuna habari napata,kaburi kulifukua, Wapi haki nitapata,niweze kuwazuia, Nikipinga wakamata,nami ndani kunitia, Mali haipo shambani,nitaifwata bungeni.   NAAMINI UMEKUMBUKA MBALI

SHAIRI: MUNGU GANI MTESAJI

Kila siku twasikia, kuna watu wameua, Wengine wajisifia, shule wakizivamia, Binafsi ninaumia, pia ninawachukia, Mungu gani atesaye, mie hapo nina shaka. Pande za Naijeria, boko wanajinafasi, Mataifa kwingilia, washajiita mabosi, Wale watu wanalia, na kujiona na mikosi, Mungu gani atesaye, mie hapo nina shaka. Walianza makanisa, sasa wameenda shule, Watu kweli wametesa, mie ninawapa pole, Nini sasa wamekosa, jamani mabinti wale, Mungu gani atesaye, mie hapo nina shaka. Wajiita waslamu, jamani hawaogopi, Kweli umwagaji damu, wapi wao wamekopi, Nipeni hiyo elimu, kaka kweli hawongopi, Mungu gani atesaye, mimi hapo nina shaka. Poleni ninyi mabinti, mungu awape imani, Mlipo mlipige goti, mkaomba kwa imani, Hao hawataki noti, bali kuvunja imani, Mungu gani atesaye, mimi hapo nina shaka. Dini zote zinapinga, mambo hayo kutokea, Husein utaniunga, kama sitowakosea, Pia nitoe ujinga, siyo kwa kunizomea, Mungu gani atesaye, mimi hapo nina shaka. Mshindwe boko haramu, mfanyayo tumechoka, Nawaping...

SHAIRI: MBELE YETU NYUMA YAKO

Kisikia jina lako,nachowaza kuimba, Sisahau nyimbo zako,tangu kale twaziimba, Za kusifu chama chako,na kifo uliziimba, Mbele yetu yuma yako,Kapteni pumzika. Poleni wana Songea,na Mbinga alikotoka, Pole kwa watanzania,mwenzetu ametutoka, Sasa tunakulilia,nyimbo tutazikumbuka, Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika. Poleni na wanachama,Mwenzenu katangulia, Kaimba nyimbo za chama,nani atawatungia, Msije waza kuhama,kisa nyimbo kusikia, Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika. Ulitunga za wenzako,nani atakutungia, Leo hupo peke yako,wengi tunakulilia, Nasi tunafwata huko,wewe umetangulia, Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika. Kikutana na mwalimu,mwambie twamtamani, Mwambie yote muhimu,usimfiche jamani, Mwambie wanashutumu,heri zama za zamani, Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika. Na ukimwona Balali ,mkae mpige soga, Mwambie halisi hali,milioni ni ya mboga, Watu tuna ngumu hali,sema tumezidi woga, Mbele yetu nyuma yako,Kapteni pumzika. Kaditama ninagota,machozi yananishinda, Nahisi kama n...