Skip to main content

Posts

Showing posts from June, 2018

SHAIRI: NI TAA YA AFRICA

Yang'aa kila dakika, na kuburudisha moyo, Wachache waaliofika, umewatoka uchoyo, Yeyote atamwalika, akaliwazike moyo, Hii taa ya labuka, kaiweka hapa kwetu, Ni kama kaisimka, na miale    yake butu, Haitakuja zimika, wala kuja shika kutu. Kama mtu anacheka, meno yake ya    kung’aa, Siku jua likiwaka, waweza ukazubaa, Wengi wameweweseka, kuiona hii taa. Ulaya na Amerika, sifa zake zasikika, Wametamani kufika, nao wakasuuzika, Wachache waliofika,wamependa Afrika, Nami nilihamanika, awali nilipoona, Homa iliyonishika, walai sikuiona Kweli niliweweseka, ile taa kuiona. Ndoto zilikamilika, kwa watu nilijivuna, Kuishika nilitaka, japo ipo juu sana, Nguvu ziliongezeka, kila nilipoiona. Picha ndani nimeweka, wanangu waje ziona, Yeyote akizitaka, nitampa kuziona, Na yeye nitamtaka, aende haraka sana. Twende bila ya kuchoka, ili iwe kumbukumbu, Hata wao wakifika, wasitwone mambumbumbu, Waijue Afrika, si bara la mbumb...

HAPPY BIRTHDAY TO YOU

MUNGU AKUPE HEKIMA Miaka mingi imepita,tangu uziache nepi, Hekima umezichota,na kuyaacha makapi, Na mengi umeyapita,sijui myaka mingapi, Mungu akupe hekima,kaka yangu Tumsifu. Kama vile jina lako,Mungu wetu twamsifu, Mema yote yaje kwako,na ujazwe utukufu, Pongezi za ndugu zako,kamwe zisije kukifu, Mungu akupe hekima,kaka yangu Tumsifu. Mama amepata mwana,mwana mwema naamini, Hasemi mtundu sana,bali unajiamini, Wewe kaka ndiwe shina,nduguzo twakuamini, Mungu akupe hekima,kaka yangu Tumsifu. Baba anajivunia,kuwa nawe kila siku, Kwa watu kujisifia,atamani uwe huku, Kakangu unatulia,huna papara za kuku, Mungu akupe hekima,kaka yangu Tumsifu. Mwisho njoo kalamuni,wataka vitu jamani, Wakutaka hadithini,ubuni picha jamani, Wasema uje ubuni,ukuze yako thamani, Mungu akupe hekima,kaka yangu Tumsifu

SHAIRI: NMPE NINI MAMANGU?

Alin i lea mapema,kabla ya kuona jua, Ninamheshimu mama,kweli nimemsumbua, Hadi leo nasimama,na kuongea najua, Mama nitakuheshimu,umefanya mengi kwangu. Usiku haukulala,mie waniangalia, Waja kujua hujala,wengine wamesinzia, Mie nikigalagala,shuka lako nafunua, Mama ninakushukuru,sijui nikupe nini. Mama wewe unapika,mie kukaa sipendi, Mama yangu umechoka, mie kulia  hupendi, Mama umeshughulika,mama wewe ni mshindi, Mama wewe ni shujaa,mola anakutambua. Baba karudi usiku,wewe wamfungulia, Kanywa pombe wamshuku,ila hujamnunia, Huko amekula kuku,wengine kanunulia, Mama umevumilia,ushindi utakujia. Leo baba hanywi pombe,na pia akusifia, Kimwona ana kikombe,maziwa anajinywea, Kikumbuka usiombe,baba yangu atalia, Mama nikulipe nini,ishi nami siku zote. Mama unachechemea,ulipigwa wanambia, Kweli sikutegemea,mama unavumilia, Mungu wamtegemea,muumba waniambia, Mama umebarikiwa,mbinguni tapokelewa. Si kwamba nakusifia,baba nimemchukia, Yeye pia kanilea,siwezi kumchuk...

SHAIRI: KUMBUKUMB YA HAYATI MORINGE SOKOINE

LEO UNGEKUWA NANI? Sasa miongo mitatu,wajina hatukuoni, Wanalalamika watu,kama wewe hawamwoni, Kuvaa vyako viatu,katu haiwezekani, Leo ungekuwa nani,Moringe wa sokoine, Wengi wasema raisi,wa muungano wetu, Eti nawe ungeasi,kukiacha chama chetu, Angekuona raisi,utunge katiba yetu, Leo ungekuwa nani,Moringe wa sokoine. Alokufwata monduli,tunaambiwa fisadi, Chamani hawamjali,yuko bize na miradi, Ilikuua ajali,kukukosa ilibidi, Leo ungekuwa nani,Moringe wa sokoine. Nimefika morogoro,ulipopata ajali, Kule kuna mogogoro,leo ardhi mali, Ninapatwa na kihoro,kuhusu yako ajali, Leo ungekuwa nani,Moringe wa sokoine. Nitakuja kutazama,mahali ulipolala, Kisha nende Butiama,nyerere alipolala, Moyoni inanichoma,sijakuona mahala, Leo ungekuwa nani,Moringe wasokoine. Najuta sijakuona,mie wale wa tisini, Nimepewa lako jina,nalitumia shuleni, Kwenye picha nakuona,nimetunza chumbani, Ulazwe pema peponi,Moringe wa jina wangu......

SHAIRI: U WAPI UJITOKEZA

Nakukumbuka kwa jina,kisa mama,alikwita, Si Jojina Saraphina,Sarah pia aliita, Mora moja nilikwona,siku kwenu ninapita, Uwapi ujitokeze,walisema upo Dar. Nilibadili na njia,kisa kwenu kupapita, Jina lililipatia,kumbe nawe ulipita, Wenyeji nawasumbua,hadi mwizi wananita, U wapi ujitokeze,walisema upo Dar. Walijua twajuana,hata jina nikakwita, Sikuwa makini sana,japo moyo ulipwita, Nilijua ningekwona,nikirudi nakukuta, U wapi ujitokeze,walisema upo Dar. Kwa yeyote ajuaye,alipo wangu muhibu, Aseme alipo yeye,kila swali nitajibu, Katoka Njombe yeye,mtoto wa baba bubu, U wapi ujitokeze,walisema upo Dar. Rangi maji ya kunde,urefu wa wastani, Nywele lazima upende,kope hadi natamani, Jino la mbele upande,na kamwanya ka thamani, U wapi ujitokeze,walisema upo Dar. Kama umeshaolewa,Sarah sema nitambue, Nijuwe nimechelewa,ili nisikusumbue, Mwenzako ni muelewa,sema moyo uamue, U wapi ujitokeze,walisema upo Dar. Kama bado njoo kwangu,sina mwingine banati, Hutoupata uchungu,mwenyewe tapiga goti...

SHAIRI: NISEME NINI UJE KWANGU

Kila nikifikiria,ninashindwa kuamua, Sawa ningevumilia,ila penzi lasumbua, Kipi sijamwambia,pendo langu kulijua, Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu. Neno nimeshachelewa,lanifanya nikose nguvu, Hasa ninapogunduwa,kisa ni uvumilivu, Ni kweli hakuelewa,ishara zangu na wivu, Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu. Sasa nina taabika,na pendo langu hewani, Si mchezo nateseka,kasema lirudi ndani, Nashindwa hata kucheka,sipo tena furahani, Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu. Rafiki niseme nini,huyu mtu aje kwangu, Najua haniamini,atesa fikira zangu, Mwambie aniamini,mawazo yarudi kwangu. Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu. Mwambie napenda Mori,sina utani kwa hili, Leo mie sina gari,kwenye gari siyo mbali, Nikikosa nina sori,ya kizungu na kiswahili, Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu. Pia mwambie ukweli,wengi wanamtamani, Hawajui yake hali,wao wapenda kimini, Tatizo la wake mwili,wakijua hataamini, Sijui niseme nini, huyo mtu awe wangu. Wengi nime...

SHAIRI: NAJUA NIPO SALAMA

Mama asante sana,pole kwa magumu yote, Ninajua twafanana,kuliko viumbe vyote, Siwazi tutagombana,ukinifanya vyovyote, Nipo mikono salama,asante mama mpenzi. Najua umeteseka,kuumwa na kutapika, Pia ulisonononeka,pia ulisikitika, Moyoni ukaniweka,mama hukutikisika, Nipo mikono salama,asante mama mpenzi. Marafiki ulikosa,wengi walipukutika, Waliona kama kosa,wala hukusikitika, Na hukufikiri posa,huruma ulijivika, Nipo mikono salama,asante mama mpenzi. Bibi alinung'unika,kuona mama walia, Uoga hukujivika,kweli ulivumilia, Hujafa hujaumbika,moyo uliuambia, Nipo mikono salama,asante mama mpenzi. Mwili ulipukutika,afya ikanyong'onyea, Uoga ukafunika,huku ukiniombea, Chakula hakikulika,mama ukanitetea, Nipo mikono salama,asante mama mpenzi. Niliihisi faraja,ulipokuwa na baba, Lilibomoka daraja,hukupunguza mahaba, Nikawaza mama naja,wapi yupo wangu baba, Nipo mikono salama,asante mama mpenzi. Ile sauti ya baba,ilinifanya...

SHAIRI: ULIPENDE JINA LAKO SITAMANI LA MWENZAKO

                JINA Mie alinipa baba,na leo nimelipenda, Hata angenita zoba,singemwona aniponda, Maana lililobeba,ndiyo yeye kaipenda, Ulipende jina lako,sitamani la mwenzako. Eti lile maarufu,nami nitafanania, Kaliona uchafu,mama alokupatia, Nawe uwe maarufu,wengine kuwavutia, Ulipende jina lako sitamani la mwenzako. Mie langu nalipenda,popote nitalitaja, Hata wakija niponda,eti walone kioja, Na kamwe siji kukonda,watachoka kuningoja, Moringe ninalipenda,japo simjui Morani...

SHAIRI: ZAIDI YA KUTOKULA

Habarini marafiki,mlofunga hongereni, Nitakuwa mnafiki,nikijifanya sioni, Siyo ishara ya dhiki,bali mwongozo wa dini, Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo. Wagonjwa na wengineo,mlioshindwa kufunga, Myafanye megineyo,itakavyo yenu funga, Sio kucheka wenzio,eti yule hakufunga, Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo. Wewe usiye husika,naomba acha makwazo, Sije mtu kwazika,wewe ukawa ni chanzo, Mtu dini kaishika,kwako liwe kubwa funzo, Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo. Na humu mitandaoni,si sehemu ya dhihaka, Eti nani simuoni,siyo lazima kwandika, Si mtafute simuni,siyo humu kuanika, Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo. Pia ule unafiki,kujifanya umefunga, Waenda kwa marafiki,kuharibu yako funga, Mola hilo haafiki,ni bora usingefunga, Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo. Liombeeni taifa,msisahau dunia, Tuyaepuka maafa,mola atawasikia, Pia wale walokufa,huko naijeria, Zaidi ya kutokula,funga ina mengi mambo....

SHAIRI: NAOMBA KUFAHAMISHWA

Kamezuka kamsemo,kuhusu hizi siasa, Naomba nipewe somo,ili nisije kukosa, Siyo ya sasa michomo,kila siku yanigusa, Kuwa rangi ya kijani,ushamba na umbulula? Kijiweni wasakamwa,bila ya kupewa hoja, Na madole utachomwa,uonekane kiroja, Na mjinga utaonwa,bila hoja hata moja, Ujanja kuwa antena,kivipi muniambie? Wewe bado ni mbumbubu,chama gani walipenda, Siasa siyo kabumbu,kijani dhambi kupenda, Chafanya kuwa ka mbu,kila siku tunakonda, Washindwa kunishawishi,matusi yatanivuta? Utajitwisha uhuni,kwa njia utumiayo, Nayo lugha ya kampeni,siyo zinivutiayo, Matusi kutia ndani,hilo hamtii choyo, Hakuna neno lingine,hadi ukatia tusi? Wala si sera ya chama,nahisi hawa wahuni, Hawana kadi ya chama,hawaendi vikaoni, Watakiharibu chama,kuitwa ni cha wahuni, Huwezi kumshawishi,bila kumdhalilisha? Mie napenda siasa,siyo kulibeba jimbo, Ndugu zangu nawaasa,yaacheni majigambo, Ntajitenga na siasa,sipoacha haya mambo,   KITAKA ASIWE NJANO,MSHAWISHI SI MATUSI.

SHAIRI: NI KIPELE AMA JIPU CHANGA

Kama ndiko kufanana,ni zaidi ya mayai, Unaweza kugombana,jibu lako kulidai, Si urefu si upana,kasoro huing'amui, NI KIPELE JIPU CHANGA,WALIMU NIAMBIENI. Wapo walopata sifa,kudai ni jipu changa, Nasi wasaka marifa,twashindwa kipi kulonga, Vichwa vinapata nyufa,fikra zikijigonga, NI KIPELE JIPU CHANGA,WALIMU NIAMBIENI. Wengine ni kaupele,kovu lake halidumu, Wala huhitaji shule,wala siyo jambo gumu, Hutotoa ukelele,kukamua siyo sumu, NI KIPELE JIPU CHANGA,WALIMU NIAMBIENI. Huenda likawa jipu,tusubiri tukajua, Sije sema chupu chupu,jipu lingejiotea, Na msindi tumpe supu,jibu akilipatia,   NI KIPELE JIPU CHANGA,WALIMU NIPENI JIBU. Jipu huliacha kovu,kovu kubwa la kidonda, Kama macho ni mabovu,tapapasa ukipenda, Ama kwa wako uchovu,uliza acha kuponda, NI KIPELE JIPU CHANGA,WALIMU NIAMBIENI. Wengine ni kaupele,kovu lake halidumu, Wala huhitaji shule,wala siyo jambo gumu, Hutotoa ukelele,kukamua siyo sumu, NI KIPELE JIPU C...

SHAIRI: BILA WEWE SI KITU

Hii dunia si kitu, bila wewe amini, Si utu siyo mtu, kufika yako thamani, Si jiwe wala    msitu, cha kukuzidi ni nini? Bila ya uwepo wako,dunia tabeba deni. Tangu haujazaliwa, deni lilionekana, Dunia ilidaiwa , kulipa lazima sana, \hapana kudhulumiwa, dhuluma hushindikana, Bila ya uwepo wako,dunia itadaiwa. Siku waliona jua,mbingu na nchi zilicheka, Siyo kuja kuungua, bali ni kuneemeka, Wewe muhimu tambua, hili ichwani weka, Bila ya uwepo wako,dunia itadaiwa. Pia wewe ni mzuri, mzuri mzuri sana, Nikiuandika uzuri, nitaandika sana mbona, Sauti na sura nzuri,na rangi ing’aayo sana, Bila ya uwepo wako, dunia itadaiwa. Mama namsifu sana, ndugu na jamaa zako, Mola asifiwe jana, leo na kesho yako, Na nani walingana, hayupo mahali pako, Bila ya uwepo wako,dunia itadaiwa. Nini kitachokuliza,na kujitoa thamani? Nani hatokuliwaza, kufanya ujiamini? Na nini utachowaza, hadi useme kwa nini? Bila ya uwepo wako,dunia itadaiwa. Hi...